Makala/Tahariri

CUF MNAELEKEA WAPI JAMANI?

TAFAKURI YA BABU.
CUF MNAELEKEA WAPI JAMANI?

Said Miraaj Abdulla

Huko nyuma niliwahi kuandika makala fulani kuhusu mgogoro unaoendelea katika chama cha CUF na nikatanabahisha juu ya tabia ya kutukanana na kuanza kupigana wenyewe kwa wenyewe na athari zinazoweza kutokea.

Bila ya kujali nani kafanya nini, baada ya tukio lililotokea leo la kushambuliwa waandishi wa habari, kupigwa watu kadhaa na wengine kujeruhiwa ikiwa ni pamoja na uharibifu wa mali; KWA MTAZAMO WANGU sasa wakati umefika wa kufanyika yafuatayo:-

Viongozi wa CUF na wanachama wake watafakari kwa kina madhara ya mbegu wanayoipanda kwa chama chao, katika jamii, katika tasnia ya siasa na hata kwa wao wenyewe binafsi kama mtu mmoja mmoja na familia zao.
Viongozi wa juu wa CFU wanaoongoza pande zinazo kinzana wakemee kwa dhati tena hadharani tabia hizi ovu na kuwataka wafuasi wao kuwa watulivu wakati wakitafuta haki ya kila upande huko mahakamani, tena bila kushutumiana.

Mahakama iharakishe kusikiliza mashauri ya CUF na kutolea maamuzi ya haki tena kwa uadilifu mkubwa ili mwenye haki ya ushindi afanye shughuli zake za kisiasa kwa salama na atakaeona kuwa upande ulioshinda hawezi kufanya nao kazi atafute pahala pengine pa kufanyia siasa, na huo ni uugwana tosha.

Wazee wa CUF wasio na upande katika mgogoro huu wakishirikiana na viongozi wa dini wanaoheshimika na kukubaliwa na pande zote mbili kuingilia kati mgogoro huu kwa maslahi ya taasisi hio na umma kwa ujumla.
Viongozi wa CUF wapunguze jazba na kiburi wakubali mapatano ya kusimamisha mapigano na kuongezeka kwa hasama miongoni mwao, kwa kuvumiliana huku wakiendelea na shauri lao mahakamani.

Kwa kua makundi yote mawili yameamua kila uchao kutumia vyombo vya habari kama ni ngao au silaha dhidi ya propaganda zao za kisiasa, nawaomba Ndugu zangu Waandishi wa habari waache kuandika habari zozote za choko choko, kashfa au dharau kutoka upande mmoja dhidi ya mwengine miongoni mwa wanachama wa chama hiki, na badala yake wajikite katika kuandika habari za maendeleo ya chama hiki kama zipo, ikiwa ni pamoja na kusaidia kupunguza mgogoro huu kwa kuonyesha njia ya kuufanya umalizike kwa amani.

Ili kurejesha imani ya viongozi wa vyama vya siasa na heshima ya ofisi ya Msajili wa vyama Vya siasa kama chombo muhimu kwa mahusiano ya kisiasa, mapatano, maridhiano, ujenzi wa demokrasia na kuvumiliana katika nchi yetu na kwakua Msajili binafsi amekua sehemu ya mgogoro huu na ana tuhuma dhidi ya uaminifu na uadilifu wa utendaji wake katika mahakama na anapaswa kujitetea kwa jambo hilo, ni wazi kwamba analazimika kuwa na maslahi binafsi katika kesi hii na kulazimika kushirikiana na upande anao tuhumiwa nao kwa pamoja jambo ambalo kwa kwawaida tuu haliwezi kumfanya tena kutoa maamuzi yoyote na kuaminiwa kuwa ni ya haki kuhusiana na chama hiki kikongwe na chenye nguvu za kisiasa katika bunge kwa mtazamo wa haki, hivyo ni vyema kwa Jaji Mutungi kuacha kutoa maamuzi yoyote kuhusiana na chama hiki kwa sasa na pia kujitazama upya katika nafasi yake aliyokabidhiwa na Rais.

Kadhalika ni wakati sasa wa Waziri Mkuu ambae ofisi ya Msajili iko chini ya dhamana yake kwa hekima na busara kubwa kutoa muongozo kwa ofisi hio na pia jeshi la Polisi nchini kuwa waangalifu na waadilifu katika kushughulikia jambo hili la CUF kabla na baada ya maamuzi ya Mahakama ili kuzuia uvunjifu wa amani na umwagaji wadamu unaoendelea na usiojuilikana mwisho wake katika chama cha CUF.
TUTAFAKARI PAMOJA.

FB

Share: