Unajua ni kitu gani kilichopelekea Wagombea wengi c.c.m Zanz
Written by ole // 08/07/2010 // Makala/Tahariri // 1 Comment
Na.B.ole,
Wana C.C.M Zanzibar wamefurahi sana juu ya mchakato mzima wa kumpata mgombea wa urais kupitia chama chao.
Wengi wao ukiwauliza utapata jibu kwamba hiyo ndio demokrasia na kuvitaka vyama vyengine vifuate mwenendo huo wa chama kikongwe cha siasa Zanzibar.
Sio vibaya kwa wanachama kujenga imani hiyo juu ya chama chao lakini kwa wale Wazanzibar walio wengi na wanaoifaham C.C.M basi hili kwao itakuwa ni sawa na kutia maji pakachani kwani ni dhahiri kwamba hayatofika nyumbani na kutumika bali utaishia na pakacha lako tupu bila chochote.
Ukweli ni kwamba C.C.M Zanzibar wamejengeka na mazoea ya kuamini kwamba yeyote yule ambae atachaguliwa au kupitishwa kule Tanganyika kama mgombea wa chama hicho ndio huyo anaehesabika kuwa tayari ndie rais.
Huu uchaguzi wa kuwashirikisha vyama vyengine huwa kama danganya toto lakini mikakati tayari huwa imeshaandaliwa kwa vyovyote vile hata kama nusu ya Wazanzibar watauwawa hio sio shida kwao ilimradi mtu wao atawale Zanzibar.
Wazanzibar hawana budi kuelewa siri nzito juu ya hili, kwanini Tanganyika hawataki kuona Mzanzibar halisi anaongoza Zanzibar ? Jibu lake nitawapeni hapo baadae kwa nini hili hawalitaki.
Historia inaonesha kwamba C.C.M Zanzibar mpaka hii leo bado wanaona kwamba chama ambacho kinastahiki kuwepo madarakani ni wao tu, hata kama Wazanzibar walio wengi hawaungi mkono.
Ndio maana katika suala la urais likagawa makundi ya wagombea na kufikia pahala kila mmoja akawa hamuamini mwenzake, hivi ndivyo sura ya chama Tawala ilivyo.
Pia kwa wagombea wengine hii itakuwa ni pata potea kwani ikiwa majina yao hayakupitishwa kule Machinjioni Dodoma wanaelewa dhahiri kwamba huo ndio utakao kuwa mwisho wao kisiasa kilichobaki wasubiri upepo utakapoelekea.
Kwa wale wana c.c.m Wanaodai kwamba kujitokeza kwa wagombea wengi ni demokrasia, nahisi wamehafilika au wanajidanganya nafsi zao, kwani tayari kati ya hao hao wagombea, kibao cha chuki na ubaguzi kimeshawakumba, demokrasia ya kuwabagua tayari imeshajitokeza wazi wazi mpaka kufikia wengine kumuandikia Mwenyekiti wa Chama chao basi ujue kisu kimeshagonga mfupa na nyasi zimeshashika moto.
Kama munakumbuka Wazalendo wenzangu nilizungumzia juu hali kuwa sio shuari ndani ya chama Tawala, lakini wanao dai kwamba wanaumwa sana wakalalama ,na kufika hata kutoa kashfa, lakini hatuna budi kuelewa kwamba hii ndio demokrasia ya c.c.m. na wafuasi wake.
Pia kuna wengine tayari wameshaanza kutaka kudai A.S.P yao, sasa kama ni suala la demokrasia haya yote yanakuja vipi tena ?
Wazanzibar eleweni kwamba Mgombea kupitia chama tawala hivi sasa, imani yake imejengeka kwamba atatawala Zanzibar japo kama hakuchaguliwa na Wazanzibar kwani hii ndio mbinu yao siku zote na mara hii mujuwe kwamba kuna ajenda nzito tayari imeshaandaliwa na Tanganyika zidi ya Zanzibar.
Wazanzibar muelewe vile vile kwamba Tanganyika siku zote hawezi kufanya kosa kwa kumchagua Mzanzibar halisi kuwa Rais wa Zanzibar abadan.
Kwa maana hiyo atakae pitishwa lazima awe ni mtu mwenye asili ya Bara au Mzanzibar ambae atashiriki kwa asilimia mia moja kuwafitinisha Wazanzibar wenzake na mwisho wake kuimaliza Zanzibar kwa kuifanya kuwa ni mkoa wa Tanganyika.
Sote tunajua kwamba Shein ndie atakae pitishwa kwenye kinyanganyiro hicho, hizi ni habari za ndani kabisa na Bilal ataahidiwa na yeye kupewa fupa ili hizi kelele za kisonge zipunguwe na Wazanzibar waone kama C.C.M Bara wamejali kilio chao jambo ambalo litakuwa ni pigo kubwa kwa Wazanzibar walio wengi.
Wale ndugu zetu wa Kipemba wao watafanyiwa dhihaka kwa kuambiwa siku zote nyinyi mulikuwa munagombania nafasi hii, kwa vile c.c.m ni chama cha demokrasia basi mara hii tumekuleteeni Mpemba mwenzenu mumchaguwe.
Shein akishapata basa atakuja wambia Wazanzibar kwamba kwao yeye ni Bagamoyo na jina lake la huko ni mkwawa.
Kumbukeni Mzee ruhusa alikuwa Mzanzibar halisi pale alipotaka Wazanzibar wamchague lakini alipokwisha pata alikuja uwanja wa Aman ni kuwambia Wazanzibar kwamba yeye ni mkisarawe.
Kumbukeni kwamba hawa wote hakuna hata mmoja ambae anajali Maridhiano kinachofanyika hapa C.C.M ni usanii wa kisiasa tu, kutaka kuonesha kwa Jumuiya za Kimataifa kwamba wao wanajali demokrasia na pale wapinzani watakapo kuja kulalamika waweze kujitetea kwamba hawa siku zote wao kazi yao ni kulalamika.
Kilio cha Mzanzibar halisi hakiwezi kusikilizwa hapa na pia nawahakikishieni kwamba endapo itatokea mara hii Wazanzibar kubwebweteka na kulalia maridhiano bila ngangari basi c.c.m wakitawala tena hii hali iliopo hivi sasa itazidi mara kumi na Zanzibar itarejea kule alikotuanzisha Salmin na Bilal.
Zanzibar tayari imeshaanza kuliliwa na bundi nasema hii sio dalili nzuri kwa Wazanzibar wanaopigania ukombozi wa Zanzibar.
Inshallah tukipata nafasi tutawaleteeni mpango kabambe ulionaswa juu ya jinsi gani mara hii Wazanzibar watakapo pigwa chenga ya mwili na chama tawala, nakupata tena kipigo cha paka mwizi, data tumeshazipata.







One Comment on "Unajua ni kitu gani kilichopelekea Wagombea wengi c.c.m Zanz"
B.Ole tuleteee tu huo mpango kabambe unaoujua. Lakini usiwe kama wagombea wa CCM kualikana shughuli halafu ukaingia mitini.