Makala/Tahariri

MATOKEO YA MTIHANI ZANZIBAR YANAPOFANANA NA WAZIRI SHAMUHUNA

Wakati Zanzibar ikijiandaa kujipapatua na makucha na uonevu wa baraza la mitihani la Taifa Tanzania (NECTA), dalili za utayari huo hazioneshi kutosha au kufikia kiwango kinachotakiwa hapa kwetu. Hii ni mfano wa mtu anaejitayarisha kuanza maisha mapya ya kujitegemea au ya ndoa ilhali binafsi hajafanya matayarisho muhimu ya jambo hilo.

Nasema kuwa matayarisho yetu ya kujitegemea kuwa na Baraza huru, letu wenyewe la mitihani ni duni na hayajarekebishwa. Kuna dalili za wazi kwamba Elimu yetu na maamuzi makuu yahusuyo mustakabli wa Elimu kuwa hufanywa kwa misingi ile ile ya kisiasa za kibinafsi zaidi kuliko usiasa wa maendeleo ya kitaifa kwa ujumla.

Usiasa huu kwa kiwango kikubwa unachangiwa na mfumo uliopo. Mfumo ambao sehemu nyeti kabisa za nchi hii hukabidhiwa watu ama wasio na uwezo au wasio na nia njema ya kuwaletea watu maendeleo bila ya kuwabagua au kuwagawa.

Tunatambua kuwa Serikali yetu ipo katika sera ya umoja wa kitaifa, lakini moja kati ya mzaha mkubwa iliofanya katika uteuzi wa mawaziri ni katika Wizara ya Elimu. Tukubali kuwa Wizara ya Elimu ni moja ya Wizara nyeti kabisa katika nchi yetu, lakini kwa muda mrefu Wizara hii imekuwa ikifeli na kurudi nyuma kwa kasi ya ajabu.

Wizara yetu ya elimu imejaa ubinafsi na ubaguzi wa kivyama na umajimbo, achilia mbali uzembe na ufisadi uliokithiri. Katika hali kama hii uteuzi wa viongozi wakuu wa Wizara hii unahitaji watu wenye roho, moyo na imani ya kweli sambamba na uwezo wa kuongoza Wizara kama hii. Na hili linawezekana kwani tumeona nini Serikali imekifanya pale SUZA kwa kumuweka Profesa Rai kuondoa usiasa katika utendaji. Hili linawezekana pia kufanywa Wizara ya Elimu. SUZA Inang’ara sasa!

Sina shaka tunatambuwa kuwa uteuzi wa Waziri Harun Ali Suleiman ndio uliouwa kabisa uhai wa Wizara ya Elimu. Kwa Waziri Haroun, tulishuhudia uhaba wa walimu uliokifu na malalamiko makubwa ya walimu nchini. Bahati mbaya, kuondoka kwa Waziri Haroun akaja Ramdahan Abdala Shaaban, ikawa ni zaidi ya bure. Juzi tumeletewa Shamuhuna kuja kulifunika jeneza la Elimu ya watoto wetu hapa visiwani.

Uteuzi wa Shamuhuna wizara ya Elimu uliwaumiza wengi wanaomjua yeye kama yeye. Mheshimiwa ni mtu mwenye chuki ya asili dhidi ya Uunguja na Upemba. Pia ni bingwa wa kuanzisha migogoro na masuala yenye utata, kukoroga mambo na kufanya sanaa ya kila aina anapotaka kuharibu na kutimiza lake. Na hili ndio sasa limejitokeza katika matokeo ya mitihani, hasa ya kidato cha pili.

Matokeo ya kidato cha pili, ambayo ndio kweli muhimu kwa watoto wetu. Ni muhimu kwamba hapo huwa wengi wanaoshindwa kuendelea, huwa ndio mwsiho wa safari zao kimasomo. Matokeo ya kidato cha pili ya mwaka huu yana mshabaha mkubwa na Waziri Shamuhuna mwenyewe. Yaani yamefanana kwa sura na tabia alizonazo Waziri. Maana kama yeye angekuwa baba, na matokeo ya mwaka huu yakawa mwana, basi tungesema amejizaa, kopi kwa kopi! Hatuhitaji hata kipimo cha vinsaba(DNA)

Matokeo yetu mwaka huu yamefanana mno na Waziri kwanza, kwa kuonesha sura ya kuwa na upendeleo ambao unahitaji utafiti wa muda mrefu (Survey) ili uweze kututhibitishia kuwa ulikuwa wa haki na usawa. Na kama hauna upendeleo basi pia tutahitaji kujuwa kwanini jadweli ya matokeo yote imelalia upande mmoja tu wa nchi na kuacha kwengine? Tuanze na moja moja.

Mwaka huu wanafunzi bora wote watatu darasa la saba na kumi, wote wanatoka Unguja. Hii ni ajabu ya Karne. Tena istoshe, wote wanatoka mjini Magharibi. Hapa hoja hii inaleta mushkeli wa dhana yangu ya kwanza ya kutokuwepoo kwa usawa yaani upendeleo, au dhana yangu ya pili, ya kuwa hakuna usawa kwa sababu ya kutotowa huduma na usimamizi sawa wa huduma za Elimu nchini. Taswira hii ya ni ya ‘Kishamuhuna’(Shamuhunaism) zaidi. Maana tangu Mapuri hili halikuwepo!

La pili, kama ukiangalia kiwango cha ufaulu mwaka huu ni kibaya mno. Yaani katika watahiniwa 19,679, waliofaulu ni asilimia 56.9% tu yaani wanafunzi 11, 195, huku wengine 8,484 wakisubiri kudura ya mungu kujua hatma ya maisha yao. Hii ni hatari.

Katika nchi kama hii ambayo haina miundo mbinu mingi na huduma za kuendeleza vijana wake, idadi ya wanafunzi kama hawa wanaofeli kwa mwaka ni hasara kwa taifa. Lakini pia hili ni matokeo ya uteuzi unaoangalia maslahi ya wanasiasa na kivyama zaidi kuliko maendeleo ya utaifa.Na pia hapa sina shaka hili ndio hasa lengo ambalo lilipelekea Mheshimiwa Shamuhuna kuwekwa pale. Yaani kwa lugha nyepesi, tukikataa kukaangwa na NECTA, tujipike wenyewe hapa hapa kwetu.

Kama nilivyotarajia, usanii ni sehemu kubwa ya viongozi wetu wa kisiasa akiwemo waziri wetu wa Elimu. Kama utayaangalia matokeo yetu mwaka huu na maamuzi yaliyofanywa utaona wazi wzi kuwa kuna usanii au kuwafanya watu wapuuzi.Kwa mfano tunaambiwa kuwa matokeo ya mwaka huu yameongezeka kwa asilimia 0.8%. Hivi hili kweli ni jambo la kusema kweli hili? Hivi hili ni ongezeko gani, na kwa kipimo gani hasa ukichukulia idadi ya wanafunzi ya mwaka jana ilikuwa ndogo zaidi kuliko ya mwaka huu. Hii aslimia inatoka wapi na inamaanisha nini kitaalamu? Usanii.

Jengine, tunaambiwa kwamba wanafunzi wapato 1340 hawakufanya mtihani kwa sababu zisizojulikana. Nakubali kwamba katika hao kuna waliofariki, waliohama, wanaoumwa, na sababu nyenginezo lakini ni jukumu la serikali kufatilia kwanini vijana wote hawa hawakufanya mtihani? Pia baada ya kufanya hivyo walikuwa waeleze iwapo vijana hao watapewa tena fursa ya kufanya tena, jambo ambalo ni haki yao kisheria. Hili hatuambiwi. Kunani?
La ajabu mno, ambalo pia kwa Waziri shamhumuna halinishangazi kwani nalo anafanana nalo kabisa ni hili la maamuzi magumu aliyochukuwa kwa skuli alizozitaja kuwa ‘tiro’. Mheshimiwa amezitaja shule kama Bwefum, Umbuji, Uzi, Ubago, Pongwe pwani, Michamvi na mtende kwa Unguja kuwa madarasa yao yatafungwa. Kwa Pemba kisiwa panza, Makoongwe na Ndagoni pia madarasa yao yatafungiwa.

Suali langu linakuja hapa. Hivi shule ikifanya vibaya huwa kosa la shule hio pekee bila Wizara kuhusika? Isitoshe, kama shule hizo zimefanya vibaya hatuoni kama ni busara tungepitisha watendaji kuuliza kuna matatizo gani hadi yakajiri hayo? Au na hili si la busara? Kama hayo yote siyo, hivi kuzifungia shule hizi ndio tushatauwa tatizo la kufanya vibaya katika masomo na mitihani?

Maana mwaka huu tumefungia skuli nane, na mwakani 10. Hata akiondoka Shamuhuna itakuwa hakuna shule hata moja itakayobaki wazi. Na hapa ndipo tutakapokuja kusema kuwa Ilani ya chama ya uchaguzi ya mwaka 2010-2020 imefikiwa kwa ari zaidi, kasi zaidi na nguvu zaidi. Na bila shaka huku ndiko waziri Shamuhuna anakotupeleka!
Tungoje tuone!

Share: