Zanzibar yatuma ujumbe kujifunza Ulaya

Written by  //  06/09/2010  //  Habari  //  1 Comment

Na Mwinyi Sadallah
6th September 2010

Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Pandu Ameir Kificho

Zanzibar inatuma ujumbe wake kwenda nchi za Ulaya zikiwemo Uingereza na Ujerumani, kujifunza muundo bora wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (GNU).

Taarifa zilizopatikana mjini hapa zilieleza kuwa ujumbe huo, utaongozwa na kamati ya watu sita wakiwemo viongozi waandamizi serikalini.

Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Pandu Ameir Kificho, alithibitisha kuwepo kwa safari hiyo baadaye mwezi huu, lakini alisema ni mapema kueleza ujumbe huo utaondoka lini.

Kificho alisema hatua hiyo imefikiwa ili kupata uzoefu jinsi ya kuendesha serikali ya umoja wa kitaifa, baada ya marekebisho ya 10 ya Katiba ya Zanzibar.

“Mpango huo upo na serikali ndiyo inayoushughulikia, siwezi kusema lini utaondoka, lakini ni kweli Uingereza na Ujerumani zimeonesha nia ya kusaidia mafunzo hayo,” alisema Kificho.

Kificho alisema serikali ya umoja wa kitaifa itaundwa baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, hivyo ni vizuri kupata uzoefu wa kuendesha serikali ndani ya Baraza la Wawakilishi, kwa vile kutakuwa na serikali na Baraza la Mawaziri Kivuli chini ya mfumo huo.

Uchunguzi wa NIPASHE ulibaini kuwa safari hiyo itawahusu wajumbe sita wa kamati ya kusimamia serikali ya umoja wa kitaifa, wakiongozwa na Mwenyekiti wake, Ali Mzee Ali na Katibu Mkuu wa Baraza la Mapinduzi, (BLM) Abdulhamid Yahya Mzee.

Wajumbe wengine wanaotarajiwa kuwemo kwenye msafara huo ni Kiongozi wa upinzani ndani ya Baraza la Wawakilishi, Abubakar Khamis Bakar na wawakilishi, Haji Omar Kheri (Tumbatu) na Ali Abdalla Ali (Mfenesini).

Wengine ni Zakia Omar Juma (Viti Maalum) na Nassor Mazrui (kuteuliwa na Rais).

Spika wa Baraza la wawakilishi zanzibar

One Comment on "Zanzibar yatuma ujumbe kujifunza Ulaya"

  1. intihan 07/09/2010 kwa 1:52 um ·

    Ni fikra nzuri, tunawatakia kila la heri katika safari yao, inshallah waende slama na warudi slama

Comments are now closed for this article.