Habari

Wasio ufahamu Muungano wa Mkataba

Wasiofahamu maudhui ya muungano wa aina ya mktaba hufikiri kwa woga kwamba ni mfumo wa kuvunja muungano kwa urahisi wakati lengo kuu ni kuhakikisha washirika kuwa na haki, usawa na heshima katika mwenendo mzima wa muungano wenyewe.

Kama ni rahisi kuuvunja wa mkataba basi watazame huu wa EU ambapo muingereza ameamua kujitoa kuanzia referendum ya kujitoa, mpaka hii leo bado hio article 50 ya kujitoa haijawekwa wazi kuhakikisha kila upande unafaidika na mabadiliko ya Muingereza kujitoa kwake na hivyo kukubaliwa kwake kujitoa. Kuna uwezekano hasa ikachukua miaka mitatu mengine mpaka wawafikiane namna ya kujitoa na namna ya ushirikiano mpya wanaoutaka.

Kurudi katika mkataba ni kurudi katika “article of union” ya 1964 ambayo ndio msingi hasa wa mawafikiano ya kuundwa kwa muungano. Si jambo geni ila kilichofanyika ni kuudogesha mkataba wa muungano wa mwaka 1964 kiasi kwamba umekuwa sawa na maandisho ya kihistoria badala ya kuwa na uzito wa kuyakabili malalamiko ya kila pande yanayozua kero na koti kuvaliwa na upande mmoja. Kuurejesha muungano wa mkataba ni kurudi katika makubaliano ya awali yalioasisiwa na Mzee Karume na Mwalimu katika maboresho mapya yanayotazama wakti, matukio na mahitaji ya sasa.

Tulipokuwa tunazungumza serikali tatu miaka ya thamanini hakuna alietufahamu upande wa pili. Lakini tumeona kama Warioba alivyolieleza huko nyuma kuwa mfumo wa serikali tatu umekuwa ndio chaguo la wengi wakiwamo hata waliomo katika safu ya sasa ya uongozi wa watawala. Itafika wakati wenye uoga wa mfumo wa mkataba wataufahamu zaidi na kujuwa kuwa kifikra waliokuja na mfumo huu walikuwa na lengo kubwa zaidi ya kuuimarisha muungano na kuufanya uwe na mvuto kwa wengine kujiunga nao na kwa mafanikio makubwa zaidi.

Maana ya mkataba ni makubaliano yatayohakikisha hakuna sheria holela za upande mmoja kuuburuza mwengine kwa sababu ya ukubwa wa mmoja bali nchi zitahisabika kuwa nchi zenye haki sawa na kuheshimiana katika maamuzi ikiwamo ridhaa ya wananchi. Mfano mdogo ni kuwa wengi wa wazanzibari mwaka 2010 waliuidhinisha mfumo wa serikali ya umoja na kubadili katiba yao. Lakini utashangaa katika mkutano wa mtukufu anasema kama yeye asingewaweka wapinzani katika serikali yake abadan. Inaonyesha wazi kwa hili kuwa mtukufu hatazami katiba yetu inavyosema na hata ridhaa ya wananchi walioridhia mabadiliko ya katiba yalioleta SUK mwaka 2010 bali ni fikra zake hata kwa asiyo na mamlaka nayo. Itafika siku atajengwa na fikra ya kutokuwapo hasa faida kwake kwa serikali ya Zanzibar, jee tutapiga makofi na vigelele?

Katika mfumo wa mkataba hakuna ataeweza kuikandamiza na kuidharau katiba ya mwenziwe kwa utukufu wake na makubaliano yote yatabaki kwa yale pekee yaliomo katika mikataba tuliokubaliana na kuiidhinisha kwa wananchi. Mwaka 1964 tulikuwa na makubaliano haya yaliozaa muungano, yalikuwa na uzito kiasi kwamba haikuwa tabu kuiachia katiba ya Tanganyika wakati huo kugeuzwa na kuwa ya muungano kwa sababu vyama kila upande vilibeba hatamu za nchi zao, na mkataba wa muungano ukawaongoza katika maamuzi.

Lakini kuunganisha vyama hata ikiwa kwa nia njema kabisa kumeondoa hii “buffer” ya utukufu wa “article of union” na kuifanya kuwa ni sehemu tu ya maandishi ya historia badala ya kuwa ndio ramani ya ujenzi wa muungano tulioukusudia na kuuwekea lengo. Matokeo yake ndio haya maadhimisho ya Rais wa Zanzibar kuwa Makamo wa Rais wa muungano asie na mamlaka yoyote, au hivi sasa kuwa katika Baraza la Mawaziri asie na mamlaka youote. Kuondosha kero, kuficha ficha na hadaa za sheria tusizofahamu ndio likarejeshwa lengo la awali la mkataba ulio wazi unaoeleza mipaka ya mamlaka zetu, maamuzi yetu na muelekeo wetu kama taifa moja katika muungano wa nchi mbili zilizoamua kwa hiyari kuishi pamoja kuendeleza miaka hamsini ya changamoto zinazolindwa si kwa hiyari na ridhaa ya wananchi bali kwa amri ya mtukufu na nguvu za roketi zake.

Ni aibu kwa washirika wa muungano kutamka hadharani kuwa koti lazima livaliwe kwa vile sisi ni wakubwa, au kuudhalilisha uongozi wa upande wa pili kwa kauli za kuwa waislam wengi kule watatusumbua. Mfumo wa sasa umeibuka kiunjanja ujanja na ndio msingi wa kero zisizokwisha. Hakuna anaechukia umoja, lakini iwe umoja huru, wa ithbati, ukweli, kuheshimiana na ridhaa sio wa kuvutana chini kwa chini kwa sababu ya kulinda maslahi. Hatuwezi kabisa kuitazama Zanzibar kwa Tanganyika kama Mombasa kwa Kenya, imeshindikana miaka hamsini kwa sababu ya msingi wa kuwepo kwake kama taifa kubwa nyuma, linalojitegemea na lililojengwa na ustaarabu wa kipeke. Kuishi katika ndoto hizi ni kujinyima usingizi wa makusudi kufikiri lisilowezekana. Umoja wa haki, usawa na kuheshimiana sio wa dharau, dhihaka na ubabe, hatutafika popote na joto la wananchi likizidi tutajutia kibri cha kudharau udogo wa mmoja kufikiri ndio udhaifu.

Share: