CCM iwaache Wazanzibari wapitishe mgombea urais wanayemtaka

Written by  //  09/07/2010  //  Makala/Tahariri  //  3 Comments

Lula wa Ndali-Mwananzela
Julai 7, 2010

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kinaamini kuwa Wazanzibari wanaweza na kwa hakika wanayo haki ya kuamua hatima ya muundo wa serikali yao kiasi cha kukubali wafanye mazungumzo ya upatanisho bila msaada wa Bara na hatimaye kuridhia kufanyika kwa kura ya maoni yenye kuruhusu, hatimaye, serikali ya mseto huko Visiwani.

CCM inaamini Wazanzibari wanajua ni kitu gani kinawafaa na kitu hicho kiwe vipi. Imani hii ya CCM kwa Wazanzibari imebakia kwenye masuala hayo tu; linapokuja suala la urais wa Zanzibar, CCM Zanzibar imenyimwa haki ya mwisho.

Tunapoelekea siku chache ambapo tutamtambua mgombea wa kiti cha urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM, ‘mchezo’ mzima unahamishwa kutoka Zanzibar na kupelekwa Dodoma ambako hatimaye majina matatu (kati ya watu 11 waliojitokeza) yataibuliwa na Halmashauri Kuu ya Taifa ili hatimaye yapelekwe kwenye Mkutano Mkuu ambapo jina moja litapitishwa kuwa mgombea wa CCM huko Zanzibar.

Sasa ukiuliza kwa haraka haraka jibu utakalopewa ni kuwa: “Huu ndio utaratibu wa CCM”, lakini ukiangalia kwa karibu utaona kuwa ni utaratibu mbovu ambao unatokana na uchakachuaji wa demokrasia ambao CCM imeufanya kwa muda mrefu sasa. Wakati mwonekano wa demokrasia unapigiwa mbiu, demokrasia yenyewe inapigwa vita kiaina!

Tujiulize kama CCM inaamini kuwa Zanzibar inaweza kuwa na baraza lake la kutunga sheria kwa mujibu wa mkataba wa Muungano, na kuwa hivi karibuni wameweza hata kuwa na bendera yao na wimbo wao wa taifa, na kuwa Wazanzibari wanaweza kuamua suala zito na nyeti kama kuweza kubadilisha katiba yao na kurusu kura ya maoni ambayo itabadilisha mfumo wa utawala visiwani humo, inakuwaje Wazanzibari hao hao washindwe kuamua mgombea wao wa mwisho awe ni nani?

Hili linatokea kwa sababu japo CCM inaamini (na inayo sababu ya kuamini) kuwa Wazanzibari wana uwezo na mwamko mkubwa wa kisiasa lakini linapokuja suala la vitendo, CCM inaogopa mwamko huo.

Kutokana na ukweli huo Wazanzibar japo wanauwezo wa kuchagua wagombea wao, uwezo huu umechakachuliwa na utaratibu mbovu wa CCM kama unavyoonekana katika Katiba ya CCM.

Sasa ni utaratibu mbovu kwa sababu moja kubwa, kwamba suala la mgombea ambaye atapigiwa kura kwenye uchaguzi mkuu na Wazanzibari tu linaamuriwa na watu ambao hawana nafasi ya kupiga kura baadaye. Yaani, kwa nini jina la mgombea wa kiti cha urais wa Zanzibar lipitishwe na kikao kikuu cha chama na kupigiwa kura na watu ambao hawana kura katika uchaguzi wa Zanzibar?

Kwa nini watu wa Mwanza, Iringa, Kigoma na kwingineko wawe na uamuzi wa mwisho wa nani agombee huko Zanzibar wakati wao hawana nafasi ya kwenda kupiga kura huko? Huu ni uchakachuaji wa demokrasia.

Chama cha Mapinduzi kilitakiwa kuhakikisha kuwa demokrasia inakuwepo kwa CCM Zanzibar linapokuja suala la mgombea wake. Hili lingeweza kufanyika kwa vikao vya CCM Zanzibar kufanya maandalizi ya kupokea fomu za wagombea wa urais, kuwachuja na hatimaye kuandaa mdahalo (hata miwili) ambapo wagombea hao wanaelewa misimamo yao mbalimbali kuhusu Zanzibar na Taifa kwa ujumla ili baadaye Mkutano Mkuu wa CCM Zanzibar upitishe jina la mgombea wake.

Mgombea ambaye angepatikana kwa namna hiyo ndiyo angetambulishwa kwenye Mkutano Mkuu wa Taifa kuwa ni chaguo la CCM Zanzibar.

Lakini hili haliwezi kutokea kwa sababu katika demokrasia iliyochakachuliwa na CCM, kufanya hivyo kungewapa uhuru mkubwa sana Zanzibar. Uhuru wa hatimaye kuchagua mgombea wake pasipo kile ambacho kinajulikana katika siasa za Dodoma kuwa ni “mizengwe”.

Kwa vile hili ni kweli, basi, ni ushauri wangu kuwa kama CCM inataka kuonyesha kuwa imeanza kusafisha demokrasia (baada ya kuichakachua kwa muda mrefu sasa) basi iamue mapema kuwa majina ya wagombea wa kiti cha Zanzibar, kama yalivyo, yatarudishwa kwa Mkutano wa Uchaguzi wa Zanzibar ambapo wajumbe wake waweza kuwa ni wabunge wote wa CCM wa Zanzibar, wajumbe wa NEC (Taifa) kutoka Zanzibar na wajumbe wengine kama inavyopasa ambao ndio watawasikiliza wagombea wanaotaka kugombea wajieleze na kuhojiwa maswali na hatimaye wapigiwe kura ambapo yule aliyepata kura zaidi ya asilimia 50 +1 ndiye atakuwa mgombea.

Ninaamini kwa kufanya hivyo kuna mambo kadhaa ambayo yatatokea mara moja. Kwanza, kutarudisha nguvu ya kisiasa Zanzibar ambapo uongozi kwa upande wa CCM unapatikana kwa njia ya kidemokrasia kuliko ilivyo sasa ambapo hatima ya Zanzibar inaachiliwa kwenye Halmashauri Kuu ya Taifa.

Jambo jingine ambalo laweza kutokea ni kuwa hatimaye katika mchujo mzuri wa siasa Zanzibar, Wazanzibari watapata mgombea wanayemtaka hasa, na siyo anayetakiwa na watu kutoka Dodoma kwa mtindo wa kubebana kama ilivyotokea mwaka 2000.

Kwa kurudisha maamuzi ya nani agombee kwa wana CCM huko Zanzibar, CCM itaonyesha, hatimaye, kuwa inaamini Zanzibar inaweza kujipatia mgombea wake mzuri ambaye anaweza kushindana na mgombea wa chama kingine chochote, na kuwa, kwa vyovyote itakavyokuwa, atakuwa ni chaguo la Wazanzibari.

Ni wito wangu kuwa CCM iache uoga wa kutoamini kuwa wana CCM Zanzibar wana uwezo wa kuwapima wagombea wake vizuri na hatimaye kumchagua aliye bora kati yao kuwa mgombea wa kiti cha urais. Hii ina maana ya kwamba hata kama mgombea huyo atashindwa kwenye uchaguzi mkuu, atashindwa kwa haki, na wana CCM watatambua kosa walilolifanya na hivyo kujiandaa tena baada ya miaka mitano.

Isije kuwa mtu akashindwa uchaguzi na wana CCM Zanzibar wakarudisha tuhuma na madai mazito dhidi ya uongozi wa CCM Dodoma kuwa walimbeba mgombea fulani kwa sababu ndiyo CCM taifa ilimtaka.

Hivyo, wito wa makini ni kuwa CCM Taifa irudishe mara moja na pasipo kujing’ata ulimi, uamuzi wa kutafuta mgombea wa urais Zanzibar kwa tiketi ya CCM kwa wana CCM Zanzibar.

Mikutano itakayofanyika siku hizi chache zijazo iwe ya kupanga utaratibu wa jinsi gani wana CCM Zanzibar, katika kikao maalumu, wataweza kupitisha jina moja kati ya haya 11 kupata mgombea wake.

Mchakato unaweza kuwekwa kuwa na hatua mbili, hatua ya kwanza ambapo majina mawili yaliyopata kura zaidi ndiyo yatapitishwa na halafu hatua ya pili ambapo majina yale mawili yatapitishwa na kugombea ambapo jina la mgombea litapatikana.
Utaratibu uwe kwamba yule atakayepata kura zinazofuatia ndio atakuwa ni Waziri Kiongozi endapo CCM watashinda. Ni muhimu hao watu wawili wawekewe mazingira ya kuweza kufanya kazi pamoja.

Hata kama utaratibu huu unaweza usiwe mzuri (wa Waziri Kiongozi kuwa ni yule anayefuata kwa kura za mapendekezo), lakini la muhimu kuwa wana CCM Zanzibar waachwe waamue ni nani wanataka awe mgombea wao huko Zanzibar wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Rais.

Vinginevyo, Zanzibar itaendelea kulipa gharama ya demokrasia iliyochakachuliwa na CCM!

3 Comments on "CCM iwaache Wazanzibari wapitishe mgombea urais wanayemtaka"

  1. balozi mchafu 09/07/2010 kwa 10:22 um ·

    jamani hii inauma bwana …..hata kama wote sawa lakini kuna haja ya kupata unwyemtaka

  2. shamuhuna 10/07/2010 kwa 2:07 mu ·

    Mimi nakuunga mkono muandishi mia fil mia na uyasemayo kusema ukweli yameshajidhihirisha…
    CCM mfuwa wao wa kidemokrasia unapinga uhuru wa maamuzi kwa wazanzibar..wanachama wa CCM zanzibar wana haki ya kushiriki mchakato wa kumpata mgombea urais wa Tanzania kupitia kiti cha CCM ila sifirikii kama kila mwanachama wa CCM tanzania ana haki ya kushiriki mchakato wa kumpata mgombea uraisa wa Zanzibar kwa kiti cha CCM..hii ni kitokana kuwa sio wanaccm wote tanzania wana haki ya kupiga kura zanzibar,vyereje washiriki katika kumchagua mkombea..Huko si sawa na kuchagua nyimbo wakati we sio unamlipa muimbaji!!?

    Hii mie nahisi ilikuwa ni dhana yao toka hapo awali walipo ianzisha CCM na nahisi huu ulikuwa ni mpango kambambe wa Nyerere,wazanzibar hatukuliona hili!ila sasa linajitokeza na tunaanza kuliona na kuona dosari zake,ila kiukweli hii ilikuwa ni nia mbaya juu ya zanzibara nzima na kwa CCM kama tunvyofikiria!!..kwa jinsi ya siasa za zanzibar zinavyoenda sasa,na mchakato mzima wa Muungano unavyo onesha dosari zake,nahofia sana kwa CCM kwa zanzibar soon itabaki jina tuu!!hakutakuwa na mzanzibar yeyote atakae kubali kuchaguliwa kiongozi maishani mwake na hili tutakuja kuliona…Iwapo CCM hawatobadili mfumo wao wa kisiasa na kuwapa zanzibar uhuru wake..Basi CCM zanzibar itabakia jina tuu!!

  3. fadhil 10/07/2010 kwa 10:41 mu ·

    Ni kweli Zanzibar mara zote tunapelekwapelekwa tu hilo Shein hatuna hata haja nalo.Kwanza itakuwaje Rais wa Zanzibar achaguliwe Bara? hiyu sio democrasia kwani sisi hatuwezi kuchagua kiongozi? jibu ni tunaweza ki vipi aletwe kutoka bara!! Bila shaka hizi ni njama makusudi zimepangwa za kuimaliza zanzibar, Bilal na Shamsi wanatakiwa sana tu. Au wabara wanafurahi sana Zanzibar ikimwagika damu? kweli huu niuungwana? WATUACHE TUMCHAGUE WENYEWE TUNAEMTAKA
    SHEIN HATULITAKI………………

Comments are now closed for this article.