Makala/Tahariri

SERA YETU KUBWA NI KUHUBIRI AMANI NA UTULIVU

Na: Farrell Jnr foum

1. Kilichofanyika jana ni kupeleka “message” Dodoma kuwa utulivu wetu si wa shuruti bali ni wa nia na khiyari yetu wenyewe. Tumeamua amani kudai haki yetu ili iwe rahisi kujenga mafahamiano, kurejesha mapenzi na udugu wetu pamoja na kuitumia siasa kama chombo cha maendeleo badala ya fujo, mauaji na hasama. Haya maji ya mtungi yana mwenyewe, mwenye umma, ulio na lengo si papara. Utulivu huu si udhaifu wetu bali ndio nguzo ya mafanikio yetu, usicheze kabisa na umma wenye imani, wenye ari na wenye uthubutu. Msema kweli kipenzi cha Mungu, ila msema kweli asietenda haki ndie adui wa kwanza wa Mungu. CUF ni taasisi na Zanzibar ni nchi yenye historia, ustaarabu na utamaduni wake, haiwezi kuondoka katika vifua vya wale ambao vitovu vyao vimezikwa katika vijiji vya asili zao, wale waliokoshewa majimbo ya miti ya vijiji vya asili zao ambao makaburi ya mababu na mabibi zao yapo yakibeba nasaba zao.

2. Tumepeleka taswira kwa malaika na genge lake kuwa ruka upae, Zanzibar ina wenyewe, ina ustaarabu wake, ina khulka zake na kamwe hatutafitinishwa na yoyote katika madai yetu ya haki, usawa na heshima kwa kila pande. Njoo utukane, tuma wa kutukana, jipange hasa kwa matusi yote kwa kila mmoja wetu. Lakini hatutoki katika njia za haki za kusukuma mabadiliko, kung’ang’amua ndio huku. Kusukuma mabadiliko katika njia zenye athari ndogo kwa wananchi hasa ustawi wao lakini kubwa kwa mtawala asietakiwa. Tumechaguwa juwa kulivua koti la uonevu na si upepo utaovunja hata majumba yetu. Lilipulizwa Zanzibar na coast nzima ikacheza, na sio kinyume chake. Mutaielewa maana halisi ya msamiati huu, sisi si Burundi, tumehitimu na somo la 64, mzungu anasema “Never again”.

3. Tumepeleka ujumbe mzito kwamba CUF ni taasisi madhubuti yenye umma, unaojali umoja, na utaosimama na umoja wa upinzani katika harakati zake za kusukuma mabadiliko ya kweli nchini. Si msajili mwenye funguo ya uwepo wa CUF bali vifua visivyokata tamaa katika madai ya haki, si mkuu wa polisi wala Bwana yule ataeuzorotesha upinzani kwa mgongo wa CUF. Wache wakupe jeshi hasa upite kila kijiji, kata, mji, wilaya na mkoa, kamwe hutarudi katika vifua vyetu vilivyokuamini ukatucheza shere. Bebwa na msajili, geuka nawe Jecha kuwabeba wanaokutumia kwa kutazama papara badala lengo, hii ni taasisi yenye umma, si klabu ya kahawa, mdundiko au zumna ya Malindi. Zindiko letu ni umma, si mtu au mtutu, au khofu, wala si kafara na kuvunja nazi njia panda.

4. Na kwa mafisi wanaofikiri mkono kuyumba ni udhaifu, wajitathmini. Siasa ni kusonga mbele, si visasi visivyokwisha. Hakuna anaeweza kushinda akiwa mpinzani bila ya kuungana pamoja alau kuhakikisha bunge kwanza linarudi katika ukuu wake unaohitajika, uhuru wake wa maamuzi na ukweli wake kwa wananchi. Njia ni mbili ima na mtawala katili, aliejaa na kiburi na uimla au umoja utakaoziba udhaifu wa mmoja kwa nguvu za mwengine, nipe nikupe. Hakuna aliekamilika na dhana ya umoja ni kustahamiliana, kujenga uaminifu, kujenga mafahamiano mapya hata baada ya msongamano. Siasa za kutegeana mwisho wake hazina chochote zaidi ya unafik tu, hakuna anaeweza kuleta mabadiliko akiwa mpinzani pekee bila ya umoja. Vuguvugu linasimama wakati haki iko huru, sio wakati muimla anaejitapa kwa nguvu na utukufu wa mitume na malaika.

5. Na kwa wale “pessimist” hakuna kukata tamaa, hakuna khofu ya umma kukata tamaa, hakuna kusukumwa katika tanuri la maafa. Hebu tuitazame Burundi na Congo na mauaji yale mwisho wake ni kitu gani? Wote wamerudi mezani kujadili muelekeo mpya, kung’ang’amua ni kutumia akili, nguvu za akili na uwezo wa akili kufikia lengo bila ya makosa ya 64 yaliozaa hasama, visasi, kutoaminiana hata kwa vizazi visiohusika na chochote zaidi ya historia, rangi na nasaba zao. Umefika wakati hasa kujiamini na kuamini kwamba kamba hii dhaifu, inahitaji juwa kali na si upepo wa kuezua mabati na kututia hasara inayoepukika. Nani anaedumu bila ya ridhaa hasa ya anaeongozwa? Kilichofanyika ni kuziba nyufa wakati ukuta umewekewa mwega, umeshainama, nyumba nzima imeshadata. Tuwatazame wanyonge wale waliofurika kumsikiliza kiongozi wao, kweli hawana hisia za maumivu ya kuporwa haki yao? Kinachowatutumua ni nini? Defiance defiance defiance, naam mpaka haki isimame, iwe leo, kesho au kesho kutwa lakini itasimama kwa umoja wetu, ari zetu na ukweli kuwa tuna lengo, sababu na umadhubuti kama taasisi ya kutuvusha na kutufikisha katika lengo, zaidi tuna Mungu anaesimama na haki tena kwa wakti wake akipima subra za wanaomtii.

fb

Share: