Login



Fotos

Get the Flash Player to see the slideshow.

Migawanyo

Kumbukumbu

UPIGAJI KURA WAFANYIKA KWA UTULIVU

Siku imeanza Zanzibar. Ndio nimetoka kituo cha skuli ya Mtopepo ambapo Maalim Seif ndipo alipopiga kura yake kama nusu saa iliyopita. Umma ni mkubwa kwenye kituo hicho kama picha inavyoonesha. Hali kwa ujumla ni ya utulivu kwa nchi nzima. Taarifa mbaya tu ni kuwa sheha wa Mwera amewekwa ndani kwa sababu alikuwa amekaa kituoni akimwambia kila mpiga kura apige HAPANA.

Salma Said, Zanzibar

KURA ya maoni ya kuamua kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa Zanzibar imefanyika kwa amani jana kinyume na chaguzi zilizopita ambazo husababisha watu kupoteza maisha na wengine kupata ulemavu wa kudumu.

Wananchi walianza kujitokeza asubuhi kabla ya zoezi hilo kuanza kufanyika mnamo majira ya saa 2 asubuhi chini ya ulinzi wa kawaida wa askari polisi ambao walionekana makini wakiwa hawana silaha katika maeneo ya vituo vya wapiga kura.

Katika mitaa ya mji wa Zanzibar doria ya askari ilikuwa imeimarishwa wakiwemo askari wa FFU ambao walionekana katika maeneo mbali mbali kuhakikisha zoezi hilo linafanyika katika kwa amani na utulivu.

Afisa wa kura ya maoni wilaya ya mjini, Mwanapili Khamis Mohammed alisema zoezi hilo limepata mafanikio na hadi mchana hapakuwa na malalamiko yoyote yaliojitokeza.

“Tayari nimeshatembelea vituo mbali mbali hakuna malalamiko yoyote yaliojitokeza hadi sasa ingawa ujio wa watu umekuwa ukipungua tofauti na asubuhi” alisema afisa huyo.

Afisa wa kura ya maoni katika kituo cha Kwerekwe B Haji Mwalimu Kidofu alisema kwamba wananchi wanajitokeza kwa wingi tokea asubuhi ambapo alisema zaidi ya watu 5,000 walikuwa wameshapiga kura katika vituo hivyo hadi mchana.

Alisema zoezi hilo litaendelea hadi hapo saa 10 jioni watakapoanza kazi ya kuhesabu baada ya wananchi kukamilisha wajibu wao na kupiga kura.

Hata hivyo vituo vya wapiga kura katika maeneo ya Chwaka, Uroa, Mtende, Kizimkazi Mkoa wa Kusini Unguja wananchi waliendelea kujitokeza taratibu na hapakuwa na msongamano wowote katika vituo tofauti na maeneo ya mjini ambao watu wengi walijitokeza na kupanga foleni hasa wakati wa asubuhi.

Mkuu wa kitengo cha habari na mawasiliano, Idrissa Jecha alisema hadi mchana zoezi lilikuwa linakwenda kama lilivyopangwa kwa Unguja na Pemba na hakuna malalamiko yoyote kutoka kwa wananchi katika zoezi hilo.

“Kazi ya kuhesabu itaanza katika vituo baada ya wananchi kumaliza kupiga kura katika vituo na baadae majumuisho yatafanyika” alisema Afisa huyo.

Rais wa Zanzibar Amani Abeid Karume alipiga kura katika kituo cha Kiembe samaki na kueleza kuwa amefarijika kuona zoezi hilo linakwenda kwa amani na utulivu na kuwataka wananchi kudumisha utulivu wakati wote wa upigaji kura na baada ya kupiga kura na baada ya matokeo.

Alisema kwa mujibu wa sheria ya kuweka kura ya maoni kura zote zitahesabiwa katika vituo na kutangazwa kabla ya kufanyika majumuisho ya mwisho.

Naye katibu mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad alipiga kura yake katika kituo cha Mtoni wakati mgombea mwenza wa urais wa Tanzania, Dk Mohammed Gharib Bilal alipiga kura katika kituo cha Kiembe samaki.

Maalim Seif alisema kwamba kura hiyo ya maoni imefanyika katika mazingira ya amani na utulivu kutokana na maridhiano yaliofikiwa kati yake na rais Karume huku huku akisisitiza kudumishwa amani iliyopo.

Alisema ni jambo la faraja kuona wananchi wanatekeleza haki yao ya kikatiba bila ya kusukumana tofauti na miaka ya nyuma na kuwataka wananchi kuendelea kudumisha hali ya maelewano hasa wakati huu wa kuelekea uchaguzi huu mkuu.

“”Nyote mnaona watu wanapata haki yao ya kikatiba bila ya kusukumana tofauti na miaka ya nyuma hali hii ndio tunayoitaka katika kujenga Zanzibar mpya” alisema Maalim Seif.

Jumla ya watu 407,950 wanatarajiwa kushiriki katika zoezi hilo kati ya watu walioandikishwa katika daftari la kudumu la wapiga kura na na kwa mujibu wa sheria matokeo ya kura hiyo yanatakiwa yatangazwe ndani ya masaa 48.

Share and Enjoy:
  • Facebook
  • Twitter
  • Digg
  • MySpace
  • del.icio.us

Maoni yamefungwa.