Makala/Tahariri

Katiba pendekezwa – Serikali ya Muungano itafanya itakalo Zanzibar

Othman Masoud,

+++JUKWAA la Katiba Tanzania (JUKWATA) lilifanya mkutano wake mkuu ambapo suala la hatima ya upatikanaji wa katiba mpya lilikuwa mjadala mkuu ukihusisha hoja zilizotolewa na wataalamu mbalimbali. Othman Masoud Othman, aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, aliwasilisha mada kuhusu Maslahi ya Zanzibar katika mchakato wa Katiba Mpya. Ifuatayo ni sehemu ya mada hiyo. Endelea…+++

ZANZIBAR na Tanzania Bara ziliingia katika mchakato wa Katiba inayopendekezwa zikiwa na faida kubwa ya nyaraka, kumbukumbu na uzoefu wa kero za msingi za kikatiba za Muungano. Baadhi ya nyaraka ziliingizwa katika Sheria ya Mapitio ya Katiba kama rejea za lazima za Tume ya Katiba, bila shaka kwa faida ya wananchi na hata wajumbe wa Bunge la Katiba. Wote walipaswa kutorudia kero na kasoro hizo.

Suala muhimu jee Katiba inayopendekezwa imeepuka kasoro/kero hizo za mfumo uliopo wa kikatiba ambao kwa kiasi kikubwa unakandamiza maslahi ya upande wa Zanzibar na kudhoofisha juhudi za jumla za taifa kujenga Muungano utaoendeshwa kwa maslahi ya pande mbili?

Yapo maeneo ya Katiba inayopendekezwa ninayoona ama yanazidisha au kurasimisha kero na kasoro za Muungano zinazokwaza maslahi ya Zanzibar na ambazo zimekuwa zikizungumzwa na kuwekewa kumbukumbu kwa nyaraka rasmi kwa zaidi ya miaka 50 ya Muungano.

a. Mamlaka ya Rais wa Muungano kuigawa Zanzibar katika Mikoa, Wilaya na sehemu nyengine [IBARA YA 2(2)]:

Katiba ya Zanzibar ya 1979 iliweka kifungu hicho kwa sababu ya mfumo wa Chama kushika hatamu. Katibu wa Mkoa wa Chama alikuwa pia ndiye Mkuu wa Mkoa. Hivyo Rais wa Zanzibar hakuwa na mamlaka peke yake kuunda Mkoa kwani akiunda Mkoa wa kiserikali anaunda Mkoa wa kichama. Hata hivyo, mfumo huo ulipoondolewa Katiba ya Zanzibar ya 1979 ilifanyiwa marekebisho kupitia Sheria Na. 9 ya 1982 ambayo ilirejesha mamlaka ya kuigawa Zanzibar katika Mikoa, Wilaya na Sehemu mikononi mwa Rais wa Zanzibar.

Athari zake: Maswali

 • Rais wa Muungano katika kuigawa Zanzibar katika Mikoa, Wilaya na Sehemu atafuata Sheria ipi, ya Zanzibar au ya Muungano itayotungwa kwa mujibu wa ibara ya 2(3) ya Katiba inayopendekezwa?
 • Rais wa Muungano anauwezo chini ya ibara hiyo ya Katiba inayopendekezwa kuunganisha mikoa mitano na kuufanya mmoja;
 • Rais wa Muungano anauwezo wa kuigawa Zanzibar katika Wilaya, na kwa mamlaka hayo anauwezo wa kuufanya Mkoa kuwa Wilaya?
 • Rais wa Muungano anauwezo wa kuigawa Zanzibar katika Shehia? na jee anauwezo wa kuifanya Wilaya kuwa Shehia?
 • Kuna kifungu chochote katika kinachomlazimisha Rais wa Muungano kuzingatia Sheria za Zanzibar za Tawala za Mikoa? Kuzingatia ushauri wa Rais wa Zanzibar au kuzingatia maslahi ya Zanzibar katika kuigawa Zanzibar katika Mikoa na sehemu; [angalia Katiba ya Marekani inazuia States kuunganishwa kuwa State moja au kugawanywa kuwa State zaidi ya moja]
 • Kuna kifungu chochote kinachomzuia Rais wa Muungano asiifanye Zanzibar kuwa Mkoa mmoja, Wilaya moja au Shehia moja?
 • Zanzibar ina haki gani na kwa utaratibu gani wa kikatiba kupinga mgao wa Mikoa, Wilaya na sehemu ataofanywa na Rais wa Muungano inapokuwa haikuridhika

b. Ukuu wa Katiba Ibara ya 9 zingatia ibara ya 166 [2]:

“[9(1) Katiba hii ni sheria kuu katika Jamhuri ya Muungano kwa mujibu wa masharti yaliyowekwa na Katiba hii..”

Katiba inayopendekezwa ibara ya 1(3) inaeleza Hati ya Muungano ndio msingi mkuu wa Jamhuri ya Muungano. Ibara 74(3) inaeleza kuwepo mambo ya Muungano na yasiyo ya Muungano. Ibara 75 inaeleza Serikali ya Muungano itakuwa na mamlaka ya kusimamia mambo ya Muungano tu kwa Jamhuri ya Muungano na mambo yasiyo ya Muungano ya Tanzania Bara, na Serikali ya Zanzibar itakuwa na uwezo wa kusimamia mambo yasiyo ya Muungano kwa Zanzibar. Ibara 133 inaeleza mamlaka ya Bunge kutunga sheria. Ibara 166 inaeleza mamlaka ya Baraza la Wawakilishi kutunga sheria kwa mambo yote yasiyo ya Muungano kwa Zanzibar.

Katiba inayopendekezwa itasimamia mambo ya Muungano na yasiyo ya Muungano kwa Tanzania Bara, na Katiba ya Zanzibar itasimamia mambo yasiyo ya Muungano kwa Zanzibar.

Ni dhahiri kuwa Katiba ya Muungano itatumika Zanzibar kwa mambo ya Muungano, na kwa mambo yasiyo ya Muungano Katiba ya Zanzibar ndiyo itayotumika

Athari: Maswali

 • Katiba ya Zanzibar nayo ni Sheria sawa na Sheria nyengine kwa madhumuni ya ibara ya 9(2) ya Katiba inayopendekezwa; Katiba ya Zanzibar haiwezi kuwa Sheria sawa na Sheria nyengine kwa vile haikutungwa na Mamlaka ya kutunga Sheria bali imetungwa na Wananchi kupitia constituent assembly]
 • Jee Katiba inayopendekezwa ikipita, Kif. 2A cha Katiba ya Zanzibar kitahitaji kurekebishwa au kitabatilika wenyewe kwa kufuata masharti ya ibara ya 9(2)
 • Ibara ya 9(4) inaeleza kuwa sheria, mila na desturi lazima zifuate Katiba hiyo [inayopendekezwa]. Jee sheria ni pamoja na Sheria za Kiislamu na jee matumizi ya sheria za Kiislamu ni suala la Muungano?
 • Mila na desturi za Zanzibar ambayo ndiyo sehemu ya utamaduni wa Zanzibar zinafungwa na ibara 9(4)? Kama ni hivyo mila na desturi za Zanzibar zitaendelea kuwa salama iwapo zitapingana na Katiba inayopendekezwa? (kwa mujibu wa utaratibu mamlaka ya kutoa tafsiri sahihi ya Katiba yamo mikononi mwa Mahkama na sio Dola (Serikali/Utawala) wala viongozi)
 • Kama Katiba inayopendekezwa ndiyo kuu kwa mambo yote kutakuwa na haja ya kuwa na Katiba ya Zanzibar na kama itakuwepo itakuwa na nguvu ya kikatiba au sheria sawa na sheria nyengine?

c. Mfumo wa Serikali Mbili [ibara ya 73]:

Ibara 73 imeweka bayana mfumo huo. Ibara 75 imeweka bayana zaidi kuwa Serikali ya Muungano itasimamia mambo yote ya Muungano kwa Jamhuri ya Muungano yote na mambo yasiyo ya Muungano kwa Tanzania Bara.

 • Ibara 112 inaeleza kuwa mamlaka ya kuamua kuhusu sera zote ni ya Serikali ya Muungano.
 • Ibara 114 inayohusu muundo wa Baraza la Mawaziri, ukiachia Rais wa Zanzibar hailazimishi kuwe na Waziri kutoka Zanzibar katika Baraza hilo.
 • Katika uteuzi wa Waziri Mkuu chini ya ibara 110 haulazimishi kushauriana na Rais wa Zanzibar.
 • Katika uteuzi wa Mawaziri chini ya ibara 115 Rais wa Muungano anashauriana na Makamu wa Kwanza na Waziri Mkuu lakini Rais wa Zanzibar ambaye ni Makamu wa Pili hahusiki katika uteuzi.
 • Hakuna ibara inayoweka utaratibu wa namna ya kuihusisha, kuishauri au kuishirikisha Zanzibar katika kufanya maamuzi yoyote yanayohusu masuala ya Muungano
 • Hakuna mfumo maalum wa kuunda Wizara za Muungano
 • Hakuna bajeti wala mapato yaliyoainishwa kwa mambo yasiyo ya Muungano, na hakuna mfumo wa matumizi unaopaswa kutenganisha baina ya mapato na matumizi ya Muungano na mambo yasiyo ya Muungano
 • Hakuna mfumo wa kikatiba unaoipa haki Zanzibar ya kupinga maamuzi ya kisera yatayofanywa na Serikali ya Muungano, yaliyo kinyume na maslahi ya Zanzibar
 • Hakuna mfumo wa kikatiba unaoibana Serikali ya Muungano kufanya maamuzi yoyote yale kwa faida ya upande mmoja hata bila kuishirikisha Zanzibar na bila ya ridhaa ya Zanzibar

Matokeo ya jumla ya upungufu huo ni kuwa Serikali ya Muungano iliyoundwa bila ya kuishirikisha Zanzibar inauwezo wa kufanya maamuzi ya kisera/kiutawala pasina ridhaa ya Zanzibar. Serikali ya Muungano inaweza kutumia rasilimali za Muungano kwa faida ya upande mmoja pasina ridhaa wala kuishirikisha Zanzibar. Kwa ufupi, Serikali ya Muungano ina mamlaka ya kufanya lolote inalopenda.

Shukrani za dhati ziende Mwandishi wa Mwanahalisi na Mawio Jabir Idrisa, na Othman Masoud kwa taaluma yake ya sheria.
Imehaririwa na MZALENDO.NET.

Tagsslider
Share: