Makala/Tahariri

Tunaishi katika zama za madikteta mamboleo

Ahmed Rajab
JARIDA la Foreign Affairs la Marekani, toleo la Septemba 26, 2016, lilikuwa na makala kuhusu “madikteta mamboleo”. Jarida hilo linawaita “madikteta wapya” na linajaribu kueleza kwanini watawala wanaojikita juu ya “ubabe” siku hizi wako mbele miongoni mwa wanaotawala duniani.

Watawala wababe si wageni. Historia imekuwa ikikumbana nao tangu enzi za mafirauni wa Misri. Sema siku hizi ni kama wameumbika tena kwa sababu tawala zenye kutambulika kwa ubabe wa viongozi wao zimezagaa kwingi.

Jarida la Foreign Affairs limewataja viongozi kadhaa kuwa ni mifano ya hao wababe. Limeanza na Rais Vladimir Putin wa Urussi, Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki na Rais Xi Jinping wa China, ambaye siku hizi amebandikwa lakabu ya “Mwenyekiti wa Kila Kitu”, kwa vile anasemakana kuwa na madaraka mengi kushinda kiongozi yeyote mwengine wa China tangu Mwenyekiti Mao Zedong.

Nadhani sababu za kiitikadi ndizo zilizolifanya Foreign Affairs liwataje viongozi hao watatu kwa kuwa jarida hilo labda linawaona kuwa ni mahasimu wa Marekani na huenda tawala zao zikawa dhidi ya maslahi ya Marekani. Lakini ukweli ni kuwa viongozi hao watatu si peke yao duniani wenye kutawala kibabe. Kuna Rodrigo Duterte, Rais wa Philippines, kwa mfano.

Vituko vya Duterte vinawashangaza wengi. Nafikiri moja ya sifa za viongozi wababe ni kufanya vituko vya ajabuajabu. Duterte hataki mchezo, anasema, na anaonyesha kuwa tayari kupambana na yoyote anayejaribu kumpinga. Jaji mkuu wa nchi yake, Maria Lourdes Sereno, na hata Rais Barack Obama wa Marekani, wote anawaona kuwa ni mboga. Alithubutu kumtukana Obama kwa kumwita “mtoto wa kahaba”.

Kuna na wengine duniani kama Duterte; na hata barani mwetu watawala wababe wamejaa tele. Mtindo wa kutawala kibabe unaonekana kuwa ndio mtindo wa kisasa wa kutawala. Kila pale Rais anapojilimbikizia madaraka na akazidi kututumka ndipo anapojiona (na anavyotaka aonekane) kuwa ndio mtawala asiyetaka upuuzi, mtawala mwamba, mwenye madaraka yote na nguvu zote.

Huyaona mahakama na majaji kuwa hawafanyi kazi yao wanapowaachia huru washtakiwa kwa kufuata sheria kwa mfano, au wanapokuwa hawatoi hukumu za adhabu kali kama atakavyo yeye.

Bila ya kuijali Katiba na sheria za nchi huviagiza vyombo vya dola viwatumilie nguvu wananchi wanapomuudhi. Hapo ndipo anapotunisha musuli na kujifanya “mbabe wa wababe”.

Hatari iliyopo ni kwamba mtawala wa namna hiyo mara moja hugeuka na kuwa mtawala wa mabavu, wa kidikteta. Huwa dikteta mamboleo. Wagonjwa wa aina hiyo wameenea kwingi duniani.

Jarida la Foreign Affairs linasema kuwa takwimu zinaonyesha kwamba tawala za wababe zimeongezeka duniani, hasa baada ya kumalizika kwa Vita Baridi. Jarida hilo limeandika kwamba “mnamo 1988 tawala za wababe zilikuwa asilimia 23 ya tawala zote za kidikteta. Leo, asilimia 40 ya tawala zote za kimabavu zinatawaliwa na wababe.”

Kinyume na wanavyodhania wenyewe, aghalabu watawala wa kibabe huwa hawana kheri na nchi zao. Mfumo wao wa utawala unapobadilika na kuwa wa kidikteta huwa ni kizingiti kikubwa cha maendeleo kwa kuwa unawakandamiza wananchi kwa kuwanyima na kuziminya haki zao.

Afrika imeonjeshwa zamani shubiri ya utawala wa kibabe. Wakati wa udikteta wake Rais Mobutu Sese Seko wa iliyokuwa Zaire, alikuwa ni mfano mzuri wa madikteta wa Kiafrika wa zama hizo. Alikuwa bahalula, kichekesho, na wakati huohuo alikuwa katili.

Sikujaaliwa kukutana naye ana kwa ana. Nikimuona kwenye picha na televisheni tu. Ulipokuwa nchini mwake, ukitaka usitake, sura yake ukiiona saa zote kwani kila ulipogeuka ikikukodolea macho.

Picha yake ilikuwa kila mahala. Hata magauni ya akina mama yalikuwa na sura ya Mobutu kwenye sehemu ya makalio.

Taarifa za habari kwenye televisheni zikianza kwa kuonyeshwa mawingu na katikati ya mawingu ikichomoza sura ya Mobutu.

Viroja hivyo vilipokuwa vikiendelea, Mobutu alijitajirisha na kujineemesha, yeye na waliokuwa wake. Nchi aliifisidi na kuiangamiza.

Mobutu alikuwa mtawala aliyekubali kutumiwa na ubeberu na aliyeyapenda maisha ya kizungu, raha na buraha zake. Asubuhi, kwa mfano, kabla ya kustaftahi (kufungua kinywa) Mobutu alikuwa na mazoea ya kupiga pegi moja au mbili za wiski.

Akinywa ulevi huo mkavumkavu bila ya kuuzimua. Wakati wa chakula cha usiku akinywa shampeni ya rangi ya waridi aliyokuwa akiiagiza kutoka Ufaransa. Hata maji ya kunywa akiagiza kutoka Ufaransa.

Lakini juu ya ubazungu wake Mobutu huyohuyo 1971 alilibadili jina la nchi yake na aliamrisha iitwe Zaire badala ya Congo.

Kadhalika, alilibadili jina la mji mkuu, Leopoldville, na akalazimisha uitwe Kinshasa.

Baadaye akayaingilia majina ya watu binafsi akianzia na lake la Joseph Mobutu na 1972 ajajiita Mobutu Sese Seko. Aliwaamrisha raia wote nao waache kutumia majina yao ya mwanzo ya Kikristo, ya kizungu, na akawashurutisha watumie majina ya Kiafrika.

“Utawala wa mtu” wa Mobutu ulidumu kwa miaka 31. Kufikia hapo alikuwa chakari; madaraka yalikwishamlevya. Hata hivyo, juu ya udikteta wake, au labda kwa sababu ya udikteta wake, nchi yake ilikuwa na utulivu wa aina yake. Sio kama sasa kusikokwisha mapigano.

Ijapokuwa alikuwa kibaraka wa mataifa ya Magharibi, tena kwa hiyari yake, Mobutu huyohuyo hakuchelea Januari 1967 kuitaifisha kampuni ya madini ya Union Minière du Haut Katanga (UMHK), iliyokuwa sehemu ya shirika la kibiashara la Kibelgiji, Société Générale.

Kazi kubwa ya kampuni hiyo ilikuwa kuchimba shaba na baadaye kobalti, bati na urani. Siku hizi Union Minière inaitwa Umicore N.V. na inajishughulisha zaidi na teknolojia ya usafishaji wa madini yenye thamani kubwa.

Alipoitaifisha kampuni ya UMHK Mobutu pia alinyakua dola za Marekani milioni mia nane ($800m) zilizokuwa mali ya kampuni hiyo. Kadhalika, alitangaza kwamba serikali yake haitowalipa fidia hata ya senti moja wamiliki wa kampuni hiyo.

Alijitetea kwa kuhoji kwamba Wabelgiji waliunyonya utajiri wa nchi yake kwa zaidi ya karne moja. Kwa hivyo, ng’o, hawapati kitu, alisema.

Kwa kuchukua hatua hiyo, Mobutu aliwakuna wazalendo, hususan wasomi. Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Lovanium walipiga mbio wakiviteremka vilima vinavyouzunguka mji wa Kinshasa wakamiminika barabarani wakiandamana na kuimba nyimbo za kumtukuza Mobutu.

Kwa kukataa kulipa fidia, Mobutu alihalifu sheria ya kimataifa. Ubelgiji haikukubali. Ikakimbilia Benki ya Dunia na ikataka misaada yote iliyokuwa ikipewa Zaire isimamishwe mara moja. Benki ya Dunia na wafadhili wote wengine wa Zaire wakairidhia Ubelgiji. Mobutu na Zaire yake wakawa mtegoni.

Mobutu hakuwa na hila. Hatimaye alilazimika kuilipa fidia, ingawa kwa mlango wa nyuma. Alipokuwa akiitaifisha Union Minière Mobutu akitaka kuonyesha kwamba yeye ndiye mwenye nguvu zaidi ya Ubelgiji. Siku alikiamrisha chama chake cha Mouvement Populaire de la Révolution (MPR) kifanye maandamano ya kuwapinga Wabelgji kwenye ubalozi wao.

Wababe wengine wa Afrika hawakuwahi hata kushika hatamu za serikali. Mfano ni Jonas Savimbi aliyekuwa kiongozi wa wapiganaji wa Unita nchini Angola aliyepigana kwa zaidi ya miaka 30 na majeshi ya serikali ya chama cha MPLA.

Nilishuhudia kwa macho yangu 1990 namna Savimbi alivyokuwa akiwachezesha kindumbwendumbwe wafuasi wake nilipozuru kwa wiki moja mji wa Jamba ulio kusini-mashariki mwa Angola na uliokuwa makao makuu ya maeneo yaliyokombolewa na wapiganaji wa Unita.

Savimbi alikuwa hodari, jasiri na alijaaliwa kuwa na haiba kubwa. Ilikuwa haiba ya kutisha. Ingawa aliuliwa na majeshi ya serikali, yakisaidiwa na intelijensia ya Israel Februari 22, 2002, hadi leo malaika hunisimama kila ninapoyakumbuka mazungumzo yetu ya usiku wa manane. Nilichukuliwa usiku mwingi pamoja na waandishi wengine watatu wa kimataifa kwenda kuzungumza naye.

Tulipakiwa kwenye gari la kijeshi kutoka kambi iliyopewa jina la “Kwame Nkrumah” giza zito lilipokuwa kukuu, tukapitishwa vichakani hadi kwenye handaki moja kubwa lililozungushiwa miti na majani mengi. Juu ya handaki kulikuwako wapiganaji wa Unita kila mmoja akibeba bunduki nzito.

Tukateremka ngazi kwenda chini ya ardhi ambako tulikuta chumba kikubwa kilichobandikwa ramani za kivita. Tulimuona Savimbi ameketi kitini, mbele yake pakiwa meza refu na viti tulivyowekewa sisi, wageni. Baadhi ya wakuu wengine wa Unita walisimama nyuma yake.

Baada ya kulahikiana na kupeana mikono nilikuwa wa mwanzo kusema. Nikimuangalia Savimbi nilimwambia: “Kabla hatujaanza ningependa kuuliza kwa sababu alikuwa rafiki yangu, yuko wapi Sangumba?”

Ilikuwa kama nilichokoza sega la nyuki. Savimbi alinyanyua kono lake akapiga ngumi mezani huku akinitolea macho na kunguruma: “Sangumba, Sangumba, Chinguji, Chinguji, kila anayekuja hapa huwauliza.Utamuona (Sangumba) wakati muwafaka!” Kimya kilitanda.

Nikamuuliza tena: “Una maana kwamba yu hai?” “Ndiyo,” akanijibu bila ya kupepesa macho.

Sangumba alikuwa Jorge Sangumba, mmoja wa viongozi wa Unita aliyewahi kuwa mwakilishi wa chama hicho jijini London katika miaka ya 1970 nilipojuana naye.

Chinguji alikuwa Tito Chinguji, aliyewahi kuwa mwakilishi wa Unita jijini Washingon, Marekani. Sikuwahi kukutana naye ingawa sifa zake zilinifika haraka pamoja na tetesi kwamba yeye na Sangumba walikuwa wameuliwa na Savimbi.

Kwa hakika wakati huo Chinguji alikuwa bado hakuuliwa. Alikuwa amewekwa kizuizini tu. Lakini Sangumba alikwishauliwa. Niliyathibitisha mauaji hayo jioni kabla ya Savimbi kunambia kwamba Sangumba alikuwa hai. Nilikutana kwa ghafla na kiongozi mwingine wa Unita niliyemtega kwa swali akakiri kuwa Sangumba alikuwa ameshakufa, ingawa yeye alinambia kwamba alikufa katika mapigano.

Siwezi kwa sasa kuyasimulia yote niliyoyaona Jamba. Lakini nina hakika kwa niliyoyashuhudia kwamba lau angeshika serikali, Savimbi angetawala kibabe.

Kama ilivyo kawaida ya viongozi wababe Savimbi akijiamini laisa kiasi. Akijiona. Na akiamini kwamba akijua kila kitu na kwamba yeye pekee ndiye aliyekuwa Mwafrika halisi. Kibri chake kilikuwa kiasi hicho.

Zaidi ya hayo alikuwa mtu wa kulipiza kisasi, asiyeambilika na aliyekuwa mshirikina, mtu wa kuwasikiliza wachawi na warogaji.

Kwa ufupi, madikteta mamboleo wetu kwa kuudekeza ubabe na kuhusudu “utawala wa mtu mmoja” hujiapiza wenyewe kwa kugeuka mafirauni wa kisasa. Hali huzidi kutisha

wanapotawala kwa niaba ya vyama vya siasa vyenye nguvu na visivyojali kushirikiana nao kuzikiuka sheria.

Share: