Makala/Tahariri

Kutozungumzia Muungano ni kosa kubwa zaidi la mchakato wa Katiba

GARIMOSHI la Katiba mpya linaendelea kwenda kasi na hakuna dalili ya kukoma mpaka Katiba “mpya” itakapopatikana.

Msisitizo hadi sasa umekuwa juu ya ujio wa “Katiba mpya” hata kama upya wake utakuwa bado na mambo ya zamani. Mchakato huu ambao ulikosewa toka mwanzo una kila dalili ya kufanya zoezi la Katiba mpya kutofanikiwa na kutokukidhi mahitaji ya Watanzania.

Sheria inayosimamia mchakato huu na ambayo iliweka uwezekano wa tume ya Katiba kuundwa imeweka wazi mambo kadhaa ambayo wananchi (yaani wenye nchi) hawapaswi kuyazungumzia na kuyabadilisha isipokuwa tu kujadili kwa namna ya kuboresha. Yaani, wananchi (wenye nchi) wakitaka kuondoa jambo fulani kati ya haya, sheria inakataza.

Kifungu cha 9 cha Sheria hiyo ya 2011 kifungu kidogo cha 2 kimeweka orodha ya mambo ambayo ni lazima yadumishwe kwenye Katiba mpya na la kwanza kati ya hayo ni “kuwapo kwa Jamhuri ya Muungano”.

Jambo hili kwa haraka laweza kuonekana kuwa ni jema, lakini tukiangalia kwa karibu tutaona kuwa kwa maamuzi ya watu walioko madarakani mojawapo ya matatizo makubwa kabisa ya kisiasa ambalo Taifa linahangaika nalo ni hili – uwepo wa Jamhuri ya Muungano.

Ikumbukwe kuwa tulipoungana na kuunda taifa la Tanzania tulikuwa nchi mbili kila moja ikiwa na hakimiya kamili. Kulikuwa na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na kulikuwa na Jamhuri ya Tanganyika. Nchi hizi mbili ziliungana na kuunda nchi hii ya Tanzania. Tangu wakati huo hadi sasa hata hivyo Muungano wetu umekuwa sababu ya fahari lakini pia sababu ya maswali.

Miaka ya karibuni maswali haya yameanza kugeuka na kuwa shari baina ya watu wa pande zetu mbili. Kuna mgogoro ambao tayari umehusisha viongozi wa kitaifa. Wapo wananchi wa Zanzibar ambao wanaamini kuwa pamoja na kuingia katika Muungano, Zanzibar ilibakia kuwa nchi na imeendelea kuwa nchi. Hawa wanachodai ni kuwa kilichopotea baada ya Muungano ni serikali ya Tanganyika lakini Zanzibar imeendelea kuwapo.

Matokeo yake ni kuwa Wazanzibari wameendelea kushikilia Zanzibar lakini wakati huo huo wanadai Tanzania. Wazanzibar wana haki zote kama Wazanzibari na wana haki zote kama Watanzania. Wazanzibar wanaweza kuteuliwa katika ajira Zanzibar na wanaweza kuteuliwa katika ajira Bara; wanaweza kuomba kazi Zanzibar wanaweza kuomba kazi Bara; wanaweza kumiliki ardhi Zanzibar na wanaweza kumiliki ardhi Bara. Wazanzibar wakija Bara kwamba wanatoka Zanzibar haichukuliwi kwa namna yoyote tofauti.

Hivyo, Mzanzibari anaweza kwenda Bukoba, Iringa, Mwanza au Tanga na kufanya shughuli zake akijua yuko ndani ya nchi yake. Lakini pamoja na hayo bado ana haki ya kipekee Zanzibar.

Mtu wa Bara (Mtanzania anayetoka Bara) akienda Zanzibar hana haki zile zile isipokuwa kama vile ni mgeni (alien). Hana haki ya ajira au kuteuliwa kwenye nafasi mbalimbali. Rais wa Zanzibar hawezi kumteua mtu wa Bara kufanya kazi za Zanzibar bila kuonekana ameenda ‘nje’ ya Zanzibar kutafuta ajira japo Mzanzibari naye ni Mtanzania na mtu wa Bara naye ni Mtanzania. Mtu wa Bara ni Mtanzania akiwa Tanzania lakini akiwa Zanzibar yeye ni mBara kwani Zanzibar ni ya Wazanzibari lakini Tanzania ni yetu sote.

Mtu wa Bara kwa Zanzibar yeye ni mgeni. Na tumeshuhudia baadhi ya Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wakijaribu kutunga sheria zenye kuwashughulikia watu wa Bara kama wageni Zanzibar ndani ya Muungano huu huu.

Inaonekana walioungana ni watu wa Bara lakini watu wa Zanzibar wao bado hawajaungana. Wanataka chetu kiwe cha wote lakini cha kwao kiwe cha kwao. Kisingizio (haiwezi kuwa sababu) ni kuwa ati “Zanzibar ni ndogo”.

Hivyo, kutokana na udogo wake basi ni lazima kuwe na nafasi za kuwalinda Wazanzibari. Hivyo ardhi ni kwa ajili ya Wazanzibar na ajira mbalimmbali ni kwa ajili ya Wazanzibari. Ni sawasawa na kule Marekani ati mtu wa California akienda Michigan aonekane ni mgeni na asiwe na haki hizo japo na yeye ni Mmarekani.

Katika mfumo huu ambao tunaambiwa una kero nyingi mara nyingi kinachoitwa “kero” ni kile ambacho Muungano unaathiri Zanzibar. Lakini maoni yangu ni kuwa kama kuna kero kubwa ya kimfumo ni ile ambayo inawabagua watu wa Bara wanapoenda Zanzibar au wanapotaka kuishi na wao kunufaika na Zanzibar kama sehemu ya nchi yao. Wakati Bara mtu anaweza kutoka Kigoma na kwenda Arusha au kutoka Mwanza kwenda Tabora kujaribu maisha na asipate shida yoyote ya kuonekana mgeni alimradi yeye ni Mtanzania mtu huyo huyo akienda Zanzibar ataonekana mgeni na hatopewa ule ulinzi wa kisheria ambao yeye kama Mtanzania anao katika nchi yake.

Mtu wa Bara anapoenda Zanzibar ni kana kwamba anakwenda nchi nyingine lakini Mzanzibari akija Bara anaenda sehemu ya nchi yake.

Hivyo, swali ambalo huwa watu wanauliza kwanini Wazanzibari wanapewa ajira kwenye wizara zisizo za Muungano lina makosa kwa kiasi chake. Lina makosa kwa sababu Mzanzibari ana haki zote kama Mtanzania lakini si kila Mtanzania ana haki sawa Zanzibar – japo nayo ni Tanzania.

Mzanzibari anapoomba nafasi kwenye chuo kikuu chochote Bara anafanya hivyo kama Mtanzania na nina uhakika Bodi ya Mikopo inatoa mikopo kwa Wazanzibari vilevile – kwa sababu na wao ni Watanzania. Mzanzibari anaweza kuomba kazi kwenye idara au vitengo vya Bara ambavyo si vya Muungano na akapewa ajira hiyo – si kama mgeni (kwa mfano Mkenya au Mganda) bali akapewa nafasi kama Mtanzania kwani hiyo ni haki yake.

Lakini mtu wa Bara hawezi kuomba ajira kwenye idara au kitengo Zanzibar akachukuliwa kama Mtanzania tu; itapaswa ajibu swali kama yeye ni Mzanzibari. Kwani Wazanzibari wana urithi Zanzibar na wana urithi Bara.

Ni katika hili tunaweza kuona kuwa kutozungumzia uwepo wa Jamhuri ya Muungano ni kosa kubwa. Kama Wazanzibari wanataka kuendelea kuwa na nchi yao na ambayo watoto wao watairithi basi wapewe nafasi hiyo. Watu wa Bara nao wapewe nafasi ya kufurahia urithi wao bila watu “wengine” kupewa urithi wasioutaka. Kosa hili la kutokuzungumzia “uwepo wa Muungano” ni kosa ambalo bado litaendelea kutuandama kama jinamizi.

Watu wa Bara nao wataanza kuchoka kuona nafasi “zao” zinachukuliwa na Wazanzibari wakati wao hawawezi kuchukua nafasi kule Zanzibar bila ya kuonekana wanachukua nafasi za “Wazanzibari”.

Hivyo, japo ni kweli wanaweza kutuletea Katiba mpya, hali halisi ni kuwa bado tutakuwa na tatizo lile lile la zamani; Muungano. Hata tukiwa na serikali tatu bado matatizo yatakuwa yale yale.

Je, Wazanzibari watakuwa na haki zozote Tanganyika? Je, Watanganyika watakuwa na haki zozote Zanzibar? Kosa hili litakuja kutugeuka mbele ya safari na kutuumiza kama Taifa. Tufikirie.

Raia Mwema

Share: