Wapemba, Waunguja na karata yao ya mwisho.
Written by ole // 28/07/2010 // Makala/Tahariri // 1 Comment
Na.B.OLE,
Wapemba na Waunguja watafanya kosa jengine la pili, ambalo watalijutia maishani mwao, pindipo wataikataa kura ya maoni hapo tarehe 31 july.
Kosa la mwanzo ambalo ni lile la kuhadaliwa kwa Muasisi wetu wa Taifa la Zanzibar na Julius Nyerere na kulazimishwa Muungano ambao leo hii ndio kiini na chanzo cha matatizo ya Zanzibar.
Wazanzibar wote hawana budi kuelewa kwamba hii ndio karata yao ya mwisho na nafasi pekee ya kuikoa nchi yao kwenye midomo ya chewa, kinyume na hapo ni kusema Zanzibar bye bye.
Naamini siku zote majuto huwa ni mjukuu,Wazanzibar kuna haja ya kukumbuka kwamba ikiwa tutashindwa kuamua mustakabali wa Taifa letu basi tusije kutafuta mchawi wetu, kwani Wachawi tutakuwa ni Wazanzibar wenyewe.
Wananchi wengi wanamlaumu Hayati Abeid Karume kwa kuwaingiza kwenye janga hili la Muungano. Ni kweli makosa yalifanyika lakini kufanya kosa sio kosa bali kosa ni kurudia tena kosa.
Tuelewe kwamba Mh. Karume alikuwa pekee yake katika maamuzi hayo ,lakini leo hii wanao takiwa kufanya maamuzi ni Wazanzibar wote.Sasa kama tukipinga nani tutakuja kumlaumu hapo baadae . Jee huu si utakuwa ujuha na upumbavu wa mwisho kwa Wazanzibar ?
Leo hii Wazanzibar wakiipinga nafasi hii azim basi hakuna wa kumlaumu tena ,kwani bahati tumeipata lakini tutakuwa tumeshindwa kuitumia.
Hatuna budi kuwacha tofauti zetu ili tuweze kuwa kitu kimoja kuondoa huu ukiritimba na udhalimu wa kutawaliwa jambo ambalo ndilo linaloleta mifarakano miongoni mwa jamii ya Kizanzibar.
Sote tunapenda mazuri na hakuna hata mmoja anaependa kuishi kwa kubahatisha kila siku, kama wazanzibar walivyo leo hii.
Lazima tushikamane pamoja ili tuwashinde nguvu maadui zetu.Ukombozi wa Zanzibar utaletwa na Wazanzibar wenyewe na sio wageni.
Naamini kuna watu watakufa kihoro pale watakapowaona Wazanzibar sasa wamekaa pamoja na kushirikiana kujenga nchi yao.
Wazanzibar wote ni ndugu, kugombana na kubaguana ni jambo la aibu na wala halikubaliki katika jamii iliostaarabika kama Zanzibar.
Wote wale ambao hawapendi maendeleo ya Zanzibar hawana budi kuelewa kwamba sasa wakati umefika na mageuzi yanayokuja yataifikisha Zanzibar katika hatua mpya na nzuri kimaendeleo, hawana budi kujiunga na wenzao katika kuinusuru Zanzibar yetu.
Ushauri wangu kwa wote wanaopinga Serikali ya Umoja wa kitaifa Zanzibar, waelewe wazi wazi kwamba Wazanzibar walio wengi leo hii hawako tayari kurudishwa kule tuliko toka, hivi sasa tunahitaji kuishi kama binaadam kwa amani na utulivu kwenye visiwa vyetu.
Hivi ni visiwa vyetu, tuna haki ya kujitawala wenyewe na kama kuna watu wapendi basi hao sio Wazanzibar, kwani Wazanzibar hawana sifa na hulka hizo.
Tumechoka kugombanishwa na mafisadi ambao hawana ihsani, fadhila wala shukurani, wamekuja Zanzibar wakapokewa, wakasomeshwa na leo hii ndio wanachukua nafasi hii kuwafarakanisha Wazanzibar, au hizi ndio fadhila na shukrani zao kwa wenyeji ?.
Huu ni ushenzi usiomithilika na hauna tena nafasi katika jamii yetu. Hivi sasa tunasonga mbele kuhakikisha Zanzibar inarudisha tena hadhi yake, ule wakati wa kuogopana na kuoneana haya sasa umeshapitiwa na wakati.
Kama wako watakaochukiwa kwa Wazanzibar kupatana na kuishi kwa vizuri, umoja na udugu wao wa asili, hawana budi kujielewa kwamba laana za muumba zimeshawashukia.
Tuko tayari kupigania nchi yetu kwa bei yeyote ile, lengo na madhumuni ni kumuona Mzanzibar anaishi kama binaadam mwengine bila matatizo yeyote yale.
Sio haramu wala kosa la jinai kwa Wazanzibar kudai nchi yao, hii ni wajibu na haki yao na hawana budi kushinda vita hii, ili kulikwamua dola na Taifa la Zanzibar ambalo mapapa wamelikodolea macho.
Mambo mengine yanatia uchungu, katu Wazanzibar tusirudi nyuma katika jitihada za kuigombania nchi yetu, kwani ni haki yetu kufanya hivyo na kama tukiiwachia basi lawama nyingi zitatuandama sio hapa duniani tu bali hata mbele ya muumba.
Kwani lazima kiumbe anaejitambua,apiganie haki yake hata kwa ncha ya upanga ikibidi kufanya hivyo, huo ndio uzalendo na uchungu wa kile kilicho kuwa chako.
Narudia tena, kwa uwezo wa mola hakuna mtu yeyote atazuia ukombozi wa Wazanzibar, wakati umefika hawana budi wale mafisadi kusalimu amri na kuwapisha Wazanzibar wenyewe wakae pamoja, kushirikiana na kuongoza nchi yao kwa aman ,ili Wazanzibar wanufaike na nchi yao kimaendeleo.
SOTE TUTAPIGA NDIO 31 JULY.







One Comment on "Wapemba, Waunguja na karata yao ya mwisho."
bustani hupendeza sana ikiwa na rangi za maua mbali mbali, na maua yanaponawiri basi ujue yule mpandaji ni hodari sana wakushughulikia ile mimea kwa kutilia maji kila siku, mbolea, kung’owa majani ili kuyapa nafasi yale maua yajifarague nasio magugu. kuwepo waunguja, wapemba, wahindi, wabara, wazungu n.k nikatika sifa za uumbaji, kwani m/mungu ni tajiri na ni hodari wakuumba, hakosi spea katika kazi yake na kila kitu ni perfect,sisi kama binaadamu nilazima tu- appriciate kile tulichobarikiwa, watu rangi mbali mbali, dini mbali mbali, mapishi tofaouti, sikukuu tofauti sherehe za harusi tofauti na maziko vile vile na hivyo ndivo ncchi inaponawiri na kupendeza,ikiwa tuta heshimiana. laa ikiwa wewe sikupendi umeumbwa kwa moto, au mimi nimetengenezwa kwa dhahabu, au wewe unaishi mwezini na huna nafasi duniani……yote ni mambo ya zamani tu kwanini hatusomi kama sote tumeumbwa na mmoja na kuwacha tofauti zetu .jana katawala Muunguja leo mwache atawale Mpemba, tuangalie wapi M/mungu anatuelekeza, haina haja ya kuuza nchi yetu kwasababu ya shetani bora tumlanini, tushikamaneni kama wenzetu wengine, na kupiga kura ya ndio kwa maslahi yetu?