Habari

Ushauri kwa Serekali iliopo madarakani – Kodi za vyakula!

Nimekuwa kwa muda nikifuatilia kwa njia za kienyeji jinsi ya hali ya maisha ilivyo nyumbani au visiwani Zanzibar.Niseme ukweli nimekuwa nafurahishwa pale ninaposikia mambo ya uchumi ni mazuri huko nyumbani (fuatilia video hapo chini kujiridhisha kama SMZ imepata ongezeko la asilia kadhaa kulinganisha na mwaka uliopita yaani 2015).

Kwa vile serekali imekuwa na pato la kutosha kiasi na mambo ni mazuri, nami nitoe ushauri kuhusiana na suala zima la kodi za vyakula kupitia bandari yetu ya Zanzibar.Serekali inapokuwa na mfuko ulionona nasi wananchi tungependelea kuona kodi za vyakula zikipunguzwa au kuondoshwa kabisa.

Ni mazoea kuona wakati serekali inapokuwa na wakati mgumu bei za kodi zikipandishwa, na mara hujakaa vizuri ukaona miaka ya kupumzika ikapandishwa au malipo ya wazee yakapunguzwa na vitu kama hivyo.Nimejiridhisha kwa kufuatia kauli ya Dr.Shein kuwa SMZ inafanya vizuri na uchumi unaenda vizuri kukosa mwanya wa kushauri ongezeko la kodi.

Kutokana na utalii kushamiri visiwani Zanzibar, wananchi wengi wamepata ugumu wa maisha.Hii inatoka na ukweli kuwa watalii wengi wana pato la juu la kimagharibi na kusababisha mazao mengi kama pweza, samaki, matunda n.k kuuzwa zaidi kwenye mahoteli kwa bei za juu.Hili limepelekea kwa namna moja au nyengine bidhaa hizi muhimu kwa mzanzibari kuwa haba au kupanda bei mara dufu katika masoko.

Nashauri serekali iliopo na wawakilishi wetu waliopo barazani wakawa na huruma na kulipigia chapuo hili la kodi za vyakula.Sina uhakika vyakula kama michele ya Bara ikiingizwa Zanzibar inatozwa kodi kiasi gani kulinganisha na bidhaa zengine.Lakini si jambo geni kuona bidhaa zengine zikawa na asilimia ya juu ya kodi kulinganishwa na ile ya vyakula kuwa ya chini kabisa.

Hili la kuondosha au kupunguza kodi liko ndani ya mikono yetu, wala hatuna wa kumnyooshea kidole.Nataka niamini wawakilishi wa wananchi wanaopata maposho hadi ya kukaa kwenye viti wataniunga mkono juu hili!

Wasalaam

Share: