Makala/Tahariri

Umeme – Daktari Shein agonge panapoumia

Jabir Idrissa,

NILIPOMSIKIA Dk. Ali Mohamed Shein akijiapiza kuwa atakuwa tayari kuiona Zanzibar watu wake wanawasha vibatari – badala ya umeme – iwapo itakatiwa umeme na Tanzania Bara, haraka akili yangu ilifikiria kumbukumbu za Baraza la Wawakilishi za vikao vya mwaka 2012.
Katika mwaka huo, wajumbe wa baraza hilo walijipa muda kujadili tatizo la umeme linalochangiwa na mzigo mkubwa wa deni linalotokana na umeme wa Tanesco, na kuhusisha na ufisadi ndani ya shirika lake la ZECO – Zanzibar Electricity Corporation – hata kulazimika kuundwa kamati mahsusi ya kuchunguza.

Kulikuwa na tuhuma za ufisadi zilizotupiwa shirika lenyewe la Zeco, ikielezwa kuwa wapo watumishi wasiokuwa waaminifu wanashirikiana na baadhi ya watumiaji wakubwa wa umeme, wakiliibia shirika na kulipunguzia uwezo wa kutoa huduma nzuri kwa wateja wake.
Zanzibar, hususan kisiwa chote cha Unguja, hutumia umeme unaotokana na miundombinu inayotunzwa na kuhudmiwa na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).

Umeme huo hufikishwa Zanzibar kwa njia ya waya zilizochimbiwa baharini kutokea eneo la Ras Kilomoni, maeneo ya Kunduchi, nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam, ukitokea kituo kikuu cha Ubungo na kupokelewa kwenye kituo kikuu cha Fumba, magharibi mwa Zanzibar.
Historia inaonesha uwekezaji uliofanywa wa kufanikisha kuwekwa kwa waya hizo kutoka Dar es Salaam mpaka Fumba na hatimaye kituo kikuu cha usambazaji cha Mtoni Kidatu, mjini Zanzibar, uligharamiwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa sehemu kubwa kutokana na msaada wa serikali ya Norway.

Lakini baada ya miundombinu hiyo iliyojengwa miaka ya 1980, kuchakaa, Zanzibar ilipata msaada wa Serikali ya Marekani kupitia mradi uliofadhiliwa na Mfuko wa Millenium Challenge (MCC) mwaka juzi. Utekelezaji wa mradi huo uliwezesha kutandikwa waya mpya kutokea Ras Kilomoni hadi Fumba, na hatimaye kukamilisha usafirishaji umeme huo mkubwa kwenye kituo kikuu cha Mtoni Kidatu.

Ndani ya Baraza la Wawakilishi, baada ya Hija Hassan Hija, aliyekuwa mjumbe kupitia Chama cha Wananchi (CUF), kuwasilisha hoja binafsi ya kutaka baraza liunde kamati teule ya kuchunguza tuhuma za ufisadi Zeco, wawakilishi waliridhia uchunguzi ufanyike.
Lakini, mwishowe, uchunguzi ulifanywa kwa kutumia Kamati ya Kudumu ya Baraza ya Hesabu za Serikali na Mashirika ya Umma. Baraza liliridhia majibu ya serikali kwamba kamati hiyo ichunguze bali kwa kumjumuisha Hija katika uchunguzi.

Kamati ilikamilisha uchunguzi na kuwasilisha ripoti yake barazani. Ilitoa mapendekezo kadhaa, miongoni yakiwa kuchukuwa hatua za kinidhamu na kisheria kwa wale waliotajwa kushiriki ufisadi ndani ya Zeco. Likawepo pia pendekezo la kuchunguzwa uhalisia wa deni la Tanesco kwa Zeco na kufuatilia mazungumzo ya kiutawala kati ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Serikali ya Muungano.

Ni katika pendekezo hilo linalohusu deni la umema ambao Zeco inauziwa na Tanesco, ilionekana kuwa deni hilo limekuwa likikua huku likilimbikizwa. Pia ilionekana Zeco inanunua umeme kwa bei ya juu hata kuliko namna Tanesco inavyouza umeme kwa taasisi mbalimbali za ndani ya Tanzania Bara. Ilielezwa kuwa Zeco inanunua uniti kwa Sh. 210 wakati Tanesco inauza umeme kwa wateja walioko Tanzania Bara kwa uniti Sh. 118.

Kamati ya uchunguzi ya Baraza la Wawakilishi ilieleza kuwa tofauti hiyo ya bei ya umeme inamaana kuwa ukichukua gharama za umeme pekee, ni wazi wafanyabiashara wanaowekeza watakimbilia kufungua miradi yao Bara kuliko Zanzibar. Hapo panajenga picha kuwa Zanzibar inanyongwa kiuchumi.

Eneo hili hasa la Zanzibar kuzibiwa fursa ya miradi ya kiuchumi, ndilo ninalolenga lieleweke kwa Dk. Shein wakati anaposhikilia hatamu za uongozi ndani ya tuhuma za kuwezeshwa tu na vyombo vya dola, ilhali inajulikana Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilishindwa uchaguzi mkuu wa 25 Oktoba 2015.

Dk. Shein kwanza ninaamini amejikusuru tu kutamka kuwa Zanzibar itawasha vibatari kwa sababu, ninajua fika si nyumbani kwake kutakowashwa nishati hiyo ya kinyonge, isipokuwa kwa wananchi wanaojihudumia kimaisha. Ubaya ni kwamba wananchi hao wanyonge ndio wanaomhudumia yeye kwa kila kitu anapoishikilia Ikulu bila ya ridhaa yao.

Shida nyingine kwa Dk. Shein ni kwamba anajua fika deni la umeme ni la siku nyingi. Amekuwa kiongozi wa ngazi ya juu ndani ya CCM na serikali zote mbili, lakini alitoa mchango gani kumaliza tatizo hilo? Alikuwa Makamu wa Rais tangu Julai 2002 baada ya kifo cha Dk. Omar Ali Juma. Akaendelea baada ya uchaguzi mkuu wa 2005 hadi alipopelekwa kugombea urais Zanzibar mwaka 2010.

Katika muda wote huo alikuwa mjumbe wa Baraza la Mawaziri la Serikali ya Muungano, mbali na kuingia katika vikao vyote vya juu vya CCM ikianzia na Kamati Kuu na kuishia Mkutano Mkuu, alisaidia vipi kuishawishi “Serikali baba” ya Muungano kufuta deni au kuliwezesha kulipwa kwa utaratibu endelevu unaozuia kukua kwake kwa kasi?

Hii hali ya kukua kwa deni la Tanesco kwa Zeco, mashirika mawili yenye uchumi usiofananika kwa hali yoyote ile, tena ikiwa ndani ya manung’uniko ya Zeco ya kuuziwa umeme kwa bei kubwa kuliko wateja wengine wa kitaasisi, na ikijulikana kuwa uchumi wa Zanzibar kama nchi ni kiduchu usiostahili kushindanishwa kwa namna yoyote ile na Tanzania Bara, inathibitisha kuwa kero kuhusu uendeshaji wa muungano inaendelea kuitafuna Zanzibar.

Kero hiyo ya Tanesco kuiuzia Zanzibar umeme kwa bei kubwa huku Dk. Shein akishuhudia viongozi wenzake wa CCM wanavyoshikilia kuidhoofisha Zanzibar kiuchumi kutokana na sera mbalimbali za kimuungano, ni donda lisilopona hasa kwa sababu hakuna dawa iliyopendekezwa ndani ya Katiba inayopendekezwa ambayo wao CCM waliipitisha kwa shangwe kubwa.

Si haki na wala si uwajibikaji wa kueleweka, pale Dk. Shein anapotoa kauli ya kuhiari Zanzibar izimiwe umeme na Tanesco ya Tanzania Bara akiwa tayari kuwa wananchi wa Zanzibar watawasha vbatari wakati akijua si yeye atakayeishi kwa nishati hiyo ya kinyonge.

Dk. Shein angesema ukweli uliopo. Angejilaumu kwa kuongoza ndani ya kero zisizopatiwa ufumbuzi maisha, tena akawatupia lawama viongozi wenzake wa CCM kwa kutoipatia Zanzibar haki kulingana na ushirika wake katika Muungano ulioasisiwa 26 Aprili 1964.

Hivi leo kada huyu wa CCM anajua Serikali ya Muungano ikiamua inaamua. Iliizimia Zanzibar umeme kwa siku kadhaa mwaka 2003. Mara ya pili umeme ulikosekana Zanzibar kwa miezi mitatu mwaka 2011. Daktari yupo uongozini.

Kwa kuwa suala hilo limebainishwa na Baraza la Wawakilishi kama sehemu ya kero kubwa za Muungano wa Tanzania, ambao Zanzibar ni mshirika mmojawapo pamoja na Tanganyika, lakini Dk. Shein hajajielekeza na jitihada za kutatua hilo, basi hajaonesha mapenzi ya kweli kwa Wazanzibari.

Tagsslider
Share: