Habari

WATOTO WA KARUME WAPINGANA

Hassan Ali Ame (TANZANIA Daima) Zanzibar

MTOTO wa Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Marehemu Abeid Amani Karume, Balozi Ali  Abeid Karume, amekinzana na kaka yake, Rais mstaafu, Amani Abeid Karume na  wanasiasa wengine wanaodai Zanzibar kuwa na mamlaka kamili (Dola) akisema hilo  litavunja Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Akihutubia mkutano wa hadhara huko Makunduchi Mkoa wa Kusini Unguja, Balozi  Karume alisema kwamba madai ya wanasiasa wanaotaka Zanzibar ipate kiti chake  Umoja wa Mataifa hayana msingi kwa kuwa mamlaka kamili ya Zanzibar  yalikwishapatikana tokea Januari 12 mwaka 1964 yalipofanyika mapinduzi na  kuondoa utawala Sultani.

“Wazanzibari msikubali kuchezewa akili na wanasiasa wanaotoa madai hayo,  Zanzibar kuna Mahakama, Serikali na Baraza la Wawakilishi, hayo ni mamlaka  kamili. Hakuna mamlaka kamili ya uendeshaji wa nchi yanayopindukia hayo,” alisema Balozi Karume.

Akizungumzia historia ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Balozi Karume  alisema ulifanyika kwa malengo makubwa ya kuimarisha udugu na umoja pamoja na  kufungua njia ya Afrika kuwa moja.

Hata hivyo, alisema vijana Zanzibar lazima wakumbuke kabla ya mapinduzi ya  mwaka 1964 Zanzibar haikuwa na raia bali wote walikuwa chini ya Sultani, ndiyo  maana hata Waingereza Desemba 10, 1963 walimkabidhi Mfalme Jamshed bin Abdullah  hati za uhuru kabla ya wananchi kuamua kujikomboa kwa njia ya mapinduzi.

Balozi huyo alisema tokea mwaka 1964 hadi sasa hakuna jambo linalofanyika  kuinyima haki Zanzibar katika mfumo wa Muungano licha ya kuwepo kwa kasoro ndogo ndogo ambazo zimekuwa zikifanyiwa kazi na pande mbili za Muungano.

Alisema wanaotaka Zanzibar kuwa na mamlaka kamili wakifanikiwa ipo siku  watadai kujitenga kwa visiwa vya Unguja na Pemba.

Akifafanua alisema kwamba iwapo mapendekezo ya rasimu ya katiba mpya ya Jaji  Joseph Warioba yatapitishwa kama yalivyo na mabaraza ya Katiba na Bunge lake,  muungano utakuwa katika hatari ya kuvunjika.

Alisema kwamba mfumo wa muungano wa serikali tatu haufai kwa maendeleo ya  Muungano kutokana na kuwa mzigo mkubwa katika gharama za uendeshaji wake na  upande mmoja wa Muungano kuwa na nguvu ndogo za kiuchumi.

Hata hivyo, aliwataka wanachama wa CCM wakati ukifika washiriki kutoa maoni  katika mabaraza ya katiba, huku wakichukua tahadhari kubwa dhidi ya watu  wanaofanya kampeni za kutaka Zanzibar kujitenga katika muungano wa Tanganyika na  Zanzibar.

Alisema kuwa wananchi waende kutoa maoni wakitetea msimamo wa kuendelea na  muundo wa serikali mbili kwa sababu wanaotetea muungano wa mkataba wameshindwa  kuzingatia maslahi ya wananchi wa pande mbili na Muungano wenyewe.

Alisema sera ya mambo ya nje ya Tanzania imekubalika kimataifa ndiyo maana  mataifa yenye nguvu kubwa za kiuchumi duniani ikiwemo Marekani na China wamekuwa  wakitembelea Tanzania na kuunga mkono harakati za kiuchumi.

Sera ya kutaka Zanzibar kuwa na mamlaka kamili katika mfumo wa Muungano  imekuwa ikitetewa na Kamati ya Maridhiano, Rais mstaafu Aman Karume na kuungwa mkono na Makamu wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif Sharif Hamad.

Lakini Rais wa Zanzibar,  Dk. Ali Mohamed Shein amesema haitambui kamati hiyo ya maridhiano ambayo ipo  chini ya Mwenyekiti Waziri wa zamani wa Muungano, Hassan Nassor Moyo.

Wakati huo huo, Maalim Seif ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi  (CUF), amesema kuwa ataendelea kutetea msimamo wake wa kutaka Zanzibar kuwa na  mamlaka kamili katika mfumo wa Muungano licha ya jambo hilo kutozingatiwa katika  rasimu mpya ya mabadiliko ya katiba.

Msimamo huo ameutangaza juzi wakati akihutubia wananchi katika mkutano wa  hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Upenja Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Alisema kuwa nchi yoyote duniani ili ikamilishe sifa ya kuwa nchi, lazima iwe  na mambo manne ikiwemo kutambuliwa kimataifa, ardhi, watu, serikali pamoja na  uwezo wa kuingia makubaliano na nchi nyengine.

Alisema kuwa mabadiliko ya katiba yazingatie umuhimu wa Zanzibar kuwa na  Benki Kuu yake, uhamiaji, uraia, sarafu, na mambo ya nje ili iweze kujitegemea  katika mipango yake ya kiuchumi na kudhibiti mzunguko wa fedha.

Alisema kwamba iwapo Zanzibar itarejeshewa mamlaka yake kutoka katika mfumo  wa Muungano itaweza kujiunga na Umoja wa Mataifa (UN), Umoja wa Afrika (AU)  pamoja na Jumuiya ya Kimataifa ya Kislamu (OIC).

Share: