Noti mpya zinakuja-BoT

Written by  //  04/07/2010  //  Uchumi  //  Zima maoni

Na Joseph Mwendapole

4th July 2010

Benki Kuu ya Tanzania (BoT), imesema inatarajia kuchapisha noti mpya hivi karibuni.

Hayo yalisemwa jana jijini Dar es salaam na Ofisa Tawala wa benki hiyo, Harry Mwansembo, katika maonyesho ya kimataifa ya biashara yanayoendelea.

Alisema noti hizo zitakuwa kwenye mzunguko na noti za sasa hadi zitakapobadilishwa na zile za zamani zote kuondoka katika mzunguko.

“Noti mpya zikija zitakaa katika mzunguko na hizi za sasa hadi BoT itakapohakikisha zile za zamani zimerudi zote na haziko katika mzunguko,” alisema.

Aliongeza kuwa zitakapoanza kutumika noti mpya, wananchi wataelimishwa kuhusu alama ambazo watatumia kuzitambua ili kuepuka matapeli ambao wanaweza kujaribu kuzighushi.

Alisema kutakuwa na alama za uficho ambazo hata matapeli yakijitahidi kwa namna gani hayataweza kutengeneza noti zinazofanana na hizo mpya zitakazotengenezwa.

“Kuna alama za uficho ambazo wananchi wataonyeshwa ili kukabiliana na matapeli ambao wanaweza kujaribu kuzighushi,” alisema.

Aliongeza kuwa suala la ujio wa noti mpya linashughulikiwa na timu maalum ambayo ndiyo inajua ni lini zitaanza kutumika. Kuhusu noti bandia, alisema inakuwa vigumu kukabiliana na suala hilo kwa kuwa Sheria yake si rafiki na inawatisha wananchi kwenda kutoa taarifa polisi ama kwao pindi anapopata noti bandia.

“Sheria si rafiki, inasema anayekutwa na noti bandia ndiye anashtakiwa sasa mtu akigundua kuwa amepewa noti bandia anachoweza kufanya ni kuitupa ama kuichana maana akienda nayo polisi anakamatwa,” alisema.

Aliongeza kuwa kuna haja ya kuiangalia upya sheria hiyo ili iwe rahisi kukabiliana na watengenezaji wa noti hizo bandia.

CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

Comments are closed.