WARAKA MCHAFU WASAMBAZWA
Written by salma // 09/09/2010 // Habari // 7 Comments
TAARIFA YA VYOMBO VYA HABARI
Chama cha wananchi CUF kimemuandikia Kamishna wa Polisi (CPZ) wa Zanzibar barua ya malalamiko kuhusiana na waraka wa upotoshaji dhidi ya chama na mgombea wake wa kiti cha Urais wa Zanzibar, Maalim Seif Shariff Hamad.
Chama kinasikitishwa na kitendo cha hujuma kinachofanywa na watu fulani cha kutengeneza waraka potofu na kuusambaza kwa wananchi na ndani ya vikosi vya Ulinzi vya SMZ kwa nia ya kukipaka matope chama pamoja na mgombea wake.
Waraka huo unadai mambo mbali mbali kama ahadi za Maalim Seif atakapopata Serikali baada ya Uchaguzi Mkuu wa tarehe 31 Oktoba 2010. kwa mfano, waraka unadai serikali ya CUF itataifisha mahoteli ya kitalii na itavunja uhusiano na Nigeria, na itawafungulia mashtaka viongozi na watendaji wote wa SMZ na CCM mambo ambayo hayana ukweli wowote. CUF kinatamka bayana kwamba hakihusiki kwa namna yoyote ile na kuandaa na kusambaza waraka huo. Ni waraka wa uongo na wenye lengo la kuvuruga matumaini ya wazanzibari wanaokiamini chama na mgombea wake.
Chama cha CUF kinatanabahisha wananchi wote wa Unguja na Pemba, watanzania wote popote walipo pamoja na ulimwengu mzima kwamba ahadi za chama na mgombea zipo kwenye ilani yake ya Uchaguzi ambayo itazinduliwa rasmi kampeni za Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar zitakapoanza.
Nje ya ilani hiyo ni mgombea atakayetamka ahadi anayoona inawezekana kutekelezeka, iwapo atapewa ridhaa ya kuongoza serikali.
Chama cha CUF kimemuomba kamishna wa Polisi Zanzibar afanye uchunguzi ili kujua chanzo cha waraka huo na kinaweza kuanzisha uchunguzi wake kwa Mhe. MASOUD MSELEM kwa umaarufu Roho Mbaya ambaye ni sheha wa shehiya ya Limbani, wilaya ya Wete, Pemba ambaye amekutwa akitolesha kopi waraka huo katika duka moja mjini wete.
Ni matumaini ya chama chetu na mgombea Urais wa Zanzibar, Maalim Seif, kwamba hatua hiyo itachukuliwa haraka ili kukomesha mtindo mbaya unaojirudia kila ufikapo Uchaguzi Zanzibar.
Chama cha CUF kinasisitiza kitafanya kampeni za kiungwana kama kawaida yake, kwa kueleza sera yake na nini Serikali ya CUF itafanya itakapoingia madarakani baada ya Uchaguzi.
HAKI SAWA KWA WOTE
Salim A. Bimani






7 Comments on "WARAKA MCHAFU WASAMBAZWA"
ninanukuu: chama cha cuf kinasisitiza kitafanya kampeni za kiungwana………………………….na nini serikali ya CUFitafanya itakapoingia madarakani.
suala jee ile serikali ya umoja wa kitaifa haitokuwapo ikiwa mtashinda?
ramazani njema kwa wote
sasa haya ni musuala gani jamani hapa kwani kwa kuwa serikali ya umoja itakuwepo ndio wasiseme nini watafanya wakishinda mbona mnakurupuka kusema vitu kabla kufikiri?!!! kama ilivyo cuf kuweka malengo yao na ccm wataweka ikiwa wakishinda watafanya nini kwa ajili ya zanzibar kwani mfumo bado ni wa vyama vingi na ilishasemwa hapo kabla si vibaya pia kuyachukuwa yote mazuri katika hiyo serikali yetu hata iwe si ya chama kilichoshinda!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!
eid njema
kama kukurupuka basi sote tumekurupuka kwani suala liko wazi .makubaliano kama sio kiini macho yanasema serikali ya umoja wa kitaifa kwa hiyo haina maana kwamba itakua serikali ya cuf au ccm,labda sikufahamu au labda pia makubaliano yamewekwa kua na serikali mbili moja ya chama kitachoshinda na nyengine iwe ya kitaifa.
sikukusudia utashi wa kisiasa bali nilikua ninajaribu tu kuelewa hali halisi kwani tangu mwanzo nilikua na wasi wasi na hayo makubaliano ya seif na karume na kidogo kidogo wasiwasi wangu unazidi kuwa nkubwa kutokana na hizo kauli ambazo hua zinatoka katika huu ukumbi ambao ninathubutu kusema ni SAUTI YA CUF na kila anaejaribu kuingia katika ukumbi huu lazima akubaliane na yasemwayo au la sivyo hubandikwa jina
furaha na amani iwe kwa wote
Wakati ukifika hakuna anaeweza kuzuia mabadiliko mzee chacha… nani alifikira Banda ataondoka Malawi au Kaunda Zambia au kuanguka kwa USSR, ujamaa katika Eastern Europe. Hivyo kaa chonjo usije ukagongwa na gari moshi la mabadiliko kwani sasa limeshika kasi na halizuiliki tena. Kukaa kaa barabarani unaweza kukokotwa na mkondo, baadae usije ukalia na ulimwengu..
ww chachandu huwezi kufikiri unaongowa na hisia zako baada ya hali halisi… hivi ni nani asiejua kama serikali ijayo ni ya pamoja? mpaka katiba ishabdilishwa tena kiini macho kiko wapi hapo? nyie ndio wale kama mayahudi walivyomwmabia nabii musa (AS) kuwa hawamuamini mungu mpaka wamuone? chama kutangaza sera zake haina maana kuwa hakuna serilai ya pamoja… na ndio maana hata ccm pia watatangaza sera zao? au ww ulitakaje mwenzetu? watu kampeni waendeshe vp? jaribu kuwa na ubongo wa kufikiri na sio kushabikia shabikia tu… ila ninaungana na ww jambo moja tu.. ktk mtandao huu ukionekana unapinga pingana na watu basi unaonekana msaliti maana watu wengi humu wanatete upinzani kwa hilo naungana na ww..maa salaam…eid njema
Watu wamechoshwa na ukandamizaji sasa wanataka kujikomboa ndio ukaona wengi wanakwenda sambamba na sera za CUF lkn sio kweli kua kila anaepinga anaonekana msaliti kwani kutafautiana mawazo ipo ila mawazo ya kibaguzi na kuturejesha nyuma ndio hapa yanapingwa.
Naomba musome ile mada ya madai kuhusu seif dhidi ya jumbe hayana mashiko mutaona jinsi tulivopingana.
Jamani fuatilieni hali halisi na si mkae majumbani mkisikiliza propaganda za viongozi wa CCM tu ambao wanajitafutia madara kwa njia ya kuchochea ugonvi na ubaguzi kwa raia.
Sera ya serikali ya umoja wa kitaifa ilikuepo ktk ilani ya CUF ktk uchaguzi wa 2005. Kwa hiyo hili si jambo geni lkn tatizo ni kua watu hawasomi sera bali wanasikiliza propaganda labda ndio kua hawajui kusoma au ndio kasumba zimewajaa.
Watu wanasema kuuliza si ujinga lkn ndio tuulize maswali ya kijinga kama hivi?
Serikali ya umoja wa kitaifa ipo germany,marekani, nk. Jee huko hakuna chama kinachoongoza serikali? Au serikali zinaitwaje? Democratic sio chama tawala marekani? Ah mnaboa kwa maswali ya kitoto bana hayajenda shule.
EID MUBARAK