Makala/Tahariri

Kinana Hajanena kitu Bado

Kama ulitegemea Kinana aje kufanya kampeni basi sahau. Kampeni maana yake kumwaga sera, kuwapa matumaini wananchi, kuonyesha rekodi ya utendaji na mafanikio ya chama, na kuvutia wananchi ili wakupe kura. Mwaka mmoja sasa tokea wawepo kote tena wenyewe pekee, Jee kuna mabadiliko ya kuyatangaza? Kuna Maendeleo? Si walituahidi Dubai, iko wapi? Mishahara kupanda jee? Lipi hasa la kujivunia?

Lazima akujenge khofu, akuvunje matumaini, aitusi na kuidharau imani yako kwa sababu hakuna adui mkubwa wa idhlali kama imani. Imani ndio iliopasua bahari Mussa (AS) akapita. Imani ndio ilioangusha himaya ya firauni, imani ndio iliomsukuma Mandela akatoka jela na kuongoza nchi kwa wema na ihsan, imani ndio iliomsukuma Dr King akawaambia wanyonge kuwa ana ndoto ya mabadiliko. Hivi kuna aliejuwa kuwa tutashinda mpaka wakafuta uchaguzi? Tuliwezaje? Ni imani na kutokata tamaa, ni imani ya kujuwa unasimama na lenye haki, ni imani kutoka ndani ya moyo ya kusema mpaka kutapambazuka.

Mwaka mzima wako wenyewe kila pembe ya utawala na lipi hasa waliloweza kulibadili? Njaa imeondoka au hata ina matatajio ya kupungua? Maji na umeme? Kazi kwa vijana zimeongezeka? Uonevu umepungua? Vipi msimamo wa haki umeimarika? Vipi mwenendo wa nchi nzima wa giza totoro umeanza kunawirika? Afya na sera nzima ya tiba na kinga? Nenda kwenye elimu, hata vile vidiploma vya wanyonge nusura wavifute, watakwambia uchumi umekuwa waulize upi? Wa makaratasi ni sawa maana ni milki ya wachache si kwa walio wengi, uchumi kwa wananchi jee? Kilimo kinasuasua, mifugo haina mbele wala nyuma, uvuvi wa kubahatisha yaani tupo tu kienyeji enyeji. Unafikiri Kinana atakuja na ndoto ya neema au giza la kebehi, dhihaka na uchochezi tuzidi kuhasimiana?

Kambeba Polepole aje atwambie nini wazanzibari hasa tumfahamu? Kwamba sheria na katiba ikae pembeni tutumie hekima baada ya kushindwa uchaguzi huru na haki? Hebu hasa waseme lipi la kujivunia zaidi ya kufuta chaguzi kwa ubabe maana unapoona serikali nzima inaomba hata pesa ya fulana na kofi mia tano kweli itaweza kukuletea mabadiliko yenye manufaa na maisha yako?

Wanalolijuwa katika kampeni ni matusi, dhihaka na kejeli. Katika utawala wanalolifahamu no uonevu na khilaki za ubaguzi, yaani tuna serikali ya sherehe na vifijo, watoto wa masikini watabaki kuwa wabahatishaji katika mlo, mavazi na hata pa kulalia. Umetembea shule za mashamba, ng’ambu na mjini ukawaona watoto wanavyosota? Si kwa mavazi, si kwa elimu inayotolewa wala si kwa ndoto ya elimu kuwafungua. Mtoto hana viatu, kakaa chini, katandika kipolo ili asichafuke na vumbi la sakafu iliojaa mashimo. Hii ndio “future” wanayojengewa vizazi vyetu ili viwe tegemezi maishani mwao, kujenga mabadiliko kuna hitaji nia thabit na ridhaa ya wananchi. Tunaendeshwa kibahati nasibu, mnyonge na kizazi chake awe mtumikaji tu na mbusu pete ya mtawala.

Unakwenda mashamba mahotelini wanakuuliza kwenu wapi unawajibu hapa hapa Zanzibar. Mgeni anaanza kwa kukuhadithia alioyakuta njiani kutoka uwanja wa ndege mpaka Nungwi. Hatarajii kabisa kuuona umasikini wa kupindukia, unainamisha chini kichwa huna la kumjibu. Halafu linakuja jitu lililojaa tuhuma za ubadhirifu, wizi wa wanyama pori na matumizi mabaya ya pesa za chama linakwambia mshindi ni king’ang’anizi wa madaraka na yule alieshindwa si uchaguzi tu akaufuta bali hata uongozi ndie “hero” wa kupigiwa makofi. Nasi pwa pwa pwa tukazanishe kumpigia makofi. Unarudi nyumbani hujui unaamkaje kesho yake, maisha yako mazima yamejengwa kiutegemezi na kubusu pete ya mfalme mpya. Na iwe maisha ya kwako umeshayasukuma unapotaka mwenyewe basi huna ndoto basi za kizazi chako kuwa huru, kinachojitegemea na kinachosimama kwa miguu na mikono yake mwenyewe? Hivi haikupitikii kuwa kama ni mwananchi una haki ya kuishi kwa matarajio badala ya utegemezi?

Mwaka mzima sasa kuna mabadiliko katika kilimo ili kiweze kutoa ajira za kujitegemea kwa wahitimu wetu wa kidatu cha pili na nne? Hivi kuna msukumo wa ajira kwa vijana wanaosukuma siku mabarazani? Ni aibu kubwa kwamba ndoto kubwa za vijana wengi ni kuzifananisha na mafanikio ya bongo flavor, mpira na uuzaji wa madawa. Hebu tuwe wakweli nini hasa dhima ya uongozi? Halafu linakuja jitu kuchochea mfarakano zaidi ati ndio kampeni. Unajuwa kule upande wa pili husema nini anapotembelea? Huwaita mawaziri wa chama chake mwenyewe mzigo, huku kwetu thubutu, tumegeuzwa wajinga wa kufuata upepo, kupulizwa katika ubaguzi na uhizibu katika karne hii ya leo. Umepata kuwaona wanapowapokea hao mahizibu wanapokwenda kuomba msaada? Lasi na baragashia huwa juu na huwaita “watukufu” huku kwetu ndio humwaga petroli ya visasi visivyokuwapo.

Hakuna kukata tamaa mpaka safari tufike, tujenge tamaduni ya demokrasia kiasi kwamba “loyalty” ya chama isiwe ndio kigezo cha kukipigia kura bali sera ndio ikusukume wapi pa kuelekea. Unapiga kura ukijuwa anaekuja atajenga msingi unaokubalika wa maisha kwa kila mwananchi na umasikini hasa usifikie kiwango cha walio wengi kuishi kwa kibahatisha katika mavazi, malazi na makaazi. Elimu isiwe ya kubahatisha kwa wanyonge bali ndio dira na ndoto ya mafanikio si ya wananchi pekee bali ya maendeleo mapana ya nchi, na sera nzima ya afya ijenge matumaini kwa watumiaji wote badala ya sukuma siku kwa matabibu na wanaotibiwa.

Hakuna kukata tamaa mpaka siku ardhi yetu tukufu tuliojaaliwa na Mwenyezi Mungu itaposimama juu kwa insaf, uadilifu na haki kwa kila anaeikanyaga bila ya kujali aila yake, rangi yake au nasab yake. Tutafika kwa imani, ujasiri na kutokata tamaa kwetu tena bila ya kumwaga damu ya yoyote kwa msukumo wa maslahi ya kunguru mroho asieshiba kwa miaka hamsini ya vita ya panzi.

Tagsslide
Share: