Habari

TUNACHOJIFUNZA WAISLAMU KUTOKA VURUGU LA ZANZIBAR

Awali ya yote tunatanguliza pole kwa ndugu zetu wote wa Kiislamu waliosibiwa na matokeo ya vurugu lililotokea karibuni Zanzibar. Imma walioathirika moja kwa moja au kwa mbali kama kukamatwa, kuteseka kwa vishindo vya mabomu na madhara mengine ya kisaikolojia. Wajibu wa kufarijiana kwa Waislamu ni suala letu kisheria, kwa kuwa umma wetu ni umma mmoja, na anapodhurika Muislamu mmoja kutokana na qadhia fulani, lazima athari zake ziwaguse Waislamu wote.Kama alivyotubainisahia Mtume wetu SAAW.
“Mfano wa Waumini katika kupendana kwao, na kuhurumiana kwao na kuamiliana kwao kwa upole ni mfano wa kiwiliwili kinaposibiwa na maumivu mwili mzima hupata maumivu” (Imewafikiwa na wote)
Pia Allah Ta’ala anasema:
وَاخْفِضْ جَنَاحَكَ لِلْمُؤْمِنِينَ (الحجر: 88
“Na wainamishie bawa lako ( la huruma) kwa Waumini”(TMQ 15:88)
Baada ya kutoa mkono wa faraja kwa matokeo na natija ya vurugu hilo. Sasa ni wajibu kuangalia kwa kina na kwa umakini mafunzo na ibra inayopatikana katika tukio hili. Hatukusudii kunyoosha kidole wala kufanya uadui kwa yoyote, bali dhamira ni kutoa mafunzo kwa lengo yafasiriwe kivitendo na kujisahihisha kwa ikhlasi kwa ajili ya Uislamu wetu hususan ikizingatiwa kwamba sisi ni Umma mmoja mtukufu uliobeba mfumo mtukufu wa kumkomboa mwanadamu, na wenye malengo maalumu na njia maaalumu kutoka kwa Allah Ta’ala kuyafikia malengo hayo.
Kwa kuanzia, matukio ya vurugu yalianzia kutokana na kutiwa mbaroni kwa idhilali Ustadh Mussa Juma na jeshi la Polisi wakati akiwa katika Msikiti wa Biziredi usiku wa kuamkia siku ya Jumapili tarehe 27 Mei 2012. Alinyakuliwa kijanja na askari kanzu waliokuwa wamevalia kana kwamba ni waswalihina. Walimsomba, kumuingiza garini na kumrundika mahabusu. Baada ya muda mfupi, taarifa za kukamatwa kwake zilienea miongoni mwa Waumini kama moto katika nyika kavu. Na hapo Waislamu wakaanza kukusanyika kituo cha Polisi Madema wakidai kuachiwa kwa ustadh huyo. Kuanzia hapo tena na kuendelea ndipo vurugu zikashtadi na kuendelea kwa siku kadhaa. Kinachodhihirika hapa ni namna Waislamu walivyokuwa na hisia juu ya dini yao na kuhisi thamani ya matukufu ya kidini/ alama za dini (sha’air). Matukufu ya Uislamu ni mengi kuanzia kitabu cha Quran, Mtume SAAW, miezi mitukufu, misikiti, masheikh na maustadh wa dini hii tukufu nk. Hatukatai wapo waliokuwa na msukumo wa ‘kiuaswabia’ zaidi, lakini waliowengi kwa upana wake walisukumwa nafsini mwao na hisia ya kidini na tuliweza kusikia ‘takbir’ na ‘tahlil’ nje ya kituo cha Madema, wakati Waislamu wakipinga vikali kukamatwa kwa Ustadh huyo. Huu ni wajibu wa kidini na jambo zuri ambalo tunamshukuru Allah Ta’ala kuwamo ndani ya vifua vya Waislamu walio wengi. Umma wetu unahitaji kufinyangwa nalo kwa upana zaidi na kutanuliwa ufahamu huu kwa upeo. Ili wakati wote uwe tayari kulinda, kutetea na kuhifadhi alama zote za dini yetu ikiwemo Quran, Mtume, misikiti ikiwemo Misikiti mitakatifu nk. Au kwa upana wake kuutetea Uislamu kikamilifu katika kiwango cha kimfumo. Allah anasifu kitendo hicho aliposema:

ذَلِكَ وَمَنْ يُعَظِّمْ شَعَائِرَ اللَّهِ فَإِنَّهَا مِنْ تَقْوَى الْقُلُوبِ (الحج: 32
“Ndio hivyo! na anaeadhimisha alama za Allah, basi hayo ni katika uchaji wa moyo”
(TMQ 22: 32)
Pili, Kuwepo kwa hisia nzito na nishati thabiti kwa umma wa Kiislamu katika kusimama kidete kupinga udhalilishaji wa Waislamu. Fikra hii ndiyo iliyomsukuma Mtume SAAW kuzuia udhalilishaji wa mwanammke wa Kiislamu uliotendwa na mayahudi wa Bani Qainuqaa, na ndio msimamo ulioshikiliwa na Makhalifa baada yake. Hali hii inadhihirika sio tu hapa Zanzibar bali Waislamu ulimwengu mzima. Vuguvugu lilioanzia Kaskazini mwa Afrika na kuendelea nchi za Mashariki ya Kati kama Yemen, Bahrain na kupamba moto ndani ya Syria ni kielelezo cha dhati cha nishati ya umma huu katika kupinga dhulma na udhalilishaji. Nishati hii ni suala la kimaumbile na kihistoria. Waislamu ndio waliokuwa mstari wa mbele katika kupambana na wakoloni. Na kimsingi katika biladi za Waislamu mapambano hayo yalishtadi zaidi. Kwa mfano, Tanganyika viongozi kama Abushiri, Bwana Kheri na wengineo walikuwa mstari wa mbele katika harakati za mapambano dhidi ya wakoloni licha ya kuwa baadhi ya harakati hizo zilikuwa na mapungufu yake, na hatimae baadhi yake kutekwa nyara na makafiri kwa niaba ya wakoloni. Nishati waliyonayo Waislamu ni kutokana na ukweli wa maumbile ya mfumo walioubeba wa Kiislamu, ambao una fikra ya ubwana (kuwa juu), na uimara kuanzia aqeeda yake na misimamo yake yote ambayo huzalisha nishati hiyo yenye nguvu na kujiamini katika kukabiliana na dhulma na kila kitendo cha udhalilishaji.
Tatu, katika vuguvugu hili licha ya kuwemo waliojifunga na thaqafa ya Kiislamu kwa kiasi Fulani, lakini lazima tukiri kwamba wapo wengi waliosukumwa na suala moja tu la ‘uaswabia’ wa kupigania ‘ uzanzibari’. Watu hao ni katika wizi, wazinifu, walevi nk. wasiojali kabisa dini wala uchaji Mungu. Kwa maneno mengine, katika vuguvugu hili watu hawakufungwa kwa lengo moja na thaqafa moja ya Uislamu, bali wamefungamanishwa zaidi na suala la ‘uzanzibari’ ambalo ndilo kauli mbiu kuu katika mkondo wote wa matukio haya. Jambo hili ni hatari kwa namna mbili. Kwanza, fikra ya kulingania ‘uzanzibari’ ni fikra ya aswabia ambayo ni haramu Kiislamu. Na pili kuwemo watu wengi ambao wamekosa thaqafa ya dhati ya kiislamu hupelekea kutukia matukio mbalimbali kinyume na Uislamu ambayo ni hatari, na ambayo huwapa mwanya na fursa maadui kuipaka matope haiba ya Uislamu na Waislamu kwa jumla.
Nne,baada ya vurugu hizi kulidhihirika taasisi zinazojinasibu na Uislamu na baadhi ya wanaojivisha maguo ya usheikh lakini kimsingi ni maadui wa wazi wa Uislamu. Kwa wao wakati Uislamu unaposibiwa na misiba kama kutukanwa Mtume SAAW, kuchomwa Quran Karim, kuuliwa, kudhulumiwa Waislamu au kupata msiba wowote, watu hao hubakia kimya cha mfu! Lakini leo katika tukio la kuchomwa makanisa, matukio ambayo taasisi za kiislamu zimekanusha kuhusika. Masheikh hao na taasisi hizo kwa jazba na hamasa wanalaani na kuwa kifua mbele. Hatusemi kwamba tunaunga mkono kuvunjwa makanisa, bali tunakosoa mtazamo potofu wa taasisi hizo na baadhi ya Masheikh wa aina hii. Hivi wao wanaumizwa zaidi kudhurika makafiri kuliko kudhurika Waislamu wenzao?
Tano, kulidhihirika upole na unyenyekevu mkubwa kutoka kwa viongozi wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar kuwafanyia viongozi wa makanisa. Licha ya makasisi hao kuonyesha ubabe wa waziwazi. Upole huo ulidhihirika wakati wa mazungumzo, kuyapatia makanisa yao ulinzi, Raisi kudiriki kuwaita wakiristo ‘ndugu zetu’ katika mkutano wake na waandishi wa habari na karibuni kutangazwa na serikali ya Zanzibar kwamba makanisa yatapewa hati miliki kikamilifu. Hii ni kutokana na maumbile ya mfumo wa kidemokrasia, licha ya kuwa unashikilia misimamo ya kuitenga dini na mambo ya utawala/usekula, lakini kimsingi upo karibu zaidi na dini za kikafiri kuliko Uislamu. Hata Waislamu wakijipendekeza vipi kwa mfumo huu bado nafasi ya dini za kikafiri itabakia kuwa juu kwa kuwa makafiri ni mila moja. Na lau Uamsho na wengineo wangeufahamu ukweli na uhalisia huu wa mfumo wa kidemokrasia wasingejitia kibarua cha kujipendekeza kwao, wala kuwafanyia hizo wanazoita dua kwa ajili ya viongozi wanaotawala kwa utwaghuti.
Sita, kudhihirika kukosekana dira ya kweli, muelekeo na malengo thabiti ya mfumo wa Kiislamu katika vuguvugu hili, tangu awali kufikia kujiri vurumai lililotokea karibuni na hadi leo vuguvugu hili linaloendelea. Hapa lazima tukumbushane kwamba suala la ulinganizi wa Kiislamu lazima lijengwe juu ya ufahamu kwamba lengo lake kuu ni kuutawalisha Uislamu wote katika maisha. Na katika kufikia lengo hilo ni wajibu kupitia njia/manhaj iliyowekwa na sheria, na sio kutumia mbinu za haramu kama kulingania fikra ya uaswabia/ ubaguzi kama inavyodhihirika katika vuguvugu hili. Mambo hayo lazima yaambatane pia na upeo na uweledi wa kuelewa siasa za kimataifa na utambuzi wa malengo ya madola ya kibepari katika biladi za Kiislamu, kwa lengo la kujiepusha na mitego yao kuwafedhehi na kuonesha uovu wa sera zao kwa Umma ili kulinda maslahi na haiba tukufu ya umma wetu. Kinyume na hivyo, harakati zisizojengwa juu ya ufahamu sahihi na kushikamana na njia ya Kiislamu humalizikia kutekwa nyara na wenye ajenda za kisekula, kupoteza muelekeo na kutoleta natija yoyote ya kimsingi. Hatari zaidi huvunja moyo umma, baada ya umma kudhihiri kufanyiwa usaliti katika kuyafikia malengo na matarajio waliyokuwa nayo.
Vuguvugu hili lazima tukiri kwa ikhlasi limekosa muelekeo na dira sahihi ya Kiislamu na kugubikwa katika pembe zote na fikra haramu na ya hatari ya uaswabia wa kujilabu na kujinasibu mahala unapotoka au kuzaliwa. Fikra ambayo ni haramu kwa dalili za kukata ndani ya Uislamu.
