Habari

MAALIM SEIF APONZA WAHARIRI ZANZIBAR

SERIKALI ya Zanzibar imekiri kuondoa Wahariri wawili wa Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC) kwa madai ya kuwagonganisha vichwa (fitna) Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohamed Shein na Makamu wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Shariff Hamad, kwa kutoa kipaumbele zaidi kwa Maalim Seif katika kutangaza Habari.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Mjini Zanzibar,  Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari,  Utamaduni, Utalii na Michezo Ali Mwinyikai, alisema wahariri hao wameondolewa katika nafasi hizo baada ya kuonekana kukiuka utaratibu na mwongozo wa shirika hilo ambapo wengeweza kusababisha fitna kwa viongozi hao wawili.

Wahariri walioondoshwa ni Juma Mohammed Salum, Muhariri Mkuu Idara ya Televisheni na Msaidizi wake Ramadhan Ali, ambao wamehamishiwa katika Idara ya Habari Maelezo.

Mwinyikai alisema hayo kufuatia mkutano wake na waandishi wa habari waliyotaka kujua nini chanzo cha wahariri hao kuondoshwa katika nafasi zao na kuhamishiwa Idara ya Habari Maelezo. Hatua ambayo walilalamika kukwaza uhuru wa habari na hasa ikizingatiwa wahusika ni watendaji wenye kuheshimu maadili ya Uwandshi.

Aidha, Waandishi hao walisema katika mkutano huo dhana ya uhuru