Makala/Tahariri

Oman ndiko Kwenye Mapinduzi ya kweli, Zanzibar ni BT na Hasad!

Karibu Zanzibar kwaheri Oman: By Muhammad Yussuf
3 April at 12:36 ·

Dear Friends,
Kama nilivyowaarifu wanachama wa ZIRPP na marafiki zangu wote, nilifanya ziara ya mapumziko nchini Oman kuanzia tarehe 24 Februari 2017 hadi tarehe 15 Machi 2017. Kwa hivyo, napenda kutumia fursa hii kutoa shukrani zangu za dhati kabisa kwa mapokezi mazuri niliyoyapata kutoka kwa wenyeji wangu, na hasa zaidi kutoka kwa Bwana Abdulla Amor Ali Ameir Al Marhuby na mke wake, Freya Khamis Abdulla Ameir Al Hinai, kwa ukarimu wao wa kupigiwa mfano na kwa kunitembeza katika sehemu mbali mbali za Oman ikiwa ni pamoja na Muscat na katika miji na vijiji mbali mbali nje ya Muscat na sehemu za kihistoria.

Kusema kweli nimeshapokewa na wengi lakini sijapata kuona kiwango na aina ya mapokezi na takrima niliyoipata kutoka kwa Abdulla Amor na mke wake Freya. Kwa muda wote niliokuwa nao (tokea siku ya kuwasili kwangu nchini Oman hadi kuondoka), nilijisikia niko zaidi ya nyumbani. Nyuso na bashasha zao zitabaki ndani ya moyo wangu daima milele. Namuomba Allah azidi kuwapa moyo wa upendo na ukarimu, afya njema, neema na maisha marefu – Ameen.
Vilevile, shukrani zangu zimwendee shemegi yangu, Mohammed Abdulla Ameir Al Hinai (Eddie) na mke wake Shariffa, kwa kunipokea kwa mikono miwili na kuniandalia hafla maalum iliyoniwezesha kukutana, kula na kunywa pamoja na watoto na wajukuu zake.

Pia napenda kuwashukuru ndugu na rafiki zangu wa siku nyingi, kama vile Prof. Ibrahim Noor, Prof. Harith Ghassany, Mohammed Amor Ali Ameir na mkewe Zeinab Burhan Mkelle; Sheikh Ali Amour Ali Ameir na mke wake, Bi Maimuna; Sheikh Abdulla Al Harthy; Abdulla Saleh Mbamba na mke wake, Saida; Ghalib Salum, Madni na Safaa kwa kunikaribisha majumbani mwao na kuniandalia chakula, iwe cha mchana au usiku, na kwa kunitembeza sehemu mbali za Muscat, Oman.
Ikiwa ni ziara yangu ya kwanza kabisa katika nchi ya Oman, kwa hivyo, lazima nikiri kuwa sikuwa nikiijua vizuri Oman kabla ya ziara yangu hiyo. Niliijua kupitia maandishi, picha na kwa kusoma historia yake kama ilivyoandikwa na waandishi mbali mbali kuhusu mahusiano yake na Zanzibar na maingiliano ya siku nyingi baina ya watu wake. Kwa hivyo, ziara yangu hii imenipa fursa ya kuiona na kuijua Oman kama ilivyo kupitia macho yangu mwenyewe na kupitia mazungumzo na simulizi za ana kwa ana na wenyeji na marafiki zangu hao.

Tokea siku ya kwanza ya kuwasili kwangu nchini Oman, ratiba ya matembezi yangu ilipangwa na kutekelezwa kwa ufanisi wa hali ya juu na wenyeji wangu, rafiki yangu mpenzi wa siku nyingi, Abdulla Amor Ali Ameir Al Marhuby, na mke wake mpenzi, Freya Khamis Abdulla Ameir Al Hinai, ambaye ni mtoto wa shemegi yangu, Khamis Abdulla Ameir Al Hinai, kaka wa mke wangu, Zakia. Watu wawili hawa ndio walionitembeza sehemu mbali mbali nchini Oman, na ndio walionipangia ratiba ya kuonana na kutembelea ndugu, jamaa na marafiki zangu popote pale walipokuwa katika makaazi yao. Wengi wao niliwatembelea majumbani mwao kuitika mialiko yao ya chakula cha mchana au usiku, na wengine walinifuata nilipofikia kwa mazungumzo mafupi ya kujuuliana hali baada ya kutoonana kwa miaka mingi.
Kwa hivyo, kuanzia tarehe 25 February 2017 hadi tarehe 14 Machi 2017, siku moja kabla ya kuondoka kwa safari ya kurejea Zanzibar, Abdulla na Freya walihakikisha kuwa sitoondoka Oman kabla ya kutembelea sehemu muhimu mbali mbali na za kihistoria ili niweze kujionea kwa jicho langu mwenyewe jinsi Oman ilivyo na hasa zaidi kuhusiana na kiwango cha maendeleo yaliyopatikana katika nyanja za elimu, afya, miuondombinu ya barabara/usafiri, utamaduni na kadhalika katika miaka 40 iliyopita.

Kwa muktadha huo, siku za mwanzo za ziara yangu, Abdulla na Freya walinitembeza sehemu mbali mbali za mji wa Muscat; kama vile Muscat City Center Mall, Al Bustan Palace, Sultan’s Old Palace, Muscat International Book Fair (ambako nilinunua vitabu vitatu). Tarehe 28 February 2017 na tarehe 1 Machi 2017, Prof. Ibrahim Noor alinitembeza Sultan Qaboos University ambako nilitembelea Kitivo cha Sayansi na Teknologia na katika Idara ya Elimu ya Sanaa na kula chakula cha mchana katika mkahawa wa Chuo Kikuu hicho baada ya matembezi hayo. Pia nilipata fursa ya kutembelea The National Museum iliyopo Muscat, ambamo historia ya Masultani wote waliotawala Zanzibar, kuanzia Seyyid Said bin Sultan mpaka Seyyid Jamshid bin Abdulla, inazungumziwa; na Sultan Qaboos Grand Mosque uliopo mjini Muscat.

Siku zilizofuatia, Abdulla na Freya walitutembeza, mimi na mke wangu, nje kidogo ya mji wa Muscat; kama vile Nizwa Market, Misfah Old House, Hawiyat Najm au kama inavyojuulikana zaidi ‘Dabab Sinkhole’, kule Ad Dakhiliya. Pia tulitembelea mji wa Sur wenye historia ndefu na Zanzibar ambako ndiko walikotokea wahamiaji wengi wa Kiomani na kuingia Zanzibar ambako walijuulikana kama Wasuri; na nyumba ya Marehemu Maalim Amor Ali Ameir Al Marhuby iliyopo katika kijiji cha Ibra, alipozaliwa baba yake na umuhimu wake kwa watoto na wajukuu zake.
Mohammed Amor Ali Ameir naye hakuabaki nyuma; akiwa dereva makini aliyeshiriki katika resi za magari, alichagua kututembeza katika Wilaya ya Ad Dakhaliya hadi kutufikisha katika pango maarufu lijuulikanalo kwa jina la Al Hoota Cave lililo mita 65 juu ya mlango wa kuingilia. Matembezi ndani ya pango hilo ni ya masafa ya mita 850 na yanachukuwa muda wa dakika 45 kuyamaliza; na kuna jumla ya ngazi 230 za kupanda hadi kufikia kileleni.

Kama hili halikutosha, baada ya chakula cha machana katika Ayadina Restaurant, Mohammed alituendesha hadi kileleni cha Al Jabal Akhdhar. Juu huko tulijoinea mji mkubwa uliojengwa na kujengeka na wenye kujitegemea kwa kila kitu. Hapana shaka yoyote ile kuwa teknologia iliyotumika katika kupitisha barabara pana ya njia mbili (kwenda na kurudi) katika kulichonga jabali hilo hata likaweza kupitika na uenezaji wa mataa yenye kumurika barabara hiyo, ni ya hali ya juu na iliyoigharimu serikali ya Oman mabilioni ya fedha.
Kuhudhuria Maziko

Siku ya Ijumaa tarehe 10 Machi 2017, mimi na mwenyeji wangu, Abdulla Amor, tulihudhuria maziko ya Marehemu Maalim Said Ali Al Suleiman katika viwanja vya Makaburi ya Masjid Bilal, mjini Muscat. Marehemu alikuwa mwenyeji wa Pemba na ambaye alisomesha katika skuli mbali mbali kisiwani humo, ikiwa ni pamoja na Skuli ya Michakaeni, kabla ya kuhamia Oman. Zaidi ya watu 500 walihudhuria mazishi yake yaliyofanyika mnamo saa tatu za usiku baada ya Salaa ya Ishaa.
Lakini, siku ya Jumamosi tarehe 11 Machi 2017, katika viwanja hivyo hivyo vya Makaburi ya Masjid Bilal, ndipo niliposhuhudia umati mkubwa sana wa watu uliohudhuria mazishi ya Marehemu Mohammed Ali Muhsin Barwany, mtoto wa Marehemu Ali Muhsin Barwany, aliyekuwa kiongozi wa Zanzibar Nationalist Party (ZNP) yaliyofanyika mnamo saa 4.00 za asubuhi. Wengi wa waliohudhuria mazishi hayo walikuwa ni Wazanzibari wahamiaji. Baadhi yao nilikuwa nikijuana nao kabla tokea miaka ya nyuma, lakini wengine sikuwafahamu isipokuwa baadhi yao walinifahamu kupitia mitandao ya kijamii.

Kwa mujibu wa mwenyeji wangu, wengi wa Wazanzibari wahamiaji hawa walikuwa ni wastaafu katika utumishi wa serikali ya Oman na taasisi zake mbali mbali; baadhi yao walikuwa madaktari, wachumi, washika fedha, ma-injinia, marubani wa ndege, wanasheria, walimu, maprofesa, na wengine walikuwa wafanya kazi wa kawaida. Kwa kweli, nilikuwa natafakari na kujiuliza mwenyewe kwa mwenyewe jinsi Zanzibar ilivyoipoteza nguvu kazi hii muhimu katika maendeleo ya nchi.
Makala yangu rasmi yenye kichwa cha maneno: “Kwaheri Zanzibar: Karibu Oman” kuhusu ziara yangu nchini Oman ambayo, pamoja na mambo mengine, itazungumzia michango muhimu iliyotolewa na Wazanzibari wahamiaji katika maendeleo ya Oman; na hasa zaidi mchango muhimu na mkubwa uliotolewa na Maalim Amor Ali Ameir al Marhuby katika nyanja ya elimu na katika mchakato mzima wa uanzishwaji wa Chuo Kikuu cha kwanza cha Sultan Qaboos, yaani SQU nchini Oman. Kwa kweli, kuihama Zanzibar kwa Maalim Amor pamoja na Wazanzibari wengine kumeiondolea Zanzibar nguvu kazi muhimu katika maendeleo ya nchi ya Zanzibar. Lakini, kwa upande mwengine Oman ndiyo iliyofaidika kwa kuitumia nguvu kazi hiyo muhimu kikamilifu hadi kufikia maendeleo makubwa yaliyopatikana leo.

Katika jitihada za kuifahamu Oman vilivyo, mahusiano na maingiliano baina ya Oman na Zanzibar, na hali ya baadaye ya mahusiano baina ya wananchi wa nchi mbili hizi, msiwache kuusoma waraka huo wa kurasa 20 na ushei utakapotoka hivi karibuni. Picha zifuatazo zinaonesha Wazanzibari niliokutana nao, sehemu nilizotembelea ikiwa ni pamoja na SQU, the Grand Mosque, na sehemu nyingine za kihistoria. Pia kuna picha zinamuonesha Maalim Amor Ali Ameir wakati alipokuwa Zanzibar na Oman baada ya kuihama nchi aliyozaliwa, kukulia na aliyosomea. Allah ailaze roho yake mahala pema Peponi – Ameen.
Kwaheri Zanzibar: Karibu Oman.

Share: