Habari

Warioba alijia juu Jukwaa la Katiba

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba amesema ofisi yake inafanya na itaendelea kufanya kazi kwa kuzingatia Sheria ya Mabadiliko ya Katiba iliyopitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na si vinginevyo.

Kiongozi huyo ametoa kauli hiyo siku moja baada ya tishio la asasi ya Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata) kwenda mahakamani ili kusimamisha mchakato wa Katiba Mpya.

Akizungumza ofisini kwake jana, Jaji Warioba alisema kama kuna watu wanataka kwenda mahakamani kupinga mchakato huo wanaruhusiwa kufanya hivyo.

Alisema mbali ya kufuata sheria, Tume yake inafanya kazi kwa kuzingatia maoni yaliyotolewa na wananchi zaidi ya 300,000 pamoja na makundi maalumu 160.

“Kila mtu ana haki ya kwenda mahakamani, tupo tayari kupokea ushauri lakini hatupo tayari kupokea vitisho,” alisema Jaji Warioba, ambaye pia amewahi kuwa Waziri wa Sheria na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Alisema maelezo yalitotolewa jana na Jukata hayana msingi wowote na kusema jukwaa hilo linakwenda mahakamani kujishtaki lenyewe na si Tume ya Mabadiliko ya Katiba kwa kuwa inafanya kazi zake kwa mujibu wa sheria.

“Nina shaka sana na matamko yanayotolewa na jukwaa hili, zipo asasi ndani ya jukwaa hilo ambazo zimeiomba Tume kushiriki katika Mabaraza ya Katiba bila kivuli cha Jukata. Sasa Jukwaa hili ni nani haswa?” alihoji.

Alisema kauli kuwa tume hiyo inaminya mchakato wa Katiba si ya kweli akisema imeundwa kwa kuzingatia mapendekezo ya makundi mbalimbali na inafanya kazi yake kwa kufuata sheria na inawajumuisha watu wenye weledi na uadilifu mkubwa.

“Wanaosema kuwa sisi tunaipendelea CCM maana yake ni kwamba wanabeza uteuzi wa tume hii ambayo uwepo wake umeridhiwa na wananchi wote kupitia katika makundi yao. Waliotakiwa kuiponda kwamba inafanya kazi bila kuzingatia weledi ni wananchi ambao walikutana na wajumbe wakati wakitoa maoni yako katika mikoa mbalimbali nchini,” alisema.

Alisema kwa mujibu wa sheria, Tume hiyo imepewa miezi 18 kukamilisha kazi yake na Oktoba mwaka huu ndipo itakamilisha rasimu ya Katiba, kabla ya kuanza kwa Bunge Maalumu la Katiba na baadaye kupigiwa kura ya maoni.

“Tunatakiwa tulaumiwe baada ya kuitoa rasimu ya Katiba, lakini kwa sasa ni kama tunaingiliwa kazi yetu kwa sababu hakuna mtu anayejua rasimu itakuwaje na hakuna anayejua Tume itapendekeza nini kiwemo kulingana na maoni ya wananchi, hasa suala la Muungano na madaraka ya Rais,” alisema.

Alisema Tume yake itaendelea na ratiba yake kama kawaida na kwamba mchakato mzima wa Katiba utasimamishwa iwapo tu Mahakama itasikiliza hoja za Jukata na kuziona zina msingi.

Akizungumzia marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Warioba alisema anachofahamu ni kwamba Serikali ipo katika mchakato wa kuirekebisha sheria hiyo kama ilivyoahidiwa.

Alisema kwa sasa tume hiyo inaendelea na kuandaa rasimu ya Katiba na wananchi watapata muda wa kutosha kuijadili na kutoa maoni yao.

Mwenyekiti wa Jukata, Deus Kibamba juzi alitangaza azma ya kufungua kesi mahakamani ndani ya siku saba, kuomba kusitishwa kwa mchakato mzima wa Katiba Mpya kwa madai kuwa uendeshwaji wake umejaa mizengwe, itikadi za vyama na rushwa.

Katika maelezo yake Jukata ilisema kesi hiyo itasimamiwa na timu ya mawakili 10 watakaoongozwa na Mwanasheria wa masuala ya Haki za Binadamu, Dk Rugemeleza Nshala, itawasilishwa Mahakamani siku saba zijazo, kuanzia jana. Akizungumzia suala hilo, Jaji Warioba alisema Tume yake endapo itashtakiwa na Jukata, yenyewe itawakilishwa na wakili mmoja tu.

Share: