Makala/Tahariri

Tamaa ya Waherero wa Namibia kufidiwa na Wajerumani

Na Othman Miraj,

Zaidi ya miaka 100 baada ya kumalizika enzi ya ukoloni wa Kijerumani katika Afrika Kusini Magharibi (nchi ambayo sasa inaitwa Namibia), kamishna wa serikali ya sasa ya Ujerumani juu ya suala la Namibia, Ruprecht Polenz, amezungumzia juu ya mpango wa kulipwa fidia kutokana na dhuluma waliyofanyiwa Waherero na Wanami wakati huo wa ukoloni. Ujerumani imependekeza kuanzishwe Mfuko maalum wa kujenga miundombinu na pia kuundwa Wakfu wa Mustakbali baina ya Ujerumani na Namibia.

Polenz aliyasema hayo mjini Berlin wiki iliopita. Pia alisema kwamba Ujerumani itaomba radhi na msamaha kwa mauaji ya kimbari yaliofanyiwa watu wa makabila ya Herero na Nama wakati wa ukoloni wa Ujerumani katika Namibia. Kamishna huyo alisema suala tu ni namna gani fidia itakavyokuwa ili kwamba iweze kukubaliwa na serikali ya Namibia. Alisema hivi sasa yanafanywa mashauriano baina ya serikali za Ujerumani na Namibia juu ya Mfuko huo ambao hasa ni kwa ajili ya vizazi vya jamii ilioathirika wakati huo wa mauaji. Mfuko wa miundombinu utaingiza miradi ya elimu, kama vile kujengwa vituo kwa ajili ya watu kijifunza kazi.

Pia kunapangwa kuanzishwa miradi ya kupata nishati mbadala kwa ajili ya vijiji vilivyo karibu na mwahala kulikofanywa mauaji ya Waherero na Wanami. Mfuko wa fedha unaowazwa utaviwezesha vizazi vya watu waliouliwa na kuteswa huko Namibia kupatiwa kwa bei nafuu nyumba zitakazojengwa kwenye maeneo hayo. Pia suala la kuanzishwa marekebisho kuhusu umilikaji ardhi katika sehemu hizo litatiliwa maanani.

Wakfu juu ya Mustakbali wa Ujerumani na Namibia una nia ya kuendeleza utamaduni wa kukumbushana kwa pamoja juu ya matukeo hayo ya mauaji ya kimbari. Kutaanzishwa miradi ya pamoja ya elimu na utafiti pamoja na kubadilishana ziara baina ya vijana wa Ujerumani na Namibia.

Itakumbukwa kwamba baina ya mwaka 1904 hadi 1908 wanajeshi wa kikoloni wa Ujerumani waliwauwa Waherero na Wanama wanaokisiwa kufikia laki moja. Wengine walifukuzwa kutoka maeneo yao na kuwachwa jangwani ambako walikufa. Waherero na Wanami wengi waliporwa ardhi zao na serikali ya kikoloni ya Kaizari wa Ujerumani. Afrika Kusini Magharibi wakati huo ilikuwa koloni ya Mjerumani.

Kwa miaka mingi vizazi vya Waherero na Wanama vimekuwa vikiitaka serikali ya Ujerumani iwalipe fidia kutokana na uhalifu huo wa kikoloni waliofanyiwa wazee wao. Lakini wanasiasa wa Ujerumani wamekataa hadi sasa kutambua hadharni kwamba kile kilichofanywa wakati huo kilikuwa nii mauaji ya kimbari. Hadi leo hakujatolewa tangazo rasmi kutoka ngazi za juu za serikali mjini Berlin la kuomba msamaha, wala kutolewa malipo ya fidia kwa vizazi vilivyofuata vya watu waliouliwa. Yanapozushwa masuala hayo, serikali ya Ujerumani huashiria misaada ya maendeleo ambayo inaipa Namibia.

Baada ya wanasiasa wa Kiherero na Wakinama kutoambulia chochote katika mazungumzo yao mjini Berlin kuhusu madai yao, mwezi Januari mwaka huu waliwasilisha mashtaka mbele ya mahakama ya Marekani dhidi ya serikali ya Ujerumani. Kesi hiyo iliposikilizwa mara ya kwanza mwezi huu, mashtaka hayo hayajatupiliwa mbali, kinyume na vile walivyohofia watu wengi. Hakimu Laura Taylor Swain wa Mahakama ya Wilaya alipanga kesi hiyo isikilizwe zaidi Julai 21 mwaka huu. „Huo ni ushindi wetu mkubwa, kwamba sisi ndio washindi“, alifurahia mwakilishi wa Wanama na ambaye ni mbunge huko Namibia, Ida Hofmann.

Wawakilishi 15 wa Waherero na Wanami walisafiri kwenda kuhudhuria katika kesi hiyo ya mjini New York. Hakimu alishangaa kwamba hakujakuweko mwakilishi wa serikali ya Ujerumani wakati wa kusikilizwa kesi hiyo.

Wakati huohuo, vizazi vya Waherero na Wanami waliouliwa wakati wa ukoni wa Ujerumani vimeungwa mkono na serikali ya nchi yao. Kutokana na gazeti la kila siku la „Namibian“, toleo lililochapishwa wiki mbili zilizopita, ni kwamba serikali ya Namibia ilikuwa ikitayarisha mashtaka dhidi ya Ujerumani. Serikali ya Windhoek inasemekana imewaajiri mawakili kuishtaki serikali ya Ujerumani mbele ya Mahakama ya Kimataifa ya The Hague na kudai dola bilioni 30. Ripoti ya gazeti hilo ilikuwa na kichwa cha maneno: “ Serikali inabadilisha Msimamo kuhusu Mauaji ya Kimbari.“ Gazeti hilo lilimnukuu mkuu wa kuendesha mashtaka, Sacky Shanghala, akisema: „ Hatua hii inachukuliwa ili serikali isikosolewe kwamba haijafanya kile ilichoweza kufanya kuzusha suala la machungu walioyapata watu waliouliwa na vizazi vyao vilivyofuata.“ Yeye anataraji kwamba „dhamiri ya wananchi wa Ujerumani itaiongoza serikali yao kuja na suluhu ambayo itapelekea kumalizika kwa heshima suala hili.“

Kwamba serikali ya Namibia nayo sasa inajitayarisha kuishtaki serikali ya Ujerumani, kinyume na msimamo wake wa hapo kabla wa kuhepa kuwa na malumbano ya kisheria na wakuu wa Berlin kuhusu suala hili, ni ushahidi wazi kwamba suala la kuilpwa fidia vizazi vya watu waliouliwa kiholela huko Namibia linapata uzito. Haliwezi kupuuzwa na serikali ya Ujerumani. Lakini pia hatua hii ya kushangaza ya serikali ya Windhoek huenda ikadhoofisha msimamo wa Waherero na Wanami ambao ndio tangu mwanzo walianzisha mashtaka ya kupigania zile wanazoziona kuwa ni haki zao. Kwa mujibu wa ripoti za magazeti ni kwamba serikali ya Namibia itaweza kuyaingiza madai ya Waherero na Wanami ndani ya mashtakai rasmi ya serikali. Huenda hapo tena fidia ikaenda kwa serikali ya Namibia na si moja kwa moja kwa Waherero na Wanami.

Pindi madai ya Waherero na Wanami yatashinda na vizazi ya sasa vitalipwa fidia, sitoshangaa kwamba madai ya fidia kwa mikasa karibu sawan na huo ya kuuliwa na kuteswa watu wakati wa ukoloni wa Mjerumani huko Tanganyika, Togo na Cameroon yakazushwa. Huko Tanganyika bado watu wana kumbukumbu za Vita vya Maji Maji ambapo inakisiwa wapiganaji 75000 waliuliwa ilipofika mwaka 1907. Pia wanahistoria wanasema askari wa Kijerumani waliwauwa mamia ya raia, wakiwemo wanawake na watoto. Serikali ya kikoloni ya Ujerumani inadaiwa ilitumia njaa kama silaha, ikiyaharibu mazao ya mashambani ya watu walioshukiwa kwamba wanaunga mkono ule ulioitwa „uasi“ wa Maji Maji.

Licha ya kwamba mapambano ya Maji Maji ya wananchi mwishowe hayakufaulu, lakini serikali ya kikoloni ya kaizari wa Ujerumnani ililazimika kufikiria upya juu ya siasa zake za kikatili katika makoloni yake ya Afrika. Ilitambua gharama itakayolipa baadae kutokana na ukatili huo.

Mapambano ya Maji Maji yaliwapa moyo wazalendo wa Kiafrika kupambana baadae na ukoloni wa Wazungu na pia kuyapa makabila mbalimbali ndani ya nchi ya Kiafrika mwamko wa haja kubwa ya kuungana ili kuushinda ukoloni. Kwamba ushindi wa Waherero na Wanami kudai haki zao utawatia moyo watu wengine kujaribu hivyohiyo, hilo ni jambo la kusubiri na kuona. Maajabu mengi yamejificha katika mustakbali wa mwanadamu, lakini historia haiwezi kujificha. Ni kama mtoto wa haramu, lazima siku moja atanyosha kidole chake juu ili baadae ajulikane.

Share: