Habari

WITO WANGU KWA MASHEIKH WA ZANZIBAR!!

Mr Wisdom

WITO WANGU KWA MASHEIKH WA ZANZIBAR!!

Assalam alaikum,
Nachukuwa nafasi hii kumshukuru Allah kwa kutuwezesha Kuwa waumini na kutupa tawfiiq ya Kuwa vipenzi wa dhati wa Mtume Muhammad (s).

Pia nachukuwa fursa hii kumpongeza rasmi Mufti wa Zanzibar sheikh Swaleh Kaabi na uongozi wake katika kushughulikia suala la Kijana aliyemtusi Kipenzi cha Dunia hii Mtume Muhammad (s).

Lakini naona nitowe WITO muhimu kwa masheikh wote wa Zanzibar na wa Afrika ya Mashariki kuujuwa wakati na matatizo ya jamii tunayoishi karne hizi na hasa katika suala la kuukashifu Uislamu, Mtume na vitu vitukufu vya Uislamu!

Vijana wengi zaidi Leo kinyume na karne zilizopita wameweza kusafiri kwenda kwenye nchi za Kiarabu na nchi za Ulaya na wameona mengi yanayojiri kwenye nchi hizo na kukumbana na mitihani au shida na raha kama ilivyo katika maisha.

Vijana wengi wanaokwenda Uarabuni wanasikitishwa na namna wanavyo tendewa na waisilamu wenzao na wanapokuja huku Ulaya huyasema hayo wanayotendewa kinyume na matakwa yao hadharani au kwenye mitandao ya kijamii, jambo ambalo watu wengi linawapa wasi wasi juu ya uwezekano wa Uislamu Kuwa ni Dini sahihi (ewe Allah tuthibitishe katika Dini yako) Amin!!

Huku Ulaya Vijana wengi hukirimiwa Chini ya mwanvuli wa haki za kibinaadamu na kanuni zisizobaguwa watu kwa kabila, rangi au dini kwa kiasi kikubwa ingawa udhaifu huonekana hapa na kule hata hapa Ulaya Lakini kwa sura iliyo rasmi Ubaguzi au chuki za kisiasa na kikabila kama zinavyojitokeza kwenye mataifa ya Kiislamu Ulaya hakuna sana, kwa mtazamo wa akili changa na ya ujana Vijana wengi wanaweza kughilibika kuukosowa Uislamu na hasa pale wanapo watazama watu wanavyowatendea hapo Mashariki ya kati na wanapoona picha sahihi ya kuuwana kwa miaka mingi kati ya waisilamu!!!

Majuzi hivi alionyeshwa kwenye TV ya Kimarekani Kijana Hussain ambaye ni kutoka Afghanistan, alipoulizwa kwa nini katoka kwenye Uislamu kajibu Kuwa tangu alipozaliwa mpaka Leo hajashuhudia amani wala upendo katika nchi yake kati ya hata watu wanaosali msikiti mmoja!! Anasema baba yake aliuliwa na waisilamu na sio makafiri kwa hiyo kuna haja gani yeye kujinasibisha na Dini yenye kuuwa wafuasi wake???

Pia huko Sweeden kuna msichana wa Kisomali ambaye amertadi sababu zake ni Kuwa Uislamu hauna Upendo na watu wake Huko Somalia wanauwana tangu alipozaliwa hadi Leo hii na anasema anamshukuru Yesu kwa kumkombowa na Dini yenye kuwafanya wafuasi wake wawe maaduwi wao kwa wao na wenye kuuwana wao kwa wao!!!

Hii ndio hali ya karne tunayoishi enyi Masheikh mnaokuwa tayari kumhukumu mtu anayedaiwa kurtadi kwa kumkata kichwa bila ya kuyatafiti matatizo yake na mazingira yake, ipo haja ya kuundwa kwa Jopo la Masheikh kushughulikia suala hili haraka iwezekanavyo!!

Hii ni hatari kubwa Masheikh kama hatukufanya wajibu wetu kuna uwezekano wa Kuwa na watu wengi kama Abdullah wengine ambao wako Chini kwa Chini wakiogopa kujitokeza.

Maombi yangu kwenu ni kutayarisha Jopo maalum la wataalamu watakaokuwa na dhamana ya kuwaita watu kama Dr Abdullah na naomba kwa baruwa hii tuanze na huyu huyu Dr. Abdullah aitwe mbele ya Maulamaa na Wataalamu aulizwe live nini hasa matatizo yake katika Uislamu au ni kitu gani hasa kinachomfanya awe na shaka na Uislamu?

Naomba Dr. Abdullah aulizwe hayo mbele za masheikh bila ya vitisho na kwa hekima kubwa kwa sababu Uislamu haujapatapo kuogopa kujibu hoja za makafiri wala wapinzani wake.

Basi ni wajibu sisi kutambuwa nini hasa kimewasibu Vijana wetu na kujaribu kujibu matatizo yao au masuala yao si hivyo huenda tukawakosa Vijana wengi na hasa kutokana na Dunia Kuwa ndogo na kuweza kupata habari za kila pembe za Dunia kwa urahisi!

Leo hii na katika Karne hii kuna watumwa wanauzwa na kufugwa huko Yemen, Mauritania, Mali na Sudan na hii sio siri tena kwa sasa Ulimwenguni, Vijana wanauliza kama huu ni Uislamu (nina hakika si Uislamu wa Mtume Muhammad huo) jee Allah kweli ataruhusu watu kuuzwa na kununuliwa kama Badia au kachori??

Lakini masheikh tumeinyamazia batil kwa muda mrefu mpaka Vijana wameelewa Kuwa haya ni batil baada ya kuambiwa hayo na maaduwi wa Uislamu, sasa kwa Kuwa tumeinyamazia haki na tukakaa kimya kwa sababu mambo hayo yanatendwa na Iran, au Saudia, au Yemen au Oman au Misri, kwa kuogopa Masheikh wa nchi hizo ambao nao wamekaa kimya au kuogopa kutopewa misaada na nchi hizo, naamini tutaendelea kulipa gharama kubwa kwa kutokea watu kama hawa Watakao mtukana Kipenzi chetu hadharani au kwa kufanya kampeni za siri za kuwatowa watu kwenye Uislamu na haki.

Naomba tuachie sharia ichukuwe mkondo wake kama TAARIFA YA MUFTI WA Zanzibar ilivyosema, Lakini masheikh tujitayarishe na kujibu hoja za Vijana ambazo huzipata amma kutoka kwenye mitandao, au kwa kukatana na mitihani ya nchi za Kiarabu na za Ulaya au kutokana na wasi wasi wa shetani.

Tunamuomba Allah ainusuru Zanzibar na watu wake na azilinde nchi zote za Kiislamu na mitihani ya vijana wake, Amin!!!

Share: