Habari

YALIYOJIRI KATIKA SEMINAR KUHUSU KATIBA YA TANZANIA (UK)

Hatimaye Taasisi ya kijamii ya Uingereza na Tanzania (British – Tanzania Society, UK) wamefanya semina kubwa siku ya Jumamosi wiki katika ukumbi wa chuo kikuu cha London, SOAS hapa nchini Uingereza. Semina hiyo ambayo imeleta msisimko mkubwa kwa wajumbe na watu wengine mbali mbali waliouhudhuria umejumuisha wasemaje wakuu wanne, ambao walijadili mambo tafauti yahusianayo na katiba.

Semina hiyo ambayo mwenyekiti alikuwa Bwana Andrew Coulson, ilimwaalika msemaji Fredrick Longino ambaye alizungumza kwa upana matarajio ya wananchi hasa kwa upande wa bara juu ya katiba mpya. Msemaji wa pili alikuwa Profesa Abdul Paliwala ambaye alizungumza suala la katiba kwa mtazamo wa kisheria nchini Tanzania .
Yussuf Hamad, mhadhiri chuo kikuu cha London, SOAS alizungumza kuhusu nafasi ya Zanzibar na matarajio yake katika katiba pendekezwa. Mwisho alizungumza mwanablogu maarufu ambaye alikuwa mwanamke pekee katika mjadala huu Mwanadada, Aikande Kwayu ambaye alizungumza kuhusu nafasi ya wanawake katika katiba inayopendekezwa.
Pamoja na kutolewa kwa hoja nzuri na wachangiaji wawili wa mwanzo, yaani, Bwana Abdul Paliwala na Dr. Longino, mjadala ambao uliamsha maswali mengi na mbishano mkubwa ni ule uliotokana na mchango na maoni yake aliyotoa kuhusu nafasi ya Zanzibar katika Katiba pendekezwa ambapo baada ya kumaliza kuwasilisha tu, alijikuta akivurumishwa maswali kutoka kwa wachangiaji.
Mmoja kati ya wachangiaji waliomsakama na kupingana vikali na maoni yake ni mwandishi wa BBC Swahili Bibi Zuhura Younis, ambaye alianza kwa kumpongeza Bwana Hamad kwa kuweza kuwasilisha hoja za muungano na katiba kutoka Zanzibar bila kuonesha kuegemea itikadi ya chama chochote cha siasa. Mara baada ya hapo Bi Zuhura alianza kwa mjadala wenye msisimko uliotosha kuitwa mechi!
MATCH OF THE DAY: Yussuf Hamad Vs Zuhura Younis

Hoja: Alichokisema Hamad ni kuwa Zanzibar kiujumla ilihitaji Muungano wa mkataba. Akaongezea kwa kusema kwamba Wazanzibari walihitaji katiba ambayo itaondoa kero za muungano ambazo zimekuwa zikileta sintofahamu kwa muda wa miaka zaidi ya 40.
Akasema, kuwa Wazanzibari wanahitaji muungano wenye kufuata misingi ya usawa, sio usawa wa uwiano lakini usawa wa maridhiano ya kila maamuzi yanayofanywa katika Muungano. Alitoa mifano ya kero mbali mbali za Muungano kama vile mgao wa Zanzibar wa mapato katika muungano, mapato, bandari, petrol na mambo mengine ambayo kwa kuongezwa kwake yamekuwa sababu ya mgogoro kati ya washirika wa Muungano.

Bwana Hamad alihitimisha kwa kusema, Wazanzibari hawaukatai Muungano ila wanahitaji Muungani wenye misingi ya usawa na kuheshimiana. Na kwa maana hiyo katiba nzuri yenye maslahi kwa Zanzibar ni ile itakayotokana na misingi ya usawa (Fairness) baina ya washirika wa Muungano. Pia alisistiza kuwa, ili kuondoa kero nyingi na migogoro ya kikatiba isiyokwisha, ni vyema kwa Tanzania kuzingatia katiba yenye kuzingatia matakwa ya wananchi walio wengi na sio inayosimamia misingi ya kivyama, dini wala kikabila.
Idadi ya wachangiaji kutoka Zanzibar kwa bahati mbaya ilikuwa haizidi watu wanne katika ukumbi. Kwa maana hiyo, michango mingi ilitokana na watu kutoka Tanzania bara ambao walionekana kubaliana na mengi yaliyozungumzwa na wasemaje wote. Pia walitoa michango endelevu sana hata kuhusu hoja za nafasi ya Muungano na Katiba kwa upande wa Zannzibar.
Hata hivyo, Bi Zuhura Younis, ambaye ni mmoja kati ya Wazaznibari wachache waliohudhuria alipingana na karibu hoja zote. Kwanza alianza kwa kusema kuwa Wazanzibari, hasa wa upande wa pili, wamekuwa wakilalamikia muungano kila siku, kama kwamba Muungano huo hauna jema lolote kwa Zanzibar.

Pamoja na hilo akaongezea kuwa kero ziko lakini ni ndogo ndogo sana na akasisitiza kuwa mgao wa asilimia 4.5% wanaopatiwa Zanzibar ni sahihi kwa sababu Zanzibar ni nchi ndogo sana kiidadi ya watu ukilinganisha na idadi ya watu walioko bara. Kwa hiyo hakuna haja ya kulalamika lamika.
Bi Zuhura aliisuta kauli ya Bwana Hamad kuhusu mafuta akisema, Zanzibar hakuna mafuta kamwe na kwa maana hiyo hakuna haja ya kujenga mlima kwa kichuguu cha sisimizi kwa kitu ambacho hakipo kabisa. Akihitimisha maoni na michango yake, Bi Zuhura alidai kuwa katiba iliyopo inaifaa sana Zanzibar na inalekea kwamba malalamiko makubwa ya katiba yanatokana na kelele za wapinzani ambao ni sehemu tu ya wananchi wa Zanzibar ambao nusu ni CCM na nusu ni CUF kiujumla.

Alipopewa nafasi ya majumuisho na kufafanua hoja alizozisema na zile zilizochangiwa, Hamad, alianza kwa kusema kuwa kumekuwa na dhana iliyojengwa kwa makusudi ili kuwadunisha watu fulani kutoka upande fulani kwa kuwahukumu kisiasa isivyo haki na kukana hoja zao kwa misingi hiyo. Alitoa mfano kwa kusema, katika mijadala kama hii, wasemaje wengi wanaposikia anayezungumza ni Mzanzibari au Mpemba, basi huyo huitwa ‘Mpinzani’ wa muungano hata ikiwa mtu huyo hana mfungamano na chama chochote.
Alifafanua pia kwa kusema kwamba baadhi ya wanasemina walimfahamu vibaya alizpozungumza neno ‘Fair’ wakidhani alimaanisha ‘equality’. Kwa ufupi alichokusudia kusema ni kuwa kuwe na msingi ya haki na usawa katika kufanya maamuzi ya mambo ya muungano. Moja kati ya mambo hayo ni kuwashirikisha wananchi wa pande zote mbili kwa msingi ya ukweli na uwazi. Alihitimisha kwa kusema kwamba Katiba yenye kujali na kusikiliza maoni huru ya wananchi walio wengi, ndio suluhisho moja la migogoro inayoweza kuunusuru Muungano wa Tanzania.

Tagsslide
Share: