Habari

UTALII WADODA ZANZIBAR KWA SERA ZA TANGANYIKA, HOTELI ZAKOZA WAGENI NA AJIRA BINAFSI ZIMESIMAMA

UTALII WADODA ZANZIBAR KWA SERA ZA TANGANYIKA, HOTELI ZAKOZA WAGENI NA AJIRA BINAFSI ZIMESIMAMA.

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imeshauriwa kuweka mpango mpya wa kuongeza Idadi ya watalii utakaowawezesha wageni wenye vibali vya kufanyika kazi katika nchi za Afrika Mashariki kutumia fursa ya kutembelea Zanzibar-
bila ya kutozwa visa ili kuziba pengo la hoteli kukosa wageni msimu usio wa utalii.

Ushauri huo ulitolewa na Mwakilishi wa jimbo la Tunguu na Mwenyekiti mstaafu wa Jumuiya ya Wawekezaji wa Sekta ya Utalii, Simai Mohamed Said, alipokuwa akizungumza na Nipashe kuhusu maendeleo ya sekta hiyo visiwani hapa.

Alisema wataalamu wengi wanaofanya kazi zao katika nchi zilizomo ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, watapata nafasi kubwa ya kutembelea Zanzibar endapo Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itakapoamua kuondoa malipo ya visa za kuingia nchini hatua itakayosaidia kuvutia wageni wanaofanya kazi katika miji ya Kigali, Nairobi na Kampala.

“Wakati umefika kwa Serikali zote mbili kukubaliana kuondoa ada za visa kwa wafanyakazi wa kigeni, wanaofanya kazi zao katika miji mikubwa ya nchi wanachama wa jumuiya ya Afrika Mashariki, ili waweze kuja kuziba pengo linalojitokeza wakati usiokuwa wa msimu wa utalii,” alisema.

Alisema hatua hiyo itasaidia kuondoa tatizo la vitanda vingi kutokuwa na wageni msimu wa utalii unapomalizika na utaratibu huo utasaidia badala ya wageni kwenda kutembea sehemu wanazotoka na kutumia nafasi hiyo kuangalia vivutio vya utalii Tanzania Bara na Zanzibar.

Aidha, alishauri kubadilisha jina la msimu usiokuwa wa utalii kuuita ‘Low Season’ na badala yake kuuita Msimu wa Kijani ‘Green Season’ kwa vile kuna wageni kutoka nchi za Mashariki ya Kati wanaovutiwa na msimu wa mvua na mandhari ya kijani.

Aliongeza kuwa hivi sasa kuna umuhimu mkubwa wa kuanzisha utalii wa aina nyingine unaohusisha mikutano ya kimataifa ambayo itaweza kusaidia kufungua milango mengine ya kuimarisha sekta ya utalii Zanzibar kwa kupokea wageni ambao watakuja kushiriki katika mikutano yao.

Sekta ya Utalii visiwani Zanzibar ndio nguzo kuu ya uchumi ikichangia asilimia 27 ya pato la taifa na asilimia 83 ya fedha za kigeni na kutoa ajira kwa watu zaidi ya 22,000 pamoja na Wakulima, Wavuvi na Wafugaji ambao wananufaika na soko hilo la Utalii.

Chanzo : Nipashe

Share: