Habari

Uamuzi wa Baraza Kuu ni sahihi

Sunday, 08 January 2012 13:16

Keneth Goliama

KATIBU Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharrif Hamad ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar(SMZ) jana alitinga kwenye mkutano wa chama chake huku akiwa kwenye msafara wa magari ya serikali kinyume cha matumizi ya magari hayo.

Mkutano huo uliofanyika katika viwanja vya Manzese Bakrhesa, Dar es Salaam ambapo Maalim Seif alifika eneo hilo saa 10:20 jioni akiwa kwenye msafara wa magari zaidi ya sita, yakiwemo ya serikali likiwemo alilokuwa amepanda.

Msafara huo uliongozwa na pikipiki na magari ya msafara wa viongozi ya Jeshi la Polisi.
Kwenye mkutano huo ambao Maalim Seif alitumia muda mwingi kujibu tuhuma zinazotolewa na Hamad Rashid, ulinzi ulikuwa mkali huku mwanasiasa huyo amezungukwa kila upande na polisi na walinzi wa Usalama wa Taifa.

Mbali na ulinzi huo, pia vijana wa CUF maarufu kama ‘Blue Guard’ waliimarisha ulinzi kwenye eneo hilo.Akiwa sambamba na viongozi wengine wa chama hicho, Maalim Seif aliponda kauli zinazotolewa na baadhi ya wanasiasa baada ya chama hicho kumvua uanachama Hamad, huku akifafanua kuwa utaratibu huo ulifanywa kwa mujibu wa katiba ya chama hicho.

Bila ya kufafanua ni vigogo gani, alisema kuwa baadhi ya vigogo wa Serikali walimkalisha chini Hamad Rashid na kumweleza ubaya wa kuzungumza hovyo hovyo lakini mbunge huyo hakutaka kuwasikiliza.

“CUF sio mali ya mtu wala watu lazima kila mtu afuate sheria hata kama ni mimi na Lipumba (Mwenyekiti wa Taifa) na hata muziki wa taarabu hauimbwi hivi hivi, wanasheria na taratibu zinazo waongoza,” alisema Maalim Seif.

Pamoja na kushirikiana na CCM kuunda serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar, Maalim Seif alikikijeli chama hicho akisema ni cha kihuni akikihusisha pia Chadema.

“CUF sio chama cha kihuni kama kilivyo CCM na Chadema,” alisema alidai vinashindwa kuchukua uamuzi mgumu wa kuwatimua uanachama makada wake wanaokiuka katiba waziwazi.

Alimkejeli Hamad kuwa katika Bunge lililopita alikuwa anatumwa na chama hicho kuwasilisha hoja za msingi bungeni lakini alikuwa akiogopa kuziwasilisha.Alidai kuwa Hamad alikuwa kibaraka wa Chadema kwa kumpatia aliyekuwa Mbunge wa Karatu, Dk Wilbroad Slaa pamoja na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, hoja za CUF.

Maalimu Seif alidai kuwa kitendo cha kuhamisha hoja za CUF kwenda kwa wapinzani wao, kilisababisha chama hicho kuporomoka na na kukijenga Chadema.

Tendwa apondwa
Katika mkutano huo Maalim Seif pia alimponda Msajili wa Vyama vya Siana nchini, John Tendwa ambaye alipinga kitendo cha NCCR-Mageuzi na CUF kuwavua uanachama wabunge wao, akisema kuwa ni kuwanyima haki wapiga kura katika majimbo yao.

Alisema kuwa kauli zinazotolewa na Tendwa, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Benson Bana pamoja na watu wa kada mbalimbali kupinga hatua iliyochukuliwa na chama hicho kumtimua Hamad, ni unafiki.

Alisema kuwa Tendwa anajidhalilisha kwa kuwa yeye ndio mpokeaji mkuu wa Katiba za vyama vya siasa na kumshauri kuwa kama aliziona zina kasoro, alitakiwa azikosoe kabla ya kuzipitisha.

Alisema kuwa alidhani kwamba Tendwa ataipongeza CUF kwa kuisimamia katiba yake vizuri, kinyume chake anataka chama hicho kiendelee kuvunja katiba hiyo.

“Namshangaa sana Tendwa , anachotaka mimi sikielewi kabisa. Nilidhani atatusifu kwa kuwa tumefuata sheria za nchi kumbe anataka tuendelee kuvunja katiba, hilo haliwezekani, asahau kabisa,”alisema Maalim Seif.

“Kama Tendwa anataka Hamad abaki CUF basi akamshauri bosi wake ambaye ni Rais Kikwete abadili katiba ya nchi ili nchi iwe na mgombea binafsi, Hamad kafukuzwa uanachama sio ubunge” alisema Maalim Seif.

Alisema alipoachia ubunge Rostam Aziz hakunung`unika matumizi ya pesa nyingi ya zaidi y ash 19 bilioni, lakini kwa Hamad Rashid imekuwa nongwa.

Spika wa Bunge
Maalim Seif alisema Spika wa Bunge, Anne Makinda ameshapewa barua ya kufukuzwa uanachama Hamad kama ataamua kumlea ni hiari yake.

Kuhusu Mahakama

Maalimu Seif alisema chama chake hakijapokea barua yeyote kutoka mahakamani kuhusu pingamizi la kumtosa Hamad.

Hamad alivyotimuliwa
Zaidi ya robo tatu ya wajumbe wa Baraza Kuu la Chama Cha Wananchi (CUF), walipitisha azimio la kufukuzwa uanachama Hamad Rashid na wenzake watatu.

Uamuzi huo wa Baraza Kuu la CUF ulikata mzizi wa fitina wa hatma ya Hamad Rashid na washirika wake hao kisiasa ndani ya chama hicho, baada ya kuibuka mvutano wa muda mrefu kati yake na uongozi wa juu.

Mvutano huo uliochomoza zaidi baada ya Hamad Rashid kutangaza kumng’oa Maalim Seif, ulisababisha umwagaji damu katika tawi la Chechnya Kata ya Manzese, baada ya kutokea mapambano kati ya walinzi wa ‘Blue Guard’ na mashabiki wa mbunge huyo wa Wawi.

Mbio za Hamad Rashid na washirika wake zilikwaa kisiki baada ya kikao hicho cha Baraza Kuu kilichoketi Zanzibar, kubariki mapendekezo ya Kamati ya Utendaji ya chama hicho iliyoongozwa na Maalim Seif ambacho kiliwatia hatiani wanachama hao.

Waliovuliwa uanachama pamoja na Hamad ni Doyo Hassan Doyo ambaye ni Mjumbe wa Baraza Kuu (Tanga), Shoka Khamis Juma, Mjumbe wa Baraza Kuu (Pemba) na Juma Saanane Mjumbe wa Baraza Kuu Unguja.

Hamad na hujuma
Desemba 27 mwaka jana, Hamad Rashid aligoma kuhojiwa na Kamati ya Maadili na Nidhamu, akitoa sababu kuu tano huku akiibua tuhuma nzito za kunasa waraka wa mawasiliano uliotumwa kwa barua pepe na Maalim Seif kwenda kwa mwenyekiti Profesa Ibrahim Lipumba ukionyesha mpango wa kumshughulikia yeye.

Katika msimamo wake huo, Hamad Rashid alisema alikuwa na sababu hizo tano za kugomea kikao hicho, ambazo ni pamoja na waraka huo wa siri aliodai ulitoka kwa Maalim Seif kwenda kwa Lipumba ukielekeza namna ya kumshughulikia.

Waraka huo ulioandikwa Desemba 14, 2011 ulikuwa na kichwa cha habari, “Tuwe waangalifu tusiingie katika mtego ukitaka Hamad Rashid afukuzwe kwenye chama.

Sababu ya pili, alisema baadhi walioteua katika Kamati hiyo ya Nidhamu na Maadili walikwishamtuhumu hadharani na kumtia hatiani hivyo, kikao hicho kisingeweza mtendea haki.
Alitaja sababu nyingine ya kukataa kuhojiwa kuwa ni kutoelezwa tuhuma zake hasa vifungu vya Katiba alivyodaiwa kuvikiuka.

“ Ni vema nikaelezwa ni vifungu vipi vya katiba hiyo nilivyokwenda navyo kinyume,” alisema akisisitiza msimamo wake kukataa kuhojiwa.

Sababu nyingine aliitaja kwamba alitaka apewe hadidu za rejea za kikao kilichounda Kamati ya Nidhamu na Maadili kwa sababu haipo kikatiba, hakuna chombo kama hicho.

Pia alitaka apewe nakala ya uteuzi wa wajumbe walioteuliwa katika kamati hiyo na kutaka apewe kanuni zitakazotumika katika kuendesha shughuli nzima ya kujibu tuhuma hizo na kupewa katiba iliyotumika ambayo ameivunja.Lakini pia, aligoma kuhudhuria kikao hicho kwa kuwa tayari alibaini njama za kumshughulikia zilizosukwa na Maalim Seif na Lipumba.

Hamad Rashid alijikuta kwenye mgogoro na baadhi ya viongozi wa makao makuu ya chama hicho, baada ya kutangaza dhamira hiyo yake ya kugombea nafasi ya katiba mkuu mwaka 2014.

Kuanzia hapo akajikuta ameingia kwenye mgogoro na chama hicho kiasi cha kunusurika kushambuliwa na watu wasiojulikana wakati akigawa misaada katika matawi ya chama hicho, kata ya Manzese.

Mvutano huo ulisababisha vurugu katika tawi la Chechnya ambako wanachama wanaomuunga mkono walipambana na walinzi wa Blue Guard na kusababisha umwagaji damu.

Share: