Makala/Tahariri

JEE, KASI YA UJIO WA MAJENGO MAREFU UNAENDANA NA KASI YA UTAYARI WETU KUKABILIA NA JANGA LA MOTO?

Salim Zindu

1. Hilo suala ni mtambuka kama ulivo UKIMWI, kwani kila mmoja wetu lina muhusu na ana nafasi ya kujiuliza juu ya utayari wake linapokuja juu ya suala inalohusu janga la moto. Kama ilivokuwa madhara yake huwagusa watu wengi na utayari wake unawagusa watu wengi pia

2. Watu walipata kusema, ” Ukiona vilemba vimeroa, usiulize seruni ( shuka , msuli au kikoi) Ukiona nchi ziliokwishaendelea, zenye tekinolojia ya hali ya juu, zenye tahadhari na umakini mkubwa, nchi zenye utajiri wa kupindukia. majanga ya moto ni matokeo yasiochukua muda mrefu kutokea je sisi . Hii manake sisi tunahitaji tuchukue hadhari mara mbili zaidi. Sijui kama hilo llinaafanyika au bezo linatupiga matonge.

3. Tunapojenga majengo yetu ,tunaweka hakiba na kujiuliza je moto vipi ukitokezea? Inaonesha tunajiamini kuwa hakuna moto wowote utakao tokezea. Tunasahau kuwa ” Accidents happen even in most casual houses” Ikiwa ajali hutokezea hata kwenye nyumba zenye hadhari kubwa , je kama haina hadhari hali itakuwaje? Hizo ajali zitapiga kambi na kulala humo humo?

4. Nakumbuka miaka ya 60, hapa petu Chake Chake, kumbi kubwa zilikuwa ni zile za senema.Sasa ni zaidi ya nusu karne lakini walizingatia sana uwezekano wa kutokea moto na usalama na waliokuwemo.. Kwanza kila sehemu ilikuwa na milango miwili ya kutokea inayofungukia nje. Juu ya kila mlango huekwa taa ya kandili pindipo umeme ukazimika basi watu wajue mlango upo wapi. Kulikuwa na vitangi maalumu vyente maji ya kuzimia moto na kubadilishwa kila baada ya muda.Pia kulikuwa na ndoo za mchanga kwa matumizi hayohayo na makatazo ya kuvuta sigara. Kuta zake zilikuwa ndefu kuruhusu hewa chafu kupaa juu na kutokea kwenye madieisha maalum yalioekwa kwa kazi. Kama hio haitoshi kuliwekwa mafeni mawili yenye nguvu ya kutolea hewa chafu nje.

5. Sasa tuna kumbi nyingi karibu kila pembe. Ukipata nafasi siku moja ya kuingia , angalia zinalingana vipi na zile za kizamani? Kuna maboresho yoyote au ni afadhali zile za kale? Upime utayari wetu wa janga la moto pindi likitokezea ni kiasi gani.

6. Tuangalie majengo yetu marefu yanayochomoza kama uyoga. Tuanze juu kwenye paa. Kuna mapaa aina mbili. Angali pichani. Kuna mapa fleti kama kiwanja na kuna mapaa yenye chogp , mapaa tulioyazoea ya pembe nne. Kwa mtazamo wangu kwa nyumba zenye ghorofa nyingi mapaa ya pembe nne yanaweza kuwa changamoto unapotokea moto ghorofa za katikati.Unapotokea moto katikati inakuwa chini hakufiki ki na suluhisho ni kupanda juu. Kama juu kuna paa la pembe ndio kumeshazibika hakuendeki. Lakini kama ni fleti , huwa nafasi nzuri ya kujikusanya na kusubiri kudura ya Mungu. Uwokozi unaweza kufanyika kama ni kwa helikopta au kwa kuekwa mabao na nyumba jirani au kwa vyovyote na huku jitihada za kuuzima zinafanyika.

SEHEMU YA PILI

1 Uwezekano wa kutokea moto sasa ni mkubwa zaidi kuliko wakati mwengine wowote, na kutokuwa na utayari kwa kuogopa gharama ni sawa na kupikia debe kutafuta upuchu ukapata ushuku. Ikiacha utayari wa paa la nyumba kuweka mzingira mazuri ya kimbilia utokeapo moto lakini humo ndani ya majengo yetu mukoje? Mie sijui, lakini niulize. Siku hizi kuna utamaduni wa kuweka manondo kila dirisha na milango, ukitokea moto kuna milango ya dharura ( Safety doors) Unaweza kutokea moto ikawa wa nje hana namna ya kuingia ndani kutoa uokozi lakini na alie ndani milango na mageti ya chuma, kufuli zimesha nock kwa moto hazifunguki ikawa ni kufa ukijiona. Lazima pawe na safety doors zinazoeleweka. Je zipo? Mie sijui.Siku moja niliingia kwenye ukumbi mmoja hapa Chake nikakuta madirisha yote yana nondo, una mlango mmoja tu nyuma na unachukua watu wengi kiasi. Nikaangalia mlango au dirisha la dharura sikuliona, nikaucheki ule mlango wenyewe, jee unafungukia wapi? Niasema mtume wangu, mjenzi na mjengewa, vipi? Najua walio wengi hawaiona hatari iliojificha.

2.Majengo yetu yana kengele kutoa taarifa ya moto? ( Alarm bell) Mimi sijui. Kunafanyika zoezi kama utatokea moto itakuwaje angalau mwaka mara moja? Kuna machupa na ndoor za kuzimia moto na watu wanajua kuzitumi? Mie sijui. Kuna taa za chaji milangoni kama umeme utazimiakaau kuzimwa wakati wa janga la umeme? Mie sijui Kuna ukaguzi wa nyaya za umeme na vifaa kila baada ya muda? Mie sijui.

3. Je majengo yetu yanakaguliwa baada ya kujengwa kabla ya kuhamia au mtu akimaliza kujenga anahamia wala hakuna mtu wa kumuuliza? Kuna majengo wakati huku yanajengwa ghorofa za juu, chini tayari yanfunguliwa maduka.Sheria zinasemaje. Sikusudii wale waliosita huku wakichuma nguvu mpya. Kuna majengo mabovu ambayo hugeuzwa majaa na maficho ya wahalifu, hapa tunafanya nini?

4. Vituo vya kuuzia mafuta pia ni majengo yenye hatari iliofunikwa shuka. Yanahifadhi petroli nyingi na yamezungunkwa na makaazi ya watu.Utayari na kujikinga na janga la moto ukoje? Kuna walinzi? Kama wapo wamewezesha kwa maana zake zote au ni watu wamekuja kuwapiga makofi mbu tu.Vifaa vyenye uwezo kuzima moto wa umeme na petroli vipo? Mashine za kukamulia mafuta zinafanyiwa servicing kila wakati au zinasubiriwa ziharike ndipo fundiaitwe? Sijui. Kuna mikapa ya kuzuia watu wengine wasifanye shughuli zao karibu na vituo kama vile mama mtilie, wauza kahawa, wateneza magari na vespa au au wako huru hata kuugeuza uwanja wa kituo kuwa ni eneo lao la biashara? Wanajibana hapo hapo.

SEHEMU YA TATU

1. Kutokana na michango nilopata kwa mada za nyuma ni wazi kuwa watu walio wengi hawana taaluma yoyote juu ya utayari wa kukabiliana na majanga ya moto. Sijui. Sijui kama kuna semina zozote zinafanywa kuwatanabahashisha juu ya majanga ya moto kwa viongozi wa ngazi na kada tafauti. Sijui. Sijui kama wanafunzi wamefikiwa na fununu zozote kuhusu majanga ya moto. Sjui kwenye shehia kama kuna kawaida ya kufikiwa na wahusika na kuzinduliwa juu ya majnga ya moto. Sijui. Sijui kama ukaguzi endelevu unafanya kwenye taasisi na zisizo rasmi zinafanyiwa . Sijuwi. Bado tunajidanganya kuwa moto si tatizo. Pia sijui.

2. Njia moja nzuri ya kupima utayari wetu wa kukabiliana na janga la moto ni ni lile kuvumisha moto bandia ( Mock Fire)
Wenzetu njia hii huitumia sana bila ya kujali gharama.lakini inalipa kwani huwapa nafasi ya kujitathmini na kufanya maboresho. Hapa petu sijaliona au labuda sijasikia kufanyika.

3. Mock Fire hufanywa kwenye viwanja vya ndege na hata vya watoto, hufanywa kwenye taasisi za serika na binafsi zikiwemo mashule na mwahala mwengine mwenye mikusanyiko ya watu. Hakuna aneambiwa kabla kuwa kuna zoezi litafanyika. Huwekwa wachunguzi kupima kila kasoro, mapungu na madhaifu ya kila chombo husika.

4 Hapo baragumu la zima moto linapolia wahusika huwa wanaagalia umakini wa mamlaka ya zimamoto utayari wao ni wa kiwango gani. Muda waliochukua kufika eneo la tokeo na magari yao yakiwa na majina vifaa vyengine. Urefu wa ngazi zao kufikia magorofani.Tunapojenga majumba marefu tuna vifaa na utaalamu ya kuzifikia magorofani? Huangaliwa uongozi nzima unavoratibu shughuliyenyewe na ujasiri wa wafanyakazi wa zima moto.

5. Watu wa afya nao hupimwa utayari wao. Ambulance zinafika kwenye tokeo wakati zikiwa na vifaa na huduma ya kwanza. Utayari wa madaktar na wauguzi pia hupimwa hapa. Uwepo wa madawa husika hutarajiwa yaonekane.

6. Kushindwa kwa magari ya zimamoto kwenye tokea ni kipimo cha utendaji watendaji wa mabararaza ya miji na ugawaji viwanja kwa kuruhusu ujenzi holela au kwa kutopima viwanja au urasimu na gharama kubwa kupata kiwanja hivo watu kujijengea ndivo sivo.

7. Hivo ni kwa ufupi. Bila ya mock fire ni shida kujua utayari wetu wa kukabiliana na janga la moto pindi ikitokea. Hatuwezi kusubiri mpaka moto utokee ndipo tuchakarike. Tuaatshindwa hata kujua vituo vya maji viko wapi , na kama vipo. Vipi vimejifukia au maji yamekatwa. Hivo nasubiri wachangiaji wanijibu suali langu, “Je ,kasi ya ujio wa majengo marefu inaendana na kasi ya utayariwetu wa kukabiliana na janga la moto?” Kwa sababu mie sijui.
MWISHO

FB

Share: