Viongozi wa Serikali ya Mapinduzi hawajiamini .

Written by  //  07/09/2010  //  Makala/Tahariri  //  4 Comments

Na.B.OLE,

Napenda nijenge hoja kuhusu viongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwamba ni woga na hawana msimamo wowote madhubuti katika kuwatetea Wazanzibar na Taifa kwa ujumla.

Na hii ndio sababu inayotufanya wananchi kuzama kwenye dimbwi zito na majanga makubwa ambayo hayana ufumbuzi muafaka, kuepukana na kadhia hii.

Viongozi wetu wapo kwa ajili ya maslahi yao binafsi tu, lakini linapokuja suala lenye maslahi ya nchi na Wananchi basi wao hawasimami kama ni viongozi waliochaguliwa kwa ridhaa za wananchi na wenye uchungu wa maendeleo ya Zanzibar.

Haya yanaonekana dhahiri hayataki mjadala, kwani wao kwa njia moja ama nyengine ndio waliotufikisha hapa tulipo. Kama hilo halitoshi, Viongozi hawa ndio wanaowapandikiza baadhi ya Wananchi kasumba mbaya ili wao wabakie kwenye kufaidi madaraka katika uhai wao wote, jambo ambalo sio sahihi kwani uongozi ni dhamana na si mali ya mtu binafsi wala chama fulani.

Tuangalieni mfano mmoja wa haraka haraka , pale ulipokuja mjadala wa mafuta na suala la Maridhiano viongozi wa Serikali ya Mapinduzi walivyoyapokea masuala yale.

Ukimuachia Rais na japo lake la viongozi wachache, waliobakia wote walikuwa woga kiasi ambacho walikuwa wanatazamana machoni kila mmoja anaangalia ni nani atamfunga paka kengele.

Kwani wao kwenda kinyume na Wafalme wao Tanganyika kwa jambo lenye maslahi kwetu ni kosa kubwa licha ya kwamba masuala yote mawili ni muhimu kwa Wananchi na Taifa kwa ujumla, lakini kutokana na kasumba za kutojiamini basi wanaona bora wakae kimya au atoke nje ya Ukumbi, ili asije akaambiwa na yeye alikuwepo katika mjadala ule.

Sio kweli kwamba hawaelewi kwamba Nchi yetu ina matatizo na wao tumewapa uwezo na zamana ya kutuongoza na kututatulia shida zetu pale panapohitajika maamuzi yao.

Viongozi hawa wana uweledi mzuri tu kwamba Tanganyika wanatunyonya na kutuburuza lakini kutokana na woga na kutojiamini kiutendaji huku maslahi yao wakiyaweka mbele basi hushindwa kuwatetea Wazanzibar.

Wanachohofia viongozi wetu ni kukosa kujaza matumbo yao pindipo kwamba wataitetea Zanzibar kudai haki zake za kimsingi, basi kuna uwezekano mkubwa kwa wao kupoteza nyadhifa zao, kwa maana hiyo itakavyokuwa vyovyote vile lazima wakubali ili wasing’atuke kwenye madaraka. Hawa ndio viongozi wetu walivyo hata kama kufanya hivyo ni kuwasaliti Wazanzibar walio wachagua.

Sote tulishuhudia wakati Mh. Abuu Bakari alipowaslisha hoja binafsi pale katika baraza,baadhi ya Wawakilishi wetu na Mawaziri wa Serikali, walikaa kimya kama vile kile kinachozungumzwa na kujadiliwa hakina maslahi na wao wala Taifa, kwa kuhofia tu ikiwa atachangia basi ataonekana anashirikiana na wapinzani, kwa maana hiyo uwezo wa kuhatarisha nafasi yake ni mkubwa.

Viongozi hawa hawa, baadhi yao walipita kwenye majimbo yao kuwashawishi watu waikatae kura ya maoni kwa kutia Hapana, kwani wengi wao wanahisi kwamba katika Serikali inayokuja watapoteza nafasi zao .

Naamini ndani ya Serikali ya Mapinduzi kuna baadhi ya viongozi ni Wazuri na wanaumwa na maendeleo ya Zanzibar lakini kutojiamini kwao ndio sababu tosha inayoifanya Zanzibar kuzidi kudidimia kisiasa na kiuchumi.

Viongozi hawa husubiri mpaka Madaraka yakiwatoka ndio utamkuta mtu anaanza kutoa uoza wa Serikali kwamba yeye alihusika na kuharibu matokeo au alitumiliwa kwa njia moja ama nyengine sababu ambazo ni za kijinga na upuuzi mtupu kuwaeleza Wananchi.

Kiongozi huyu huyu hakuyapinga maovu ulipokuwepo madarakani anasubiri mpaka leo hii ndio anajitokeza amekuwa si ndege wala mnyama hakubaliki popote, sasa tukufahamu vipi wakati wewe ulikuwa adui wa Zanzibar tukuweke kwenye kundi gani ? Kwani nini hukupinga kama walivyofanya wengine walio kuwa na uchungu na Zanzibar ?

Wazanzibar uchaguzi umeshatufikia, naamini kwa walio wengi wanajua kura yao wampe nani na chama gani lakini pia kupeana nasaha sio vibaya. Ni lazima tuwaelewe viongozi wababaishaji wanaohisi kuweko madarakani siku zote ni haki yao na watu wengine hawana maana na wala sifa za kuwa viongozi Zanzibar.

Wengine huleta viroja kwa kuwambia kwamba wao wanasifa 100% za kuwa viongozi wakubwa na wao wataondosha umaskini kwani Zanzibar umaskini umekua kama ni maumbile ya Wazanzibar kwa sasa wamezaliwa nao na watakufa nao.

Viongozi hawa wanasahau kwamba, wao wamo kwenye madaraka makubwa katika Serikali hawayaoni matatizo yetu mpaka hii leo ndio wanajifanya wema na bashasha kwa Wazanzibar ili tuwape kura zetu wazidi kutumaliza, wazalendo hapa tuwe makini na ufisadi wa viongozi wa aina hii.

Mimi naamini kwamba uchaguzi huu utakuwa ni wa upande mmoja tu, ule ambao una malengo ya kusimamia haki na kutoa mwanga na nuru ya maendeleo kwa Zanzibar, viongozi hao ndio watakaokuwa chaguo la Wazanzibar.

4 Comments on "Viongozi wa Serikali ya Mapinduzi hawajiamini ."

  1. Zdaima 07/09/2010 kwa 1:26 um ·

    Sadakta bwana B. Ole

    Mawazo yako mazuri ,kuhusu viongozi gani wa kuwachagua ktk uchaguzi. Lakini mm naomba watu wasiingize ukereketwa wa chama . Tuwe na vigezo muhimu kwa mfano .Uwezo wa kujenga hoja na kujiamini ,mwenye uchungu na zanzibar Kwa vitendo tuangalie historia zao . Kawafanyia nini wazanzibari ktk mustakbali wa umoja na mshikamano wao kwa wale waliokuweko madarakani{maridhiano kwa sasa iwe ajenda},uwezo wa elimu,Wenye sera za utayari kuiondolea Vikwazo Zanzibar Katika muungano{muhimu hii}.Historia nzuri katika utumishi wao wa umma{wasiwe walafi,walarushwa,wachochezi,wabaguzi n.k}.Hivi viwe vigezo vya mtu binafsi

    Kwa upande wa vyama angalau tuangalie hivi.Sera za usawa kwa rasilimali za umma,Sera zinazolenga kuondoa matatizo ya mda mrefu kwa wazanzibari{manunguniko juu ya muungano,Ukiritimba katika kupata huduma za kijamii,maendeleo duni ya kijamii,malumbano na uhasama wa kisiasa,n.k}
    Sambamba na hayo tuangalie Uwezo wa kimkakati wa chama husika na utashi wa Viongozi wao wa juu wa Chama katika kupata zanzibar Mpya yenye maendeleo.

    Viongozi hawa tuwaweke ktk mezani na tuwapime uwezo wao kwa dhati ya nafsi zetu .Nina hakika tutawabaini wenye uwezo huo na wasiokuwa na uwezo huo.

    Ramadhan kareem

  2. sale 07/09/2010 kwa 3:33 um ·

    Unayosema ni kweli
    Mimi nimefahamu hakuna kiongozi yoyote aliekaa kwa maslahi ya zanzibar bali ni maslahi yake mwenyewe tu,,
    Hivi kweli iamuliwe hakutokuwa na mshahara tofauti na wafanyakazi wengine, hakutonunuliwa magari, hakutokuwa na marupu rupu ya kijinga kwa wawakilishi, unadhani atatokea mtu kugombea nafasi hizo?
    Hao wote wamekaa kwa maslahi yao wenyewe, ingelikuwa wamekaa kwa ajili ya zanzibar, tungekuwa tuko mbali wala hatuburuzwi na Tanganyika na muungano wao ungekuwa mwisho Chumbe…
    Mimi juna langu Saleh Abdullatif Ahmed Momahammed Haji Mjimbini

  3. Mjomba 08/09/2010 kwa 2:22 um ·

    B.Ole, siandiki kwa makusudi ya kuwatete vingozi wa ccm kwa kuto ikataa dhuluma,lakini nakusudia kuwapunguzia mzigo wa lawama ulio watwisha. Vivyo hivyo, nakusudia kuwa vuua baadhi yao katika lawama hizo.

    Nianze kwa kusema kwamba sisi sote ni bin-adam wakawaida na sio wale mitume na masahaba ambao waliweza kutoa maamuzi yao kwa kupata maelekezo “sahihi” kutoka kwa mola.

    Mimi pengine na wewe (B.Ole) na wengineo tulikuwemo katika hudma za Umma japo si nafasi kubwa kama baraza la wakilishi na bunge.Vivyo hivyo kesho na kesho kutwa baadhi yetu pia watakuwemo katika nafasi kama hizo. Inapo kuja suali la maamuzi,utetezi na hata kuunga mkono jambo fulani hua tunakabiliwa na mtihani mkubwa, si bungeni,si barazani si barabarani na hata majumbani hoja yangu itabakia pale pale,kwamba ni mtihani.
    Tuchukulie mfano;
    pale yalipofanyika maandamano kule Pemba na watu kupoteza maisha. Wito ulitolewa wa maandamano,lakini kila mtu aliamua vyake.

    Matokeo ya namna hiyo katika maisha ya bin Adam ni mengi sana,mimi nilijiuliza nlipotolewa kazini: ivi, wawakilishi na wabunge wanafanya kazi gani wasipinge kitendo hicho mpaka tungerudishwa. Wengine wangejiuliza, mara tatu tuliambiwa cuf imeshinda chaguzi, kwa nini tusinge andamana mpaka kieleweke (chambelecho wenyewe), na kadhalika.
    Naomba, hapa tukubaliane tu kwamba katika sulai la kuamua hapakosi kuepo harufu ya maslahi binafsi na kutafautiana na u-binafsi.

    Maslahi binafsi sio pekee yanayo tuongoza katika kufikia maamuzi,kuana vitu vyengine vya kuangalia kama mazingira,wakati muafaka nk.Kama hivyo ndivyo ccm tunao walaumu leo si lazima wawe woga au wa-binafsi, lakini ni kitu chengine. Hata maalim Seif na Karume tunwaitao mashujaa leo, wakati fulani tunge au tutawaita woga au wa-binafsi.
    Ivi niulize suali, nijambo gani ambalo watu wote wakijiamini lingeshindikana lakini lini watu wote watajiamini kwa pamoja
    jee tuseme katika kujiamini mtu hapaswi kufikiria cosequences?

    Wajumbe wa baraza la wawakilishi na wanachama wa ccm na hasa wakereketwa, bado ni mapema kwa wao kufahamu na kuamini falsafa hii ya umoja wa kitaifa, bado wapo wanao hofia kua huu ni mtego tu kwani mambo ni kangaja hwenda yakaja.
    Nadhani wapo wanao stahili lawama lakini kunawengine bora tuwahurumie, wakielimishwa Zanzibar tutaweza kuzalisha watetezi wazuri tena kutoka CCM

  4. kocha 08/09/2010 kwa 3:07 um ·

    mimi naona nikukosa uzalendo kwa baadhi yao wazalendo wakweli walijitoa muhanga wengine wakatiwa jela wao wakiwakebehi nawengine ndio leo wanasema eti mimi nilishiriki kuzuwia wanafuzi kutoka pemba wasipige kura ovyo.

Comments are now closed for this article.