Makala/Tahariri

Misumari ya mwisho katika jeneza la Zanzibar

  • Misumari ya mwisho inapigwa sasa na tanzania-bara katika jeneza la zanzibar. je.wazanzibar mpo ?

Na Laila Abdallah.

Ombi la Januari 18,2012 la Tanzania-bara (Tanganyika ) huko Umoja wa Mataifa,New York, kutanuliwa mipaka yake ya baharini ni misumari ya mwisho inayopigwa kufuatia ule wa kwanza katika JENEZA la Zanzibar hapo April 26,1964. Mara tu baada ya kuapishwa rasmi Mwalimu Nyerere kuwa rais Jamhuri ya Watu wa Tanganyika na Zanzibar,kanuni yake ya kwanza aliotunga (decree), ilikua kuifuta Tanganyika kwa njia za kiinimacho na kuibua Tanzania ambayo ni ile ile Tanganyika aliyoifuta lakini imeibuka na mipaka mipya ya aridhni.Ilijumuisha visiwa vya Zanzibar na Pemba. Sasa inajiandaa kupiga misumari ya mwisho kwa kutanua zaidi mipaka yake ya baharini na kiliomo ndani yake tangu dagaa hadi papa.

Tangu 1964, misumari mingi imekuwa ikigongomelewa jeneza letu tena hatua kwa hatua; na sisi wazanzibari twatazama macho tu.
Kufuatia Muungano uliofanyika bila umma kuulizwa ndewe wala sikio, akiba kubwa ya fedha za Zanzibar katika Bodi ya ile iliokua Jumuiya ya AFRIKA MASHARIKI ziliporwa na Mshirika wetu wa Muungano na kuzitia kibindoni katika Bank yake (BOT) bila ya ridhaa ama ya Mzee Karume au ya serikali yake. Shabaha ilikua ni kuiua Zanzibar kiuchumi ili kuidhibiti. Sehemu ya Zanzibar katika “Currency Board ” ya Jumuiya ile ilikua 11.2%. Huo ukawa msumari mwengine kati ya mingi katika jeneza letu. Licha ya juhudi nyingi za Viongozi wetu walishindwa kuzuwia hilo. Kwani wenzetu hizo wanazoziita “KERO” ndio “MISUMARI” wanayoigongomelea JENEZA LETU hadi watapotuzika kabisa.

Msumari mwengine mjarabu kabisa ni kule kuunganishwa kwa Afro-shirazi party (ASP) na TANU, 1977 kinyume na Marehemu mzee Karume alivyowausia wandani wake wasifanye,kwani yeye binafsi hakuridhia hilo katika utawala wake mzima wa miaka 8 .Kwa msumari huo,hatima ya kisiasa ya Zanzibar ilianza kuamliwa Dodoma badala ya kisiwandui. Rais wetu Aboud Jumbe alipofanya nyoko huko Dodoma, 1984 , alikiona kilichomtoa kanga manyoya. Kuanzia hapo hata viongozi wetu wa Zanzibar bila ya ridhaa ya Dodoma,ni mwiko kukalia kiti cha Urais. Wenzetu wanatuchagulia hata viongozi wetu na marais wetu-aibu gani hii ?

Msumari mwengine katika jenzea la Zanzibar ni kuondolewa kwa wadifa wa ” Makamo-rais ” na kumfanya Rais wetu kana kwamba ni rais wa kilabu cha mpira cha ” MIEMBENI SPORTS CLUB”. Hana nchi .

Na pale Zanzibar ilipojiunga na Jumuiya ya Nchi za Kiislamu (OIC) ili inufaike kiuchumi,mshirika wetu wa muungano alitutia munda na kuupiga msumari mwengine katika JENEZA la kuizika Zanzibar katika Jukwaa la Kimataifa. Marais Mwinyi na Salim,in wakavuliwa nguo hadharani na wakakemwe na Mwalimu Nyerere watoke kwa mlango wa nyuma kama walivyoingilia. Kwani, zanzibar haitakiwi kuwa na sauti katika jukwaa lolote la kimataifa na hata kucheza dimba katika FIFA-Shiriklisho la kabumbu Ulimwenguni.

KABLA SHEREHE ZA MIAKA 50 ZA MUUNGANO 2014, MAITI (ZANZIBAR) iwe tayari kuzikwa kupitia KATIBA MPYA YA TANZANIA. Zanzibar inazikwa kule kule UMOJA WA MATAIFA,NEW YORK,ambako kaburi lake lilichimbwa 1965 pake kiti chake kama dola huru huko kilipotoweka kwa njia za kiini macho. Tanzania-bara (Tanganyika) inajua kucheza turufu yake huko kuizika Zanzibar katuika kaburi lile lile iliochmba 1965 kufuatia Muungano.
Baada ya kupora fedha zetu kutoka Jumuiya ya Afrika Mashariki iliovunjika ,sasa mshirika wetu wa Muungano amejiwinda kupora gesi na mafuta yetu kwa kuitanua mipaka ya bahari kama alivyotanua mipaka ya aridhi katika Tanganyika kubwa kwa jina la Tanzania. Wakati maliasili zao kama gesi,Tanzanite, dhahabu na almasi ,makaa ya mawe na nyenginezo, ni mali zao pekee yao, mafuta na gesi ya Zanzibar na Pemba ni ubia.

VIONGOZI WETU WA ZANZIBAR NA SISI UMMA WA ZANZIBAR, TUTATUMBUA MACHO MPAKA LINI ?
MPAKA TUZIKWE KABISA HUKU SANDA TUMESHASHOBEWA NA TUNAIONA ?

Kuna usemi “Kila umma unapata viongozi uliostahiki kuongoza.Ukiwa umma ni ngangari, utapata viongozi ngngari kama akina Jussa,Hamza na Mansuri -wenye kupaza sauti kuutetea umma.La ,ukiwa umma ni wazembe, watapata viongozi wazembe.

Wazanzibari mpo ?
Tusigeuke ile hadithi ya Mnyamwezi ” Ninamtajama tu” kumbe mwenzake anamharibu.Eti anatafuta ushahidi.
USHAHIDI kuwa mshirika mwenzetu wa Muungano hakuwa na nia njema tangu awali ilidhihiriuka pale alipopiga msumari wa kwanza,April,1964 kwa kuifuta Tanganyika .
Ilikua tangu wakati ule Viongozi wetu kuwaambia ndugu zetu kuwa, BILA YA TANGANYIKA, HAKUNA MUUNGANO.Mumeuvunja wenyewe. TUNAWEZA HATA KUWAAMBIA HIVYO LEO LAITU TUNAVIONGOZI NGANGARI- KERO ZIMETOKA WAPI IKIWA HAKUNA MUUNGANO.JAMANI “SI ULIANZA UFIZI NDIPO YAKAOTA MENO ?”
si nchi “.
Ningelikua mimi ni Rais wa Zanzibar,ningekwenda Studio za Raha leo na kulihutubia Taifa nikiwaamrisha wabunge wote wa Zanzibar katika Bunge la Muungano huko Dodoma, warudi Zanzibar mpaka waziri-mkuu Pinda, ama amewataka radhi Wazanzibari na Rais wao au washirika wetu katika huo Muungano,wameifufua Tanganyika walioifuta kini-macho.
Je, Wazanzibar mpo au tunasubiri kuzikwa kabisa 2014?
ILI KUZUWIA KUPIGWA MSUMARI WA MWISHO KATIKA JENEZA LETU ,TUDAI TUJADILI KWANZA UHALALI WA MUUNGANO KABLA KATIBA MPYA.KWANI, ULIANZA UFIZI NDIPO YAKAOTA MENO !

Tagseez
Share: