Barazani

Ukawa katika misukosuko

Dodoma/Dar es Salaam.
Friday, July 1, 2016
Bunge la Jamhuri ya Muungano jana lilimalizika kwa wabunge wa vyama vya upinzani kutoka ukumbini kwa staili waliyosema inaonyesha “kifo cha demokrasia”, huku wenzao watatu zaidi wakiadhibiwa kwa makosa tofauti na mwingine, Tundu Lissu akipambana na serikali mahakamani jijini Dar es Salaam.

Wafuasi watatu, ambao walienda Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Kisutu kushuhudia kesi ya Lissu na ambao walikuwa wamebeba mabango yenye maneno “uchwara” na “dikteta”, walijikuta wakikamatwa na kupelekwa Kituo Kikuu cha Polisi jijini Dar es Salaam.

Faraja pekee kwao jana ilikuwa ni ushindi wa mbunge wa Jimbo la Ndanda, mkoani Lindi, Cecil Mwambe (Chadema), ambaye ushindi wake ulipingwa mahakamani na mgombea wa CCM, Mariam Kasembe.

Ushindi wa Mwambe umekuja siku moja baada ya Mahakama Kuu kutoa hukumu iliyomuangusha Onesmo Ole Nangole (Chadema) wa Jimbo la Longido, ikiwa ni hukumu ya kwanza kubatilisha matokeo ya ubunge uliotokana na Uchaguzi Mkuu wa 2015.

Jana mjini Dodoma, Naibu Spika Dk Tulia Ackson alitangaza kuwasimamisha kuhudhuria vikao wabunge wengine watatu na kufanya idadi ya wawakilishi hao wa wananchi walioadhibiwa hadi sasa kufikia 12, ikiwa ni rekodi katika historia ya bunge hilo kwa kikao kimoja kuadhibu idadi hiyo ya wabunge.

Walioadhibiwa jana ni Mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi aliyesimamishwa vikao 10 kwa kudharau mamlaka ya Spika na kuonyesha ishara ya kusimamisha kidole cha kati na vingine kuvikunja, iliyotafsiriwa kuwa ni matusi.

Wabunge wengine waliosimamishwa kuhudhuria vikao vitano kuanzia jana kwa kusema uongo bungeni ni Saed Kubenea (Ubungo) na James Ole Millya wa Simanjiro.

Mwenyekiti wa Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, Kapteni George Mkuchika alisema Mbilinyi alitiwa hatiani baada ya kuonyesha alama ya kidole cha kati cha mkono wa kulia kilichogeukia juu huku vingine vikiwa vimekunjwa, alama ambayo imetafsiriwa kuwa ni matusi.

Alisema hatua ya kumuadhibu mbunge huyo maarufu kama Sugu, ilifikiwa baada ya wabunge Jackline Msongozi na Sixtus Mapunda kuomba muongozo, wakilalamika kuwa alama aliyokuwa ameitoa Sugu ni matusi.

Mkuchika alisema walipitia ushahidi mbalimbali kama wa picha za video, kuwahoji wabunge waliotoa miongozo hiyo na kupitia kesi mbalimbali zinazohusu alama hiyo na pia kumhoji Sugu ambaye alikiri kutenda kosa hilo, akitetea kuwa ni alama ya kutoridhishwa na jambo baada ya mbunge mmoja wa CCM, ambaye hakumtaja, kumtukana matusi ya nguoni.

“Kitendo hicho kimelifedhehesha Bunge, wabunge wote na jamii ya Watanzania na kimefanywa na mbunge mzoefu. Hivyo, Bunge linaazimia kuwa Mheshimiwa Joseph Mbilinyi asimamishwe na asihudhurie vikao 10 vya Bunge la 11 kuanzia leo (jana) baada ya azimio hili,” alisema Mkuchika maarufu kama Jaji.

Naye Sugu, ambaye hivi sasa amebadilisha jina la kisanii na kujiita Jongwe, alikuwa na majibu ya adhabu hiyo kwenye ukurasa wake wa facebook.

JONGWE: “Do I look like I care? Definitely NO! (naonekana kama najali? Bila shaka hapana),” ameandika Sugu kwenye ukurasa huo jana.

“Narudi zangu home (nyumbani) Mbeya. Ila wawaambie wabunge wao wa CCM waache kututukana or else nikirudi I will do it again (ama nikirudi, nitafanya tena),”

“FREEDOM to defend my mother (uhuru wa kumtetea mama yangu) dhidi ya matusi ya wabunge wa CCM ndani ya Bunge.”

Alipopigiwa simu, Sugu alisema alichoandika ni maoni yake, lakini akaongeza kuwa alionyesha ishara hiyo, ambayo anaamini si matusi, baada ya kumsikia mbunge wa CCM akimtukania mama yake.

Alipoulizwa sababu za kutoomba mwongozo baada ya kutukanwa ili mbunge huyo wa CCM achukuliwe hatua, Sugu alisema mazingira ya wakati huo hayakuwa muafaka kutokana na uamuzi wao wa kususia vikao, na pia asingeweza kuomba mwongozo kwa kiongozi wa Bunge ambaye hawana imani naye.

“Nilikuwa natoka kusoma azimio mbadala na sisi tulikuwa tumesusia vikao na niliingia bungeni kwa kuwa tulikuwa tumebuni mbinu mbalimbali za kutuwezesha kufanya kazi ndani ya Bunge. Hivyo, kwa mazingira yale, nisingeweza kuomba mwongozo,” alisema.

“Isitoshe unaomba mwongozo kwa nani? Sisi hatuna imani na Naibu Spika kwa kuwa ametunyonga katika masuala mengi ya masilahi ya Taifa. Hivyo huwezi kuomba mwongozo kwa mtu ambaye hamna imani naye.”

Naibu Spika, Dk Tulia Ackson, ambaye amekuwa kwenye mzozo na wabunge wa upinzani, pia alimsimamisha Kubenea kuhudhuria vikao vitano baada kamati ya Mkuchika kukubaliana na malalamiko ya Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Hussein Mwinyi kuwa alisema uongo.

Dk Tulia alieleza kuwa Mei 10, Kubenea alitoa tuhuma kuwa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) liliingia mkataba wa ujenzi wa mradi wa nyumba za wanajeshi na kampuni ya Hanen Guoji Industries Limited na kuipa iuendeshe kwa miaka 40 na kwamba kampuni hiyo pia ingemjengea nyumba binafsi waziri, madai ambayo kamati ilisema alishindwa kuyathibitisha.

Tayari Kubenea alishaandika barua kwa Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah kumshtaki Naibu Spika katika Kamati ya Kanuni akidai kiongozi huyo alikiuka kanuni katika kulisimamia suala hilo.

Olle Millya, mbunge mwingine wa Chadema, alitiwa hatiani na kamati hiyo kwa kosa kuliambia Bunge Mei 24 kuwa mmoja ya wabia wa kampuni ya Sky Associates inayomiliki mgodi wa TanzaniteOne unaodaiwa kunyanyasa wananchi ni shemeji wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Sera, Uratibu na Bunge, Jenister Mhagama.

Dk Tulia alisema Mhagama alieleza kuwa mtu huyo si shemeji yake na aliwasilisha malalamiko kwa kamati hiyo na baada ya kuchunguza tuhuma hizo Ole Millya alishindwa kuthibitisha.

“Kwa mamlaka niliyonayo chini ya kanuni 63(8), namsimamisha Mheshimiwa James Ole Millya kuhudhuria vikao vitano vya Bunge kuanzia tarehe ya leo (jana),” alisema Dk Tulia.

Wabunge hao watatu wanaungana na wengine tisa ambao walishasimamishwa awali kuhudhuria vikao vya Bunge na baadhi wameshamaliza adhabu zao.

Wabunge saba walisimamishwa kwa sababu ya vurugu zilizotokea bungeni Januari 27 wakati wa kutangaza uamuzi wa kusitisha Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) kurusha matangazo moja kwa moja (live).

Waliokumbana na adhabu hiyo ni Mbunge wa Bunda Mjini, Ester Bulaya na Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu ambao wamepigwa marufuku kuhuduria vikao vyote vya mkutano wa Bajeti uliomalizika jana pamoja na mkutano ujao.

Wengine ni wabunge wa Chadema Pauline Gekul (Babati Mjini) na, Godbless Lema (Arusha Mjini), Halima Mdee (Kawe) na mbunge wa Kigoma Mjini, Kabwe Zitto wa ACT –Wazalendo waliopigwa marufuku kuhudhuria vikao vyote vya Bunge la Bajeti.

Pia, Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche (Chadema) alizuiwa kuhudhuria vikao 10 mfululizo vya Bunge la Bajeti na ameshamaliza adhabu.

Juni 17, wabunge wengine wawili wa viti maalumu wa Chadema walisimamishwa kwa kosa la kusema uongo, wakati Suzan Lyimo alisimamishwa vikao vitano, Anatropia Theonest alisimamishwa vikao vitatu. Wabunge hao wote waliosimamishwa walikatwa nusu mshahara na posho.

Ukawa watoka bungeni kwa mbwembwe
Wabunge hao wa upinzani waliendelea na msimamo wa kususia vikao vinavyoongozwa na Dk Tulia na jana walikuwa na staili tofauti.

Waliingia ndani ya ukumbi wa Bunge wakiwa wamevalia nguo nyeusi na vitambaa vyeusi kichwani, tofauti na siku nyingine wakidai kuna “msiba wa demokrasia”.

Baada ya Dk Tulia kusoma dua, wabunge hao walichomoa mabango yao yenye ukubwa wa karatasi za kuandikia barua yaani A4 na kisha kutoka kimyakimya.

Mabango hayo yalikuwa na ujumbe tofauti ikiwamo, “JPM na Tulia Liacheni Bunge Lifanye Kazi”, “Magufuli Hii Si Nchi Yako Binafsi, Hatuwezi Kuongozwa na Kauli za Mtu Mmoja”, na “Kama Mko Sahihi Woga wa Nini?”

Baada ya kutoka ukumbini, wabunge hao waliimba wimbo wa “Mshikamano Daima”, ambao kwa kawaida huimbwa na wafanyakazi.

Mwenyekiti mwenza wa Ukawa, James Mbatia alisema ilikuwa ni ishara ya maombolezo yaliyotokana na tafakari ya kina katika historia ya Taifa kuhusu masuala ya demokrasia.

“Haya tunayoyaona ndani ya utawala wa Serikali ya Awamu ya Tano ni viashiria vya kuizika demokrasia. Tumetafakari kwa kina vitendo vinavyoendelea kwa muda wote tuliokaa bungeni bila kuwa na muafaka.

Tunajua mamlaka yanatoka kwa umma lakini tumeshuhudia Serikali hii imeondoka kwenye utawala wake wa kuongoza kiraia na badala yake kuwa dola inayoongozwa na polisi,” alisema.

Alidai kuwa ndani na nje ya Bunge hadi mahakamani wanashuhudia tabia za kidiktekta zikitawala. “Diktekta ni mtu ambaye ana tabia kuwa kila analolisema anatakalitekelezwe bila kupingwa na mtu yoyote,” alisema Mbatia na kuongeza.

Bila kuwa na mtazamo tofauti na mambo yakaendeshwa kwa pamoja, Taifa haliwezi kusonga mbele. Alisema hawatakubali kuporwa haki hiyo na kuwaomba Watanzania wawaunge mkono katika kuomboleza na kwamba wataendelea kupambana.

Alisema dola haijawahi kushinda jamii hata siku moja na maeneo ambako ililazimisha kuushinda umma, viongozi wao waliondoka madarakani kwa aibu.

Mbunge mwingine, Magdalena Sakaya ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa CUF Bara, alisema masilahi ya wengi yanaminywa na Serikali, ndiyo maana waliadhimisha “msiba” jana kwa kuvaa nguo nyeusi.

Jijini Dar es Salaam, Lissu alifikishwa mahakamani akishtakiwa kwa uchochezi, ikiwa ni siku tatu baada ya mbunge huyo wa Singida Mashariki, kuunganishwa katika kesi ya uchochezi kutokana na kauli yake iliyochapishwa na gazeti la Mawio kuhusu hali ya Zanzibar.

Wakili Mkuu wa Serikali, Bernard Kongola alidai mbele ya Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Kisutu kuwa Lissu, ambaye ni wakili wa kujitegemea, ni mtuhumiwa mzoefu na hana hofu ya mahakama.

“Kwa sababu ametoka kushtakiwa na Jamhuri kwa kosa la uchochezi na bado anafanya uchochezi,” alidai Kongola wakati akisoma hati ya mashtaka.

Lissu alisomewa shtaka moja katika kesi hiyo namba 233/2016, akidaiwa kutoa maneno ya uchochezi kinyume na kifungu namba 32(1)(b) cha Sheria ya Magazeti, sura ya 229 kilichofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

Kongola, ambaye anasaidiana na Nassoro Katuga na Salum Mohamed ambao ni Mawakili Waandamizi wa Serikali, alidai Juni 28 akiwa kwenye viwanja vya mahakama hiyo, Lissu, kwa nia ya kushawishi na kudharaulisha mamlaka halali ya Serikali ya Tanzania, alitoa maneno ya uchochezi.

Akimnukuu, wakili huyo alidai Lissu alisema: “Serikali mbovu ya dikteta uchwara inahitaji kupingwa na kila Mtanzania kwa nguvu zote.

Huyu dikteta uchwara lazima apingwe kila sehemu. Kama uongozi utafanywa na utawala wa kijinga, nchi inaingia ndani ya giza nene.”

Alisema hii inaonyesha kuwa hana hofu na anachokifanya kwani anaona ni kitu cha kawaida, wakati ni kinyume cha sheria.

Kwa sababu hiyo wakili huyo aliiomba mahakama kumpa Lissu, ambaye pia ni mwanasheria wa Chadema, dhamana yenye masharti magumu kwa kuwa anaweza kufanya uchochezi baada ya kuachiwa kwa dhamana.

Lissu alikana shtaka hilo na upande wa mashtaka uliieleza mahakama kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na kuomba mahakama kupanga tarehe nyingine kwa ajili kusomewa maelezo ya awali.

Hakimu Yohana Yongola alitaja masharti hayo kuwa ni mshtakiwa kuwa na wadhamini wawili wa kuaminika ambao watasaini dhamana ya Sh 2milioni kila mmoja na kumzuia mshtakiwa kusafiri nje ya nchi bila kibali cha mahakama.

Akiwa nje ya mahakama, Lissu alisema: “Kama ninachokisema si sahihi, nataka huyo dikteta uchwara aje hapa mahakamani. Aje apinge kama kweli uongozi wake sio wa kidiketa.”

Mshtakiwa huyo ambaye anatetewa na mawakili 11, wakiongozwa na Michael Ngallo, Peter Kibatala na Omary Msemo, yupo nje kwa dhamana na kesi hiyo itaendelea Agosti 2.

Watatu wakamatwa wakiwa na mabango
Hali nje ya mahakama ilikuwa na sura tofauti. Wafuasi walioonekana kuwa wa Chadema walishika mabango yaliyokuwa na ujumbe kama “Polisi Uchwara Acheni Kutumika” , “Dikteta Uchwara Utashindwa” na “Tundu Lissu Tanzania Inakuhitaji”.

Kutokana na kitendo hicho, watu watatu ambao wanasadikiwa kuwa ni wafusi wa chama hicho walikamatwa na kupakizwa katika gari la polisi na kupelekwa Kituo Kikuu cha Polisi.

Imeandikwa na Hadija Jumanne, Nuzulack Dausen na Sharon Sauwa wa Mwananchi

Lissu alifikishwa mahakama saa 6:54 mchana akiwa katika gari la polisi aina ya Toyota Landcruse la rangi nyeusi

Saa 7:30 mchana , Lissu alipandishwa kizimbani na kusomewa shtaka.

Ulinzi uliimarishwa katika mahakama hiyo ikiwemo kuwepo kwa gari moja la maji ya kuwasha, magari saba ya polisi yaliyokuwa na askari ambao wengi wao walikuwa na silaha wakirandaranda kwenye viunga hivyo.

Imeandaliwa na hadija Jumanne, Nuzulack Dausen na Sharon Sauwa

Share: