Wasomi: Bilal turufu ya CCM
Written by abuusafar // 13/07/2010 // Habari // 7 Comments
UTEUZI wa Dk Mohammed Gharib Bilal kuwa mgombea mwenza wa Rais Jakaya Kikwete umeelezewa na wachambuzi wa mambo ya siasa kuwa ni karata nzuri kwa CCM, kwani utaepusha mgawanyiko wa chama hicho Zanzibar.
Wasomi kadhaa waliozungumza na gazeti hili jana, walisema Dk Bilal ana wafuasi wengi Unguja, hivyo kitendo cha kumwengua kugombea urais wa Zanzibar, kingewafanya wafuasi wake wasimuunge mkono mgombea wa CCM visiwani humo ambaye ni Dk Ali Mohamed Shein.
Kutajwa kwa jina la Dk Bilal kuwa mgombea mwenza, hakukutarajiwa na wengi, kwani hata waliokuwa wanatajwa nyota yao kung’ara kwa nafasi hiyo, jina la mwanasiasa huyo halikuwamo.
Awali waliokuwa wanatajwa ni Waziri Kiongozi Shamsi Vuai Nahodha, Mohamed Seif Khatib na Zakhia Hamdun Meghji.
Lakini juzi usiku, Rais Kikwete alimtangaza Dk Bilal kuwa mtu atakayemsaidia kupeperusha bendera ya chama chake, kuomba ridhaa ya wananchi wamchague tena kumalizia kipindi chake cha miaka mitano chini ya kaulimbiu ya Ari zaidi, Nguvu zaidi na Kasi zaidi.
“CCM wamefanya kitendo cha busara kisiasa, kwa hali ilivyo visiwani, kwa sasa ni wazi kuwa kama Dk Bilal angekosa hata hicho alichopewa, kungekuwa na mgawanyiko mkubwa,” alisema Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Samwel Mushi.
Profesa Mushi alisema kinachozungumzwa visiwani Zanzibar kwa sasa ni maridhiano ya kisiasa na akasisitiza kuwa maridhiano hayo hayawezi kuendelezwa kama ndani ya CCM kuna watu wana kinyongo, ndio maana CCM wakatumia busara, angalau kila mtu apate.
Msomi huyo alisema jambo lolote ambalo linasababisha kutoelewana ndani ya CCM, ni lazima waliuzie na ndiyo maana wameamua kuingiza wadau wakuu wa siasa katika kugombea nafasi mbalimbali, “cha msingi pale hakuna aliyetoka bure.”
Alisema uteuzi wa Dk Bilal utaimarisha nguvu ya chama hicho Unguja na kumrahisishia kampeni Dk Shein ambaye aliteuliwa kugombea urais wa Zanzibar kwa kumshinda kwa mbali Dk Bilal. Naye Dk Mohamed Bakari wa Chuo Kikuu hicho, alisema suala la ugombea mwenza ndani ya CCM halitokani na mapenzi ya mgombea, bali kushauriana na kuona kumteua Dk Bilal ndiyo njia pekee ya kupunguza msuguano ndani ya chama hicho.
“Yawezekana Rais Kikwete alikuwa na mtu wake, lakini apende au asipende, hakukuwa na njia nyingine zaidi ya kumteua Dk Bilal ili kuziba mashimo yaliyoko visiwani Zanzibar,” alisema Dk Bakari.
Dk. Bakari alikiri kuwa Dk Bilal ana wafuasi na ngome kubwa ya kisiasa Unguja, hivyo kitendo cha CCM kumteua kuwa mgombea mwenza, ni wazi kuwa mashimo yaliyokuwa yamechimbika sasa yamefukiwa.
Pia alisema Dk Bilal anawakilisha kundi la wahafidhina visiwani humo hivyo kitendo cha kumwingiza kwenye mfumo wa uongozi ni wazi kuwa ni lazima kundi hilo lishiriki kuendeleza maridhiano ya kisiasa yaliyofikiwa kati ya Rais Amani Abeid Karume na Maalim Seif Sharrif Hamad.
“Huyu Dk Bilal anawakilisha kundi la wahafidhina, hivyo kuingizwa kwenye system (mfumo) ya uongozi utawafanya na wao washiriki kwenye maridhiano hayo ya kisiasa na hawatakuwa na haja ya kuyapinga tena,” alisema msomi huyo.
Hivyo alisema ilikuwa sahihi kwa CCM katika kipindi hiki cha maridhiano, kumteua Dk Bilal kuwa mgombea mwenza, kwani itaifanya CCM visiwani Zanzibar waendelee kuwa kitu kimoja.
Profesa Issa Shivji katika maoni yake kwa gazeti hili alisema, “Safari hii CCM imecheza karata yake ya kisiasa vizuri kwa kumteua Dk Bilal awe mgombea mwenza wa Kikwete.” Shivji, ambaye ni mhadhiri mstaafu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alisema Dk Bilal tangu aanze kugombea nafasi ya urais wa Zanzibar amekuwa anaungwa mkono na Wazanzibari wengi, hivyo kumwacha nje ya mfumo wa uongozi kungesababisha mgawanyiko mkubwa ndani ya chama hicho.
Msomi huyo alisema mkakati wa kisiasa wa kumchagua kuwa mgombea mwenza, kwanza umeondosha hali ya sintofahamu iliyokuwapo Unguja na pia CCM wamefanya hivyo ili kupoza wafuasi wa kiongozi huyo, ambaye amewahi kushika uwaziri kiongozi enzi za uongozi wa Dk Salmin Amour.
Aliendelea kusema kuwa kwa siasa za Zanzibar zilivyo, si vizuri ndani ya CCM kuwa na machafuko, kwani hiyo inaweza kurejesha nyuma siasa za maridhiano, ambazo zinaonekana kukubalika visiwani humo na walio wengi.
Naye Issa Yussuf anaripoti kutoka Zanzibar kwamba CCM imeandaa mkutano mkubwa wa hadhara keshokutwa mjini hapa kuwatambulisha wagombea wake katika uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu. “Tunaandaa mkutano wa hadhara kuwatambulisha wagombea wetu Julai 15 mwaka huu mjini hapa. Rais Karume anatarajiwa kuwatambulisha: Kikwete (anayegombea uraia wa Muungano), Dk Bilal (mgombea mwenza) na Dk Shein (urais Zanzibar),” alisema Katibu wa Uenezi na Itikadi CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai.
Vuai alisema maandalizi ya mapokezi hayo yanakwenda vizuri, na kuwataka wanachama na wafuasi wa CCM Zanzibar kujitokeza siku hiyo kwa wingi “kama ratiba haitabadilika.”
Akizungumzia taarifa kwamba baadhi ya wanachama wa CCM Zanzibar hawakufurahia uteuzi wa Dk Shein na Bilali, Vuai alisema, “tunatarajia wana CCM wote Zanzibar kuungana na kuzika tofauti zao ili kupata ushindi wa kishindo katika uchaguzi mkuu ujao.”
Hadi jana mchana, maeneo mengi mashuhuri ya CCM yalikuwa kimya wengi wa wanachama wakichelea kutoa maoni yao juu ya uteuzi wa viongozi hao wawili. “Hakuna dosari zozote katika uteuzi huo wa chama, tumepata wagombea wazuri watakaotupeleka kwenye ushindi,” alisema Mussa Ameir, mpenzi wa CCM wa Rahaleo, lakini mwenzake ambaye hakutaka atajwe jina, alisema “tulitaka Dk Bilal ndiye agombee urais Zanzibar.
Hatukufurahi, lakini hatuwezi kubadili matokeo.” Hamid Mbwezeleni, mwanasheria mashuhuri wa hapa, alisema, “kwa kuwa CCM imeshafanya chaguo lake, hakuna kibaya. Kutofurahishwa kwa baadhi ya wana CCM Zanzibar hakuwezi kuhalalisha madai yao, wanatakiwa kukubaliana na uamuzi wa chama.”
Hamad Mussa wa CHADEMA alikuwa na maoni kwamba sasa Zanzibar inaelekea kwenye mustakabali mzuri wa mabadiliko makubwa katika siasa, “kwa kuwa Wazanzibari sasa wanatarajia kupata rais wa kwanza kutoka Pemba kama Shein atashinda kwa tiketi ya chama chake.”
Katika mkutano wa kuwatambulisha wagombea wa CCM katika uchaguzi mkuu ujao jana, Dk. Bilal huku akimuita Dk. Shein kuwa ni rais mtarajiwa wa Zanzibar, aliahidi kushirikiana naye kuhakikisha CCM inapata ushindi mkubwa Zanzibar.
Akizungumza katika mkutano huo uliofanyika katika Uwanja wa Jamuhuri Dodoma na kuhudhuriwa na mgombea wa urais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais Jakaya Kikwete na Dk. Shein, Dk. Bilal alisema atachapa kazi na kutumia mwisho wa jasho lake kuhakikisha Tanzania inanawiri.
“Naahidi kufanya kazi ya kumsaidia Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Zanzibar kwa moyo wangu wote, kwa uwezo wangu wote na kwa ujasiri wangu wote,” alisema Dk. Bilal.
Dk. Bilal alisema atatumia maelekezo ya Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Zanzibar, kuhakikisha Watanzania wanapata maisha bora.
Source: Habari Leo






7 Comments on "Wasomi: Bilal turufu ya CCM"
Bilali mshapa fupa agenywe. Tunataka kufahamu nafasi ya Shemsi Vuai Nahodha. Kama hamkupa na yeye patakuwa hapatoshi mpaka kieleweke! Kwanini mumpendelee Bilali wakati Shamsi naye alikuwa na kura nyingi tena walipishana kiduchu tu!
Shamsi kwa kukosa basi mumchague Balozi wa Tanzania nchini Marekani. Sera zetu kila mtu apate cheo ili afaidike na mapinduzi. Masharubu alimuundia cheo chake Shamhuna kisicho na haja yeyote akamueka.
Tena na Shamhuna asikose nafasi yeye ndie aliyekuwa akifaa uraisi wa zanzibar kwa asilimia 100% mumendhulumu tokea Kisiwandui hata Chumbe hakuvuka, na sasa hajajua nafasi yake wakati alikuwemo katika serikali tokea ASP.
Vyeo vibuniwe hadi sote tupate, hata kama hakutokuwa na raia wa kutawala. Hii serikali yetu sote tumepindua. Mliobaki shauri zenu fungueni mbwa. Ukitia kitimtim ndio utagaiwa, kinyume chake utalala na njaa.
Chukua Chako Mapema, hadi nchi ikauke. Na ikikauka basi tunaanza kuingia majumbani. Kazi kwenu!
hii inaonyesha kuwa ccm imekuwa kisiasa , kumchagua Dr.bilal kuwa ni mgombea mwenza wa kikwete imekuwa ni suruhisho la diplomatic ndani ya chama cha ccm visiwani zanzibar
kweli kabisa bilali turufu ya ccm kuimaliza zanzibar na sio turufu ya wazanzibar kwa maendeleo yao.
Kwani hao ambao waliwahi kuwa makamo wa raisi wa Tanzania, nani kati yao ambae ameweza au angalau kujaribu kuisaidia Zanzibar? hakuna !!
kwa hivyo na Bilali ndio hayo hayo, tungojee na yeye kubatizwa na kuvalishwa ngozi za kiuno na kupewa mkuki tu, Basssssssssssssssssss!!!!
ASSALAM ALAYKUM ?
BILALI NAE PIA HANA UCHUNGU WA VISIWA VYETU MNFIKI KAMA HAO WENZIWE TU HANA LOLOTE JIPYA ALIKUA MADARAKANI KAFANYA NINI ZAIDI YA KUWAGAWA WAZANZIBAR? KIFUPI WATANGANYIKA SISI WAZANZIBAR TUNATAKA VISIWA VYETU TU NA KAMA KUNA MTU ANATAKA HUO MUUNGANO HEWA BASI AENDE HUKO TANGANYIKA AKAUNGANE NA WEVI WENZIWE HATUTAKI HATUTAKI HATUTAKIIIIIIIIII MUUNGANOOOOO AU MPAKA TUANZE KUUWANA NDI MTAELEWA TUPENI VISIWA VYETU KUUNGANA NA NYINYI IMEKUA BALAAAA LEO WAZANZIBAR WAMEKUA WALEVI DADA ZETU WAMEKUA MALAYA THAMANI YETU YOTE IMESHUKA NA HII NDIO AGENDA YAO YA SIRI HAO WATANGANYIKA KWA KUSAIDIWA NA AMERICA NA ENGLAND WAZANZIBAR AMKENIIIIIIIIIIIIIIII VIZAZI VYETU VITAANGAMIA KWA TAMAA ZETU TUDAI KWA NGUVU AU HIARI TUWE NA VISIWA VYETU OHOOOOOOOO. TUNECHOKA KUDANGANYWA HATUTAKI MARIDHIANIO WALA MSETO TUNATAKA ZANZIBAR YETU.
MSTAHAMILIVU
CCM wameekeza mpaka kwa wasomi…sasa wanawatumia ‘kupiga pasi’ hali ndani ya ccm; lengo ni kuwashusha joto wakereketwa-hafidhina…Kwa kadiri jinsi gani wapemba wanachukiwa ktk siasa za uongozi wa znz, kuna kazi kubwa mpaka kuwafanya wafurukutwa hawa kumkubali shein…labda kidogo ‘msomi’ wetu wa znz Bw. Shamsi aendelee kusimikwa kuwa waziri kiogozi..aendelee na kuchoweya!!
BABAISHA BWEGE
bilal ni turufu ya ccm lakini hata hivyo kwa lile kundi la bilal lilioko zanzibar sifikirii kawa watamuunga mkono shein kwani bilal kuwa makamo wa rais hawezi kuwalipa fidia group yake,pia bilal kuwa makamo wa rais hatusaidii kitu kwa zanzibar kwa umakamo wa raisi ni kama boya kwa zanzibar
Shein alikuwa makamo wa rais lakini hakusubutu kuinua mdomo wake hata siku moja kuongelea suala la muungano kwani yeye alikuwa katika serikali ya muungano,na alikuwa na wajibu pia wa kilishughulikia suala hili.
Umakamo wa urais ni BOYA kubwa kwa zanzibar,na rais wa zanzibar kwa kiti cha ccm ni sawa asistance katika office anvyo itumikia office,kwa hiyo ni kibaraka wa bara,hawawezi kutututea hawa,ccm ipo madarakani miaka isiopungua arubaini nakuendelea,hakuna maendele yoyote zaidi ya kurudi nyuma miaka ya 1912 mana hata taa za barabarani haziwaki tena nyengine wakati zilitakiwa ziwake na sehemu nyengine ziongezwe,tunarudi nyuma kwa kasi sana zanzibar
tuwe makini jamani na tusimame kidete mwaka huu kieleweke ,ni kuitoa ccm madarakani tu basi tungie wenye tulokuwa na uwezo na burara na imani na nchi yetu.