NATAMANI NGEKUWA NYUMBANI!
Written by mseto // 10/09/2010 // Makala/Tahariri // 2 Comments
Natamani ngekuwa nyumbani… leo ingekuwa ni siku ya mashamsham ya kila namna… kwanza najua kabla ya kwenda mskitini kuswali swala ya eid ningeambiwa nikachinje kuku, kuku huyu angekuwa yule jogoo tuliemfuga kibandani kwetu kwa kuku au yule wa kununua markiti speshel kwa ajili ya siku hii ya leo. utamu wa kuku huyu katu haufanani na hawa wanaoitwa kuku huku nliko.. maana wa huku ukiwala ni rahisi kusahau wala nini, mpaka ukumbuke kwa nini ulikwenda super market ndipo kumbukizi zikujie kuwa ulikwenda nunua kuku. wa kule nyumbani utamuwe umote: ungozini, unyamani, u’mfupani.
Haya. Likimaliza la kuku sasa ntavalia kwenda mskitini. Si jinzi. Aa, hii si siku ya jinzi. Ntavaa kanzu ya darizi au ya lasi, imeremetayo nzi aogope tua. kichwani kuna kilemba mfungo wa kiyemeni, kiomani au simpul, ningekitupia tu kichwani na mabegani: kisuudi. miguu ingedhibitiwa na makubadhi aina ya “MADE IN KWA HAJI TUMBO” au popote pale Zanzibar. Uturi ni lazima. Kwa leo ningejipaka miski ya kidonge, hii uturiwe ni wa mbali. Hapo huyoo bismillahi tawakkaltu ala Llah… naelekea mskitini.. na mswala wangu mkononi; hakiba.
Tafauti na huku, chambilecho waswahili, kimoja hakichaguliki: ukitaka n’chicho hwetaka n’chicho. Ngekuwa nyumbani ngejiuliza nende mskiti upi? Ingetegemea sasa: nataka sauti nzuri ya imamu, nataka kwenye watu wengi, nataka khutba nzuri au penye kisabeho cha tende. Mote ngemutaka, ila ngechagua pamoja.
Baada ya swala kumaliza na kusalimiana, na kukumbatiana na kubusiana na waislam ngevaa makubadhi yangu (baada ya kukifichua kimoja pembe hii na chingine nyingine) nkaelekea nyumbani sasa. Njiani ngesikia kasida za kiindonesia zikisomwa, zihusianazo na siku hii maalum. Ningepishana na watoto ambao wangeniamkia kwa tabasamu la nyuzi 180, ili nikiitikia tu wanambie “sikukuu yangu”. ngetia mkono mfukoni hawagaia chochote.
Nyumbani ukumbini tayari vyakula vijuu ya mkeka, vimefunikwa makawa. nawasubiri salim, sele bakari na wengine wasijao rudi miskitini. Ntajipumbaza kwa pirika hii na ile mpaka waje. Malaji yataanza.. Jinsi siku hii ilivo na baraka, hungeweza juwa kuwa familia hii ni ya kimaskini kwa aina za vyakula zilizopo hapa. Pana makombo alawi, sambusa, katlesi, vileja, vitumbua, meatrolls, badia, kaimati, kuku wa kupaka, mchuzi wa kuku, mikate ya ufuta, chapati, mikate ya gole, maandazi ya mafuta, mkate wa kumimina, keki, visheti na vingi vinginevyo nsivyovikumbuka kwa sasa. Ila kuna maandazi ya kupambia: haya hupambiwa kwa moto wa makumbi na vifuu ambavyo tulivitafuta na kuvikusanya kuanzia mwezi 27.
Tukimaliza hapo, kinachofuatia ni kwenda kujishibua kwa kucheza mpira. Aghlabu huwepo mechi kati ya waliooa na wasioowa. Kwa mara ya kwanza ningekuwa naichezea timu hiyo ya kwanza. Au kungekuwa na mechi ya wavutao na wasiovuta sigara: timu yangu ingekuwa ileile.
Almuradi nyumbani kuna mengi yanayoifanya siku hii kuwa KUU. Na yote nayatamani. Nyumbani “atmosphere” ya ki-sikukuu huanza wiki kabla na hubaki wiki baada ya sikukuu yenyewe. Huku, Afanaalek! Kwanza kuipata hiyo siku tu japo si kuu basi ni tabu tupu. Kwa kuwa ni siku ya kazi kama kawaida basi imenibidi kazi yangu ya Ijumaa nikaifanye usiku wa alhamis/ijumaa. nlale kidogo ndipo nende huko holini, watu waswaliko. Kwa mimi siku (ukipenda sikuKUU) yote huisha baada ya swala ya eid. Nilipo sina kombo alawi ela kombo shomari. Alhamdulillahi nna visheti vyangu nlivyoletewa zawadi mwezi ulopita, ntavila na kahawa siku[KUU] ishe!. Alhamdulillahi Rabbil Aalamina!
Nakutakieni SIKUKUU njema popote mlipo!
————–
Hamad²
Copenhagen





2 Comments on "NATAMANI NGEKUWA NYUMBANI!"
kahamad umentowa chozi skukuu ya znz tamnuu mungu atatujaliya tutaila nyumbani kila mwaka
KULLU AAMUN WA ANTU BI KHAYR.
SHEIKH WANGU MAMBO KMA HAYA USIANDIKE, UNATULIZA KWA SANA. JAMANIIII EEEEE HEBU FANYENI HUO UCHAGUZI HUKO HALAFU HIYO SERIKALI MUITULIZE NA ZAINZIBAR IWE NCHI KAMILI ISIYOTAWALIWA NA WATANGANYIKA TURUDIIIIIII, TUSHACHOKA KUISHI NCHI ZA WATU HATUNA THAMANI HATA UWE NA PHD MPAKA ZA UNDER WEAR BASI UTABAKI AS BIN MAN, WATCH MAN, SALES MAN.
JAMANI TUNATAKA KURUDIIIIIIII.
AH, SIKU KUUU NYUMBANI BWANA, SAA KAMA HIZI KUSHAJAZA WATOTO WAKO NA WA JIRANI HUYOOO MWENYEWE WAENDA KUTEMBELEA WAGONJWA, JAMAA NDUGU NA MARAFIKI, KUZURU MAKABURI NA KUWAOMBEA DUWA WAZEEE WAKO. AA AH LAKINI WAPI! YOTE NI HII CCM.