Habari

Wazanzibari watakiwa kueka mbele uzalendo

Na SALMA SAID

Juma Duni ameyasema hayo alipokuwa akihutubia wafuasi wa chama hicho katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kiwanja cha Komba wapya Mjini Zanzíbar, mkutano ambao umehudhuriwa na wanachama mbali mbali na baadhi ya viongozi wa chama hicho.

Duni ambaye Maarufu huitwa Babu, amesema njia pekee ambayo itawasaidia kupata maslahi wanayoyataka katika Muungano ni kuwepo kwa umoja na mshikamano miongoni mwa Wazanzibari jambo ambalo ni chachu ya mafanikio, na kuwaomba waongeze nguvu katika umoja hasa katika kipindi hiki ambacho Tanzania imo katika mchakato wa kutengeneza katiba mpya.

Ameongeza kuwa kwa muda mrefu Zanzíbar imekuwa ikibanwa na mambo mengi yanayohusu uchumi wake katika Muungano na kwamba sasa ni muda muafaka wa kupigania Muungano ambao utakuwa wa haki na usawa baina ya Zanzíbar na Tanganyika.

Juma Duni ambaye pia ni Waziri wa Afya wa Serikali ya Mapinduzi Zanzíbar amewataka Wazanzibari kuendeleza kudumisha amani iliyopo Zanzíbar sambamba na kutii sheria zilizopo kwa manufaa ya jamii na taifa kwa ujumla.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Jimbo la Mji Mkongwe na Mjumbe wa Baraza Kuu la (CUF) Ismail Jusa Ladhu alisema kuwa Wazanzibari wanachotaka katika Katiba mpya ni Muungano ambao utatoa haki sawa baina ya Zanzíbar na Tanganyika.

Jussa ambaye hutumia muda mwingi kuongea mambo ya Muungano amesema mshikamano ambao waliuonesha Wazanzibari katika kutoa maoni umewajengea uwezo watu wengine kutoka Tanzania Bara kuwaunga mkono katika kutetea Muungano ambao unaipa hadhi Zanzíbar.

Alisema wazanzibari wametumia fursa yao vyema katika kutetea nchi yao na hivyo hali hiyo inawapa moyo viongozi wanaoendeleza harakati za kuikomboa Zanzibar ambapo aliwataka wananchi kuwa pamoja katika kuleta mfumo mpya na wa kisasa ambayo utaondosha kero na matatizo yote yanayojitokeza ndani ya Muungano ambayo yanaonekana kushindikana katika kutetuliwa kwa vikao.

Jussa alisema njia pekee ya kuikomboa Zanzibar ndani ya Muungano ni kutekelezwa matakwa ya wazanzibari waliotoa katika mchakato wa katiba mpya ambayo asilimia kubwa wameunga mkono kuwepo mfumo wa Muungano wa Mkataba ambao utafuatiwa na mshirikiano kati ya nchi mbili zilizoungana ambazo ni Tanganyika na Zanzibar.

Mkutano huo umekuja ikiwa ni mwendelezo wa kuhamasisha uhai wa Chama hicho na kutoa elimu ya Muungano kwa wanachama wa chama hicho na wazanzibari kwa ujumla.

Tagsslider
Share: