Habari

UVCCM YAMUONYA MAALIM SEIF

Mwandishi wetu (TANZANIA Daima) Pemba.

UMOJA wa Vijana wa CCM (UVCCM) umemuonya Makamu wa Kwanza wa Rais  wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad kuacha matamshi ya kichochezi yanayoweza  kuleta  mgawanyiko.

Naibu Katibu Mkuu wa UVCCM, Shaka Hamdu Shaka alitoa kauli hiyo jana wakati  akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika huko Micheweni, Pemba  na kusema Maalim Seif anatakiwa kukubali kufanya kazi chini ya Serikali ya Umoja  wa Kitaifa (SUK) au ajiuzulu.

Shaka alisema anachokitafuta Maalim Seif ni kutokea kwa mpasuko katika SUK  kabla ya mwaka 2015 kwa kuamini hata akigombea kwa mara ya tano, hatapata  ushindi.

Alisema Maalim Seif, anaposema anabaguliwa na hashirikishwi katika SUK  Zanzibar, ni dhahiri anakusudia kutokee ghasia, mpasuko na mkorogano, ili  Zanzibar irejee katika mivutano iliyokuwepo mwaka 1995 na kusababisha watu  kupoteza maisha.

Aidha, mtendaji huyo wa UVCCM Zanzibar alimtaka Maalm Seif  kuacha kumsakama  Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Idd kwa hoja zisizo na msingi katika  majukwaa ya kisiasa.

Alisema kitendo chochote cha Maalim Seif kitakachoashiria kumpaka matope  Balozi Seif, UVCCM hautakaa kimya na kuacha atambe.

Alimtaka Makamu huyo wa Kwanza wa Rais ambaye pia ni Katibu Mkuu wa CUF  kukubali kukaa pembeni na kuwapisha vijana.

Share: