Makala/Tahariri

NYERERE ALIVYOMTETEA KARUME ACCRA KUHUSU ”UHURU ZUIYA’

NYERERE ALIVYOMTETEA KARUME ACCRA KUHUSU ”UHURU ZUIYA”
Mohamed Said May 10, 2017 0

Katika gazeti la Raia Mwema leo (Mei 10 – 16, 2017) Barazani Kwa Rajab, Ahmed Rajab kaka yangu na na mwalimu wangu katika uandishi kuna makala, ‘’Nyerere alivyomtetea Karume Accra.’’ Toka mapema leo washabiki wa Ahmed Rajab nje na ndani ya Tanzania wananiletea taarifa kuw akuna kigongo barazani kisinikose, lakini hawaniambii kigongo gani kwani kwa uoni wao hawataki kunipunguzia utamu. Naam Makala hii ni kigongo khasa wala hapana shaka. Ahmed Rajab kagusa vitu vitatu muhimu katika historia ya Zanzibar kwanza kuanzishwa kwa Afro-Shirazi Party (ASP) katika misingi ya ukabila na ubaguzi mwaka wa 1957 kije kipambane na chama cha Zanzibar Nationalist Party (ZNP) chama cha kizalendo cha kupigani uhuru. Hii Mosi. Pili ASP kuanzishwa kwa mkono wa Nyerere na tatu sera ya Karume na ASP sera yake ikiwa kukataa uhuru kwani uhuru utawanufaisha Waarabu. Anaetaka zaidi atamsoma Ahmed Rajab mwenyewe ila mimi nataka niguse pale aliposema kuwa hii siasa ya kuanzisha vyama vya siasa kwa misingi ya kikabila ilikuwa mbinu ya Waingereza kuwagawa Waafrka ili waendelee kuwatawala mbinu ambayo Ahmed Rajab kaeleza kuwa Waingereza waliijaribu Tanganyika lakini haikufaulu. Hapa Ahmed Rajab kanitaja kuwa mimi nimeieleza kwa kirefu katika kitabu cha Abdulwahid Sykes…

Namyambua kidogo kitabu cha Abdulwahid Sykes (1924 – 1968):

”Kueleweka kwa nini Abdulwahid alimuunga mkono Nyerere inahitajika uchambuzi kuelewa siasa za mfumo wa kikoloni katika Tannganyika. Mwaka wa 1951 Abdulwahid na Mwapachu walipokuwa wakishughulika kuifufua TAA, walijiwa na Ivor Bayldon, Brig. Scupham na V.M. Nazerali kuombwa kuunga mkono kuundwa kwa chama cha kisiasa kitakachojumuisha Watanganyika wa rangi zote. Hawa walikuwa wajumbe wa Baraza la Kutunga Sheria. Bayldon alikuwa mlowezi tajiri kutoka Nyanda za Juu za Kusini na alikuwa amehamia Tanganyika kutoka Afrika ya Kusini. Wajumbe wa Kiafrika wa Baraza la Kutunga Sheria walioliunga mkono wazo hili walikuwa Chifu Kidaha Makwaia na Liwali Yustino Mponda wa Newala . Watu wengine mashuhuri walioshauriwa na kuombwa kuunga mkono chama hiki walikuwa: Dr Joseph Mutahangarwa, Chifu Abdeli Shangali wa Machame, Chifu Mkuu Thomas Marealle wa Marangu, Chifu Adam Sapi Mkwawa, Chifu Haruna Msabila Lugusha, Dr William Mwanjisi, Abdulkarim Karimjee, Dr Vedasto Kyaruzi, Liwali Juma Mwindadi, H.K. Viran, Stephen Mhando, Ally Sykes na Dossa Aziz .

Huu ulikuwa mchanganyiko wa Wazungu ambao tangu hapo walikuwa raia wa daraja la juu, baadhi yao kama Bayldon walikuwa walowezi; machifu kama vile Marealle, Waafrika wasomi kama Mwapachu; tabaka ya wafanyabiashara wa Kiasia kama Karimjee na watu wa mjini kama Dossa Aziz na Juma Mwindadi. Wote hawa walikuwa viongozi waliokuwa na wafuasi katika jumuiya zao. Katika barua Nazerali aliyomtumia Ally Sykes miaka miwili baada ya kudhihiri kuwa chama kile walichokusudia kisingeweza kuundwa, Kwenye sehemu moja alikuwa na haya ya kueleza: ëHaja kubwa ilikuwa kuandaa kikundi cha watu walio wakweli, waaminifu na wenye imani katika maendeleo ya watu katika nchi yetu, pamoja na fursa sawa kwa wote.

Abdulwahid wakati huo akiwa katibu pamoja na wanachama wa TAA wasingeweza kukubali wazo kama hilo. Ingawa kwa kiasi fulani malengo ya chama hicho kilichokusudiwa yalionekana yanafanana na malengo ya wananchi hivyo kudhihirisha barabara kile ambacho TAA ilikuwa ikikipigania, Waafrika wasingeweza kuachia azma ya wa Tanganyika kwa dhamira njema ya wasiokuwa Waafrika na ambao walikuwa wakishirikiana bega kwa bega na serikali ya kikoloni. Ilikuwa dhahiri kuwa Wazungu na Waasia nchini Tanganyika hawakutaka kukubali kuwa Tanganyika kwa hali yoyote ile ilikuwa nchi ya Waafrika. Kwa TAA kukubali kuundwa chama cha siasa kitakachojumuisha mataifa yote, kulikuwa sawa na kuyaweka maslahi ya Waafrika katika mikono ya watu wachache…”

Chini: Ali Muhsin Barwani, Mohamed Shamte, Hasnu Makame na Abeid Amani Karume

Share: