Shein akosa sifa za kushiriki uchaguzi wa Zanzibar
Written by Mrfroasty (Ufundi) // 18/07/2010 // Makala/Tahariri // 8 Comments
- Shein kuwa rais wa mwanzo asieweza kujipigia kura
- Utata wa kisheria, Dk.Shein hana sifa za kupiga kura Zanzibar – vipi ataweza kuwa rais?
UTEUZI wa Dk. Ali Mohammed Shein kuwa mgombea urais Zanzibar huenda ukazua utata, MwanaHALISI limeelezwa.
Dalili za utata zilianzia kwenye Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) mjini Dodoma, Ijumaa iliyopita wakati mjumbe mmoja alipotaka Dk. Shein aondoe jina lake kwa madai kuwa amekosa sifa za kugombea urais Visiwani.
Mjumbe aliyewasilisha hoja ya Dk. Shein kuondoa jina lake ametajwa kuwa ni Nimrod Mkono, mbunge wa Musoma Vijijini ambaye pia ni wakili wa mahakama kuu.
Kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar, Ibara ya 26 (2), sifa za kuchaguliwa kuwa rais ni pamoja na kuwa Mzanzibari wa kuzaliwa na aliyetimiza umri wa miaka 40.
Sifa nyingine ni kuwa na “sifa za kumwezesha kuchaguliwa kuwa mjumbe wa Baraza la Wawakilishi; na mwanachama na mgombea aliyependekezwa na chama cha siasa kilichosajiliwa rasmi kwa mujibu wa sheria ya vyama vya siasa ya 1992.”
Lakini katika eneo la haki ya kupiga kura, kuna sharti la nyongeza ambalo ndilo linaonekana kuangaliwa zaidi na wapinzani wa Dk. Shein kuwa mgombea urais Zanzibar.
Ibara ya 7 kifungu kidogo cha 2(d) inasema Mzanzibari aweza kuzuiwa kutumia haki ya kupiga kura kutokana na “kukosa au kushindwa kuthibitisha au kutoa kitambulisho cha umri, uraia au uandikishwaji kama mpigakura.”
Katika eneo hili, hoja ni kushindwa kujiandikisha katika daftari la wapigakura Zanzibar. Taarifa zilizopo zinaonyesha kuwa Dk. Shein alijiandikisha Oyster Bay, Dar es Salaam na siyo Zanzibar.
Sifa ya kujiandikisha inajitokeza pia katika Sehemu ya Tatu inayohusu, pamoja na mengine, Baraza la mawaziri.
Ibara ya 68(b) kuhusu sifa za kuchaguliwa chini ya eneo hili inasema anayechaguliwa sharti “awe amejiandikisha au ana sifa za kujiandikisha katika jimbo la uchaguzi kama mpigakura katika uchaguzi wa Baraza la Wawakilishi.
Eneo hili pia linamgusa Dk. Shein ambaye anadaiwa kutokuwa “mkazi” wa Zanzibar “kwa zaidi ya miaka saba sasa.”
Kwa mujibu wa kanuni za kujiandikisha kwenye daftari la wapigakura, sharti mtu awe Mzanzibari mkazi na kuwa na hati inayothibitisha hivyo.
Wanaopinga uteuzi wa Dk. Shein wanadai kuwa ana hati ya ukazi Zanzibar anayodaiwa pia kukabidhiwa hadharani, lakini hakuitumia kujiandikisha kupiga kura Visiwani.
Kwa mujibu wa taratibu za kupata hati ya ukazi, kila Mzanzibari ambaye amekuwa nchini kwa miaka mitatu mfululizo, anastahili kupewa hati hiyo. Awali sharti lilikuwa miaka mitano.
Wakili mmoja wa mahakama kuu mjini Dodoma ameliambia MwanaHALISI, “Sijaelewa vema hoja za pande zote mbili, lakini jambo moja kuu ni kwamba ili kupiga kura, sharti uwe umejiandikisha.”
“Kama Dk. Shein hakujiandikisha basi hana sifa ya kupiga kura,” amesema. Kwa mujibu wa katiba, “Zanzibar itahesabika kuwa ni jimbo moja.”
Hili linafafanuliwa kwa maelezo kuwa aliyejiandikisha kupiga kura katika kumchagua mjumbe wa baraza la wawakilishi atakuwa na uwezo wa kupiga kura katika uchaguzi wa rais katika jimbo hilohilo moja.
Katika katiba ya Zanzibar hakuna panapoonyesha kuruhusu kuhamisha hati ya kupiga kura kutoka upande mmoja wa Muungano kwenda upande mwingine.
Katika mazingira haya, wapinzani wa Dk. Shein wanasema hawezi kujipigia kura na hawezi kupigia yeyote katika visiwa vya Unguja na Pemba kwa kuwa anabanwa na sheria.
Aidha, Dk. Shein hana uwezekano wa kuandikishwa kwa sasa kwa kuwa zoezi la kuandikisha wapigakura tayari limefungwa kwa pande zote mbili za Muungano.
“Hatua ya kuruhusu mgombea urais kujiandikisha wakati zoezi limekwishafungwa, itatafsiriwa kuwa ubaguzi; jambo ambalo ni kinyume cha Katiba ya Zanzibar na ile ya Jamhuri ya Muungano,” ameeleza wakili.
Hoja ya Dk. Shein kuwa au kutokuwa na sifa ilichukua muda kujadiliwa ndani ya NEC. Ilikuwa baada ya Mkono kulitupa uwanjani, aliyekuwa mwanasheria mkuu wa serikali, Andrew Chenge aliidaka na kumtetea mteuliwa.
Chenge ambaye amekuja kujulikana zaidi kwa jina la “mzee wa vijisenti,” alitumia hoja ya Ibara ya 26(2)(c) inayosema mgombea awe na “sifa za kumwezesha kuchaguliwa kuwa mjumbe wa Baraza la Wawakilishi” na mwanachama aliyeteuliwa na chama chake.
Awali Mkono alishauri Dk. Shein kuondoa jina lake ili kukiepusha chama kukumbwa na fedheha. Alisema kwa mujibu wa Katiba, mtu mwenye sifa ya kugombea urais Zanzibar lazima awe na sifa ya kuchagua mwakilishi au kugombea ujumbe wa Baraza la Wawakilishi.
Kwa mujibu wa mtoa taarifa, hoja ya Chenge ilipokewa na Mwenyekiti wa CCM, Rais Kikwete aliyechukua muda mrefu kufafanua moyo wa katiba ya Zanzibar, akisema kuwa alichokuwa akitumia ni “tafsiri ya kisheria.”
Iwapo Dk. Shein ataweza kuchaguliwa kuwa rais wa Zanzibar, atakuwa rais wa kwanza nchini kuchaguliwa bila yeye kujipigia kura.
Kawaida, vyombo vya habari duniani, katika nchi za kidemokrasi zinazotumia uchaguzi, huwafuata viongozi wanaowania nafasi za juu kupata ushahidi wa wao kujipigia kura, ikiwa kielelezo cha kuonyesha umma umuhimu wa kutumia haki yao kuchagua wanayemtaka.
Kwa upande mwingine, taarifa kutoka ndani na nje ya vikao vya CCM zimeeleza kuwa kushindwa kwa Dk. Mohammed Gharib Bilal kuwa mgombea Zanzibar kulitokana na kuungwa kwake mkono na baadhi ya viongozi bara.
Chanzo:mwanahalisi





8 Comments on "Shein akosa sifa za kushiriki uchaguzi wa Zanzibar"
Mwandishi umetueleza kwa kina kifupi dira ya DK. Shein ,tusubiri jingine hili washalipanga wanapinda sheria zao wenyewe utetezi wa dokt kikwete ni ishara tosha kuwa huna njia ya kunikatalia alau tushukuru kaja Mchokocho sio kutoka Swanga mwenye uwezo na hekima ya kuiongoza Zanzibar CCM ZNZ waamke msileweshwe,kwa rusha roho
Asante kwa makala yako nzuri. unajua haya mambo kuhusu huyu muheshimiwa ama hayakuekwa sawa mapema kabla ya uchaguzi hali itakua mbaya zenji. sio kwa upinzani ni kwa CCM. unajua ccm huyu kijana hawamtaki hasa. nimefanya utafiti wa haraka haraka tu kama siku saba hivi kuzunguka mitaaa ya zenji yaani hawantaki kabisa sababu tofauti napata sababu nilizopewa nazifanyia utafiti zaidi ili nijue kama zinauzito wowote au nichuki binafsi tu ndani ya chama hichi. ila kwa ufupi kwa sasa hali ni mbaya mmno, hili la kuto kujiandikisha ni miongoni mwa sabab ndogo tu ambayo wanaisema njenje sababu wanajua inasemea ila wana sababu nyengine nyingi sana ambazo kama wataiteeleza hali itabadilika zenji karibu tu. kinacho tusaidia wazenji ni waoga sanasana wanasemea ndani tu hawasubutu kusema hadharani.ukweli ni kwamba CCM wa zenji kijana hawantaki. ila mwakahuu ndo uyo uyo atakaenuna naapasuke.
Tunasubiri kwa hamu matokeo ya utafiti wako…kwani kunahitajika utafiti?Mie nilidhani iko clear huyu jamaa hatufai visiwani mwetu.
Anyways tusiandikie mate na wino upo, nasubiri utafiti wako mkuu.Na nitafurahi ikiwa hauna dhana za kibaguzi ndani yake, maana mtandao huu unapinga ubaguzi vikali sana.Na Mods wako imara kwa kushirikiana na watembeleaji kufuta machapisho yenye masuala ya ubaguzi mioni mwa jamii.
Maasalaam,
mrfroasty
@ Mshauri: ningeomba pia utupe msimamo wako binafsi juu ya Shein kabla hujatuchambulia huo utafiti. Na pia tungependa kujua ni mitaa gani uliyoifanyia utafiti. Isiwe umekwenda Kisonge tu halafu ukasema “vijana hawamtakaGI kabisa”. Lakini kumbe ukitembelea Nungwi au Chokocho wanamfagilia.
Mimi ninavyofahamu kuna mgawanyiko mkubwa juu ya wanaomtaka na wasiomtaka, tena mgawanyiko huu ni wa kimaeneo zaidi kuliko wana-CCM binafsi. Sasa utafiti wako usiwe umelenga upande fulani. Halafu ukatumpa matokeo ya jumla kutoka kwa watu wachache wanaojulikana mrengo wao. Utafiti wako uwe “free & fair”, sio ufuate nyazo za ZEC za kupika matokeo.
@ Nshauri (waonekana lahaja inkuganda – lkn ni jambo zuri kuwa na ‘cultural identity’)
Asante Bw/Bb Nshauri kwa maelezo yako. Lkn ingekuwa uzuri kama ungetwambia huo utafiti wako wa haraka haraka umetumia hadidu rejea gani mpaka ukafikia hitimisho hilo! Tuwekee uwazi nasi tupate changia kwa nshuwariko zaidi!!
tumuombeeni dua ajifunze hizo sifa zinazomruhusu mtu kugombea uraisi na yeye awenazo ingawa keshachelewa, kwani itakuwa khasara ikiwa sifa hana, na imani, na hata akili hana, lakini m/mungu ampe hizo sifa walizonazo wenziwe, na awe ni mwingi wa huruma juu ya wanyonge, zaidi atazame maslahi ya walio chini yake kuliko ya walio juu yake, na atapohisi ana wasi wasi juu ya uongozi wake M/mungu amuoteshe usingizini akiamka keshasoma ili asomeshe na baraza lake, na ramadhani hii Inshallah iwe kun fayakun, mahasidi ni kila pahala. ila M/mungu awape usingizi mara hii inshaallah kwa uwezo wake, wakiamka tushajaa maendeleo zanzibar amin, amin, amin
Ushindi wa bure hata hauna maana. Mimi nataka wote waende kwenye uchaguzi na kila mmoja amwage sera zake, ikisha sisi wlala hoi, tuamuwe nani wakumpa.
Jambo jengine muhimu ni kuwa mwaka huu au uchaguzi huu tuna imani kidogo uchaguzi unaweza kuwa huru na haki, kwa upo uwezekano wa CUF kushinda kwa vile chaguzi zote wamekuwa wakishinda lakini wakuu hawakutaka CUF wapewe.
Tutakapo kuwa na uchaguzi huru na haki, manaake tutapata nafasi sote kwa CCM na CUF kupata haki sawa tokea hatua za mwanzo za kampeni na siku ya kupiga kura. Mimi nina imani, kama utamuachia Maalim Seif aingiye Donge na kujieleza, basi CCM wataadhirika. Akipata fursa kuingia Tumbatu, basi CCM hawatoamini kabisa. Hili ni jimbo la CUF, sema CCM wanatumia nguvu tu. Huko Kashakazini mpaka masheikh wakubwa wakubwa wa pande hizo wana iunga mkono CUF. Bubwini ni jimbo la CUF, lakini CCM wamekuwa wakitumia nguvu, halikadhalika Mwera. Jamaani sisi binaadamu, tumepewa uwezo wa kufikiri. Kwa hiyo ukinia mimi kama wasmeavyo vijana na “PUMBA” nitakuwachia nalo. Ukija ukanipa vitu vyenye kuleta muelekeo basi nitakufahamu. Huwezi kumuahidi mtoto wa form II atapata ajira serikalini. Lakini ukimuambia nitakuendeleza kwa yale mambo unayo pendelea, basi hapo inaingia akilini.
Tupo kwenye wakati wa Maridhiano. Sote tumeshuhudia magovi yasiyo kusha kila inapo fika wakati wa uchaguzi. Ni matarajio yetu july 31 mambo yatakuwa mazuri kwa upande wa NDIO. Itakuwaje pindi ikithibitika Dr Shein hana sifa za kugombania u-rais? Na kusudia kwa ile nafasi ya umakamo. Kwasababu kama atakubalika kwa hiyo akishinda atapewa wa upidhani, akishinda Maalim Seif umakamo ni wa Dr Shein. Kitakacho tokezea ni CCM kuwa na wawakilishi lakini kura za Rais hazipo. Labda na wao wapige kura za maruhani na hii ikithibiti kura za maruhani zimepindukia 50% CUF wataupokea vipi ushindi huo? Kwa hiyo kuja kwa CUF kumuekea pingamizi kwa mtazamo wangu nahisi kama watakuja kuyarejesha nyuma maridhiano. Na nafasi hii wanaweza kuja itumia watu wa vyama vyengine kwa lengo la kutaka kuwaonesha CYF na CCM kuwa na sisi mulitutenga kwenye mazungumzo.
Inshallah haya yanayo nitatiza mimi yote yasiwepo na tuende salama kwenye kupiga kura na mwishowe tuendeleze maridhiano yetu.
Ahsanteni
Sh Kassim
Umegusia kitu ambacho tikea jana nilitaka kukiandika.
Ningewasnasihi wenzetu wa CUF mambo ya ngoswe wakamuachia ngoswe mwenyewe. Suala la Dr Shein kuwa au kukosa sifa wawaachie CCM wenyewe. Hapa wasithubutu kujiingiza kwani ni mtego (wa Tom & Jerry). Wahafidhina hawakuridhika, wao watafanya kila vitimbi kuvuruga haya yaliyopatikana. Yapi hayo!! SUK (serikali ya umoja wa kitaifa). Aina yoyote ya kipingamizi kitazua kitahanani ndani ya Zanzibar.
Pia nachukua nafasi kuwaasa vyama vyengine vilivyopo Zanzibar wasijaribu kutokonyoa haya mambo. Ikiwa Shein tokea halmashauri kapita halmashauri maalum, kamati kuu, na halmashauri kuu ya taifa, hatazuilika katika mahkama yoyote ile. Kila sehemu ataonekana kweli sifa anayo.
Ukitumia logic na sio sheria hakuna kuvunjwa sheria zozote kwa Dr Shein kugombea.