Serikali uchambue mafanikio upinzani

Written by  //  16/06/2010  //  Uchumi  //  Zima maoni

Na Salma Said,

KAMBI ya upinzani katika baraza la wawakilishi Zanzibar imesema ipo haja kwa serikali kuonesha mafanikio yaliopatikana katika kipindi kilichopita katika sekta za utalii na kilimo kwa kuyaeleza kwa kina katika
bajeti yake ya mwaka huu.

Hayo yameelezwa na waziri kivuli wa wizara ya nchi katiba na utawala bora, Said Ali Mbarouk alipokuwa akiwasilisha hutuba yake jana katika kikao cha baraza la wawakilishi kinachoendelea Maisara Mjini Zanzibar.

Alisema hotuba ya bajeti ya mwaka huu wa fedha umeleza kuwa serikali imepata mafanikio makubwa na kutoa mifano ya kumekuwa na ongezeko la uimarikaji wa miundo mbinu, kuanzishwa kwa shule za wakulima, kuanzishwa kwa miundo mbinu ya mabonde ya umwagiliaji maji, kununuliwa mtambo mpya wa “Liquid nitrogen.”, kutoa vifaa na maboti ya uvuvi, kutembelewa na watalii 134,954 na Kuwepo hoteli 23 zenye hadhi ya nyota 4 na 5.

“Mhe. Spika, katika hotuba ya bajeti ya mwaka jana tulielezwa kwamba Bajeti ya miundo mbinu itakayo imarisha Kilimo na Utalii . Ni vyema waziri akaelieza Baraza lako kwa mifano halisi mafanikio ya kilichopatikana. Haitoshi hata kidogo kutoa maelezo ya jumla pekee” alisema Mbarouk.

Alisema ni vizuri serikali ikaeleza uanzishwaji wa shule za wakulima umetoa tofauti gani ya uzalishaji kwa mlinganisho wa miaka mitano nyuma, au uanzishwaji wa miundo mbinu ya mabonde ya umwagiliaji, matrekta 45 na mbegu za aina 100 zimeongeza vipi uzalishaji wa mchele katika nchi na kwa kiasi gani umepunguza uagiziaji wa mchele kutoka nje, na kwa kiasi gani umepunguza mfumuko wa bei.

Waziri kivuli huyo alisema pia serikali inapaswa kuwaeleza wajumbe wa baraza la wawakilishi na wananchi kwa ujumla kwamba utolewaji wa vifaa na maboti ya uvuvi, umeongeza vipi upatikanaji wa samaki, na ulipunguzaje bei ya samaki kwa mlaji, au uliongezaje kipato cha mvuvi na hivyo kuchangia kupunguza umasikini wa kipato kwa wavuvi nchini.

“Mhe. Spika, Kwa bahati mbaya sana, jawabu za masuala yetu hayo hayamo katika hotuba hii ya Waziri. maana hata kule kushuka kwa mfumuko wa bei kwa mwaka 2009 na kufikia 8.9% ikilinganishwa na 20.6% ya mwaka 2008 hakukutokana na juhudi zetu za ndani isipokua imeelezwa na waziri mwenyewe kwamba kumetokana na kushuka bei ya mchele na kushuka kwa bei ya mafuta duniani na kamwe siyo uzalishaji wetu wa ndani” alisema Mbarouk.

Alisema licha ya kukubalika sababu hizo katika nadharia ya kiuchumi, lakini kwa muktadha wa ustawi wa nchi husika sababu hizo za kupungua kwa mfumuko wa bei ni tete (fragile) kwani hazitokani na juhudi za uimarikaji wa uchumi wa zanzibar.

Alisema ingekuwa ni jambo la kujivunia sana, kama upunguaji wa bei za vyakula ungesababishwa na uongezekaji wa uzalishaji wa chakula ndani na hivyo kupunguza uagiziaji wa chakula kutoka nje, na upunguaji wa bei ya mafuta ungechangiwa na uzalishaji na uchimbaji wa mafuta ndani, na hivyo kupunguza uagizaji na bei ya mafuta ya nje.

“Mhe. Spika bahati mbaya ni kwamba mipango katika bajeti hii tunayoijadili ya kurekebisha kasoro hizo imekosekana. Katika Bajeti ya mwaka huu kumetajwa misamaha ya nafuu ya uwekezaji katika kilimo jee mkulima wa ndizi ya Gando na yule wa tungule wa Matemwe watafaidikaje na misamaha hiyo” alisema waziri kivuli huyo.

Akitoa mfano wa soko la ndani alisema katika soko kuu la Mwanakwerekwe asilimia zaidi ya 70 ya bidhaa zinazouzwa hazitokani na uzalishaji wa wakulima wa Zanzibar ambapo wakulima wa nje ya Zanzibar ndio wanaofaidika na soko la mahoteli ya Utalii nchini jambo ambalo linawanyma fursa wakulima wa ndani.

“Mhe. Spika, katika hotuba yake Mhe.Waziri, anazungumzia suala la urari wa biashara katika Zanzibar na nchi za nje ambapo analalamika juu kupungua usafirishaji bidhaa nje kwa 1.5% ya usafirishaji wa mwaka jana, uliosababishwa na upungufu wa usafirishaji wa mazao ya asili ya karafuu na mwani” aliongeza waziri kivuli huyo.

Aidha alisema Kambi ya Upinzani imekatishwa tamaa zaidi kwa kukosekana kwa mipango ya kibajeti katika kuimarisha uzalishaji wa karafuu na mwani ambayo ndiyo mazao ya asili ya kuwapatia wazanzibari fedha za kigeni.

“Huaje zao kuu la kitaifa ambalo ndiyo tegemeo letu la kusaidia kupata fedha za kigeni litengewe sh. Milioni 80 tu. Serikali haikuweka mipango yeyote ya muda mfupi au ya muda mrefu kurekebisha hali hii ya mazoa yetu ya biashara” alisema Mbarouk ambaye ni mwakilishi wa jimbo la Gando kisiwani Pemba.

Comments are closed.