Katika muhadhara uliofanyika Msikiti wa Mbuyuni tarehe 29 Mei 2012 siku chache baada ya machafuko, Uamsho walitoa kauli ya kukumbushia msimamo wao ambayo wameshaisema mara nyingi:
“Mheshimiwa IGP sisi madai yetu hatutaki muungano, madai yetu sisi tunataka Zanzibar yetu, njia ipo ya kura ya maoni lakini waheshimiwa serikalini wametia pamba, kwani kuna dhambi gani kuulizwa wazanzibari kama tunataka au hatutaki muungano?
“Tunatoa salamu kwa wawakilishi wetu na tunatoa salamu kwa rais wetu Dk. Shein kwamba wazanzibari wanataka kupewa fursa na heshima yao, tunataka tuwe huru na tunataka uhuru wetu ambao umetajwa katika katiba, sisi tumekuja kwa utaratibu wetu maalumu sisi hatutaki madaraka tunataka tuulizwe tu kama tunataka muungano basi halafu tunawaacha wengine waendelee na uongozi wao hatuna tatizo”
Si hivyo tu, Ustadh Mussa Juma katika muhadhara uliofanyika hapo hapo Msikiti wa Mbuyuni Ijumaa tarehe 8 Juni 2012 aliwaagiza Waislamu wasilinunue gazeti la ‘Changamoto’. Kwa sababu linainasibisha jumuiya ya Uamsho na suala la kuanzisha dola ya Kiislamu Zanzibar. Kitu ambacho kwa mujibu wa Jumuiya hiyo si katika malengo yao.
Kwa hivyo, ukiangalia kwa makini kauli za Jumuiya hii na mwenendo wake kwa ujumla utaona licha ya kushindwa kuelewa kwa udhati waqia/hali halisi ya suala la muungano kuwa unatokamana na mataifa makubwa, pia wameshindwa kutumia njia ya Kiislamu kulitatua, lakini hata lengo la vuguvugu lenyewe si la Kiislamu, licha ya kujivisha guo la Kiislamu. Uamsho wamepigwa na butwaa, wanataka waonekane wana malengo ya Kiislamu, ilhali wanakataa ajenda ya Kiislamu, na njia wanayoitumia si ya Kiislamu. Cha kushangaza! pia wanapoambiwa ni kundi la kisekula huruka na hawakubali. Ilhali huo ndio ukweli ulivyo. Kwa sababu usipobeba ajenda ya Kiislamu huwa umebeba ajenda isiyokuwa ya Kiislamu.
Yafaa Uamsho waelewe kwamba hatukatai kwamba muungano umejaa dhulma na matatizo. Na lazima ulete dhulma na matataizo kwa kuwa fungamano lililofungamanisha muungano huu si la Kiislamu. Lakini cha msingi kuelewa ni kwamba, muungano ni tawi la tatizo na dhulma, na sio msingi wa tatizo. Msingi wa tatizo na dhulma zote ukiwemo muungano huu ni mfumo batil wa kibepari ambao ndio uliozalisha muungano huu, na kuzalisha dhulma nyengine zote. Mfumo ambao nchi zetu changa zimelazimishwa na mataifa makubwa kuubeba na kutekeleza. Hata hivyo, watawala katika nchi zetu katika kutekeleza kwao, nao huwa wana dhima na huingia katika makosa mbele ya Allah Ta’ala kwa kutabikisha mfumo batil na kumakinisha sheria ambazo si za Kiislamu. Sasa kichekesho kinakuja, Uamsho kwa upande mmoja wanaonesha dhulma ya muungano na mashaka yake ambayo tunayakubali, lakini kwa upande wa pili wanawatakasa na kuwapaka mafuta viongozi wanaotabikisha sera za mfumo wa kibepari uliozaa muungano, na ndio viongozi hao hao wanaotabikisha sheria za kikafiri ikiwemo kuulinda muungano. Jee Uamsho hawajui kwamba tamko lililokuja ndani ya Quran kukemea na kuonesha uovu wa watawala wasiotawala kwa sheria za Kiislamu ni tamko la ‘man’ ( مَن) likiwa na maana ya ‘yoyote’ hata akiwa Muislamu. Aya hizo zinasema:
وَمَنْ لَمْ يَحْكُمْ بِمَا أَنزَلَ اللَّهُ فَأُوْلَئِكَ هُمْ الظَّالِمُونَ (المائدة: 45
“Na wowote wasiohukumu kwa yale aliyoyateremsha Mwenyezi Mungu basi hao ndio madhalimu”(TMQ 5:45)

وَمَنْ لَمْ يَحْكُمْ بِمَا أَنزَلَ اللَّهُ فَأُوْلَئِكَ هُمْ الْفَاسِقُونَ (المائدة: 47
“Na wowote wasiohukumu kwa yale aliyoyateremsha Mwenyezi Mungu basi hao ndio mafasik”(TMQ5:47)

Basi vipi Uamsho wanaacha hukmu sahihi ya Kiislamu na kutanguliza akili na matamanio. Aya hizi ni qatwii- dalalah zenye dalili ya kukata hazina maana zaidi ya moja.
Aidha, yafaa Uamsho wakumbuke kwamba Tanzania ina miamala/ mahusiano mitatu. Kuna muamala wa serikali ya Zanzibar kwa raia wa visiwa vya Zanzibar. Kuna muamala baina serikali ya Muungano na serikali ya Zanzibar, na kuna muamala wa serikali ya muungano kwa wakaazi wa Tanganyika. Msingi wa miamala yote hii mitatu ni mfumo haramu na batil, kwa kuwa inatokamana na msingi mmoja wa mfumo wa kibepari chini ya mataifa makubwa ya kikoloni na kikafiri hususan Marekani. Viongozi katika nchi zetu kama viongozi wengine katika nchi changa, wao ni wasimamizi wenye kupokea maelekezo na maagizo tu kwa mujibu wa maslahi ya mataifa hayo. Kwa hivyo, unaposema unaondoa muamala uliopo baina ya serikali ya muungano na serikali ya Zanzibar, yaani kuvunja Muungano, na badala yake mambo ya Muungano kuikabidhi serikali ya Zanzibar ambayo nayo ni kijitawi kilichosimama juu ya msingi ule ule wa kibepari na uwakala wa mataifa makubwa, kimsingi hukutatua tatizo, bali umejidanganya mchana! na kudanganya umma. Kwa kuwa ulichofanya wewe ni kuondoa usimamizi wa mahusiano haya tu kwa msimamizi mmoja wa mfumo wa kibepari na kumkabidhi msimamizi mwengine. Na hiki ndicho kinachodhihirika katika vuguvugu hili kwa mujibu wa kauli za viongozi wao kama tulivyozinukuu.
Mabadiliko ya Kiislamu lazima yawe ni ya kimsingi (radical) na sio udanganyifu wa kidemokrasia, wa kuondoa sura fulani na kuibakisha nidhamu ile ile. Au kuondoa kijitawi fulani cha ubepari na kuubakisha msingi wa mfumo kama ulivyo. Au kubadilisha mwizi ama fisadi mmoja wa eneo moja na kumkabidhi majukumu fisadi na mwizi mwengine wa eneo jengine. Bali mabadiliko ya kweli ni kuondowa mfumo mzima katika mzizi wake na kuweka mbadala, na wala sio kupakapaka mafuta mfumo wala watawala wanaolinda mfumo huo. Na hilo linawezekana na ndio wajibu kulifuata kwa sababu ndivyo alivyofanya kiongozi wetu Mtume SAAW.
Saba, lazima tujifunze kwamba makafiri daima watabakia kuwa maadui zetu na kamwe si marafiki kwetu. Inapowasibu misiba na majanga Waislamu, hawaonekani viongozi wa kikiristo kuleta ujumbe wala kutoa kauli kali kama inavyodhihirika katika tukio hili. Tumeshuhudia kuchomwa moto Quran, kukashifiwa Allah Ta’ala kwa kuandikwa jina lake tukufu katika gunia la kukanyagia miguu na mkiristio hapa Zanzibar, kutekwa nyara mtoto aliyesilimu kutoka mikononi mwa Waislamu, bila ya kusahau majanga kama vile kuzama Mv. Spice kuuliwa watu Pemba katika mandamano nk. Utaona katika majanga ya Waislamu viongozi wa kikiristo hubakia kimya sio cha aliezimia bali cha mfu kamwe!
Nane na mwisho, baada ya kumalizika vurugu kulifanyika kikao kilichohusisha waziri wa mambo ya ndani, Mkuu wa Polisi, wahusika wa Serikali ya umoja wa kitaifa Zanzibar, baadhi ya viongozi wa dini ya Kiislamu Zanzibar, mabalozi wa nje kama Marekani, Norway nk. Jambo hili linadhihirisha kwamba ajenda ya muungano na ajenda zetu nyengine ziko chini ya usimamizi wa madola ya kibepari. Na kwa hakika wao ndio wanaopanga na kupangua kila ajenda katika nchi zetu. Kwanini ikiwa suala ni muungano baina ya Tanganyika na Zanzibar katika mgogoro wake washirikishwe mabalozi wa nje? Jee Marekani inapokuwa na matatizo baina ya Jimbo lake moja (state) na jimbo jengine, nchi zetu hushirikishwa katika utatuzi wa mgogoro huo kama hivi inavyofanya Marekani nchini mwetu? Au jee Uingereza katika mzozo wake mkubwa na Ireland ya Kaskazini, nchi ambayo ni mdau wenzake wa muungano wao unaoitwa United Kingdom, jee kuna siku Tanzania ilishirikishwa katika mchakato wa amani baina ya kikundi cha IRA kinachotaka kuitenga Ireland na muungano huo? Hii maana yake mataifa hayo makubwa ndio wadau wakuu wa kuamua mustakbali wa nchi zetu. Licha ya kuwa tunadai tuko huru na tunajisimamia mambo yetu wenyewe. Kimsingi masuala yetu yote likiwemo suala la kura ya maoni ya kuwa na serikali ya umoja wa kitaifa Zanzibar, zoezi lake liliratibiwa na Marekani kwa udhamini wa nchi za Jumuiya ya Ulaya.
Hivyo, ni wajibu kwa umma wetu wakiwemo Uamsho kutanua upeo, kwa kuziangalia qadhia mbali mbali kwa upana katika kiwango cha kuhusisha athari na maslahi ya mataifa makubwa katika nchi zetu changa. Na sio kuyaangalia mambo katika kiwango finyu juu juu bila ya kuhusisha mataifa ya kibepari mbayo ndiyo leo yanayotawala dunia. Tukumbuke kwamba katika kuutatua mzozo wowote katika utatuzi sahihi wa Kiislamu hulazimu kukhalifu ajenda, sera na matakwa ya mataifa haya ya kikafiri na kikoloni. Basi jee utawezaje kutatua kiudhati kama huna dola thabiti yenye nguvu na inayojitegemea?
Na ndio maana sheria ya Kiislamu inatuwajibisha tujifunge kufanya ulinganizi wa kurejesha tena dola kubwa moja ya Kiislamu (Khilafah) ikianzia katika nchi kubwa za Kiislamu, halafu iziunganishe ardhi zote za Kiislamu kuwa kitu kimoja. Na kitu hicho kinawezekana na ndio maana kikaletwa katika sheria, kwa kuwa sheria haiamrishi kitu kisichowezekana. Dola hiyo pekee ndiyo itakayoweza kufanya ukombozi wa kweli ulimwenguni kote.

Tagsmakala
Share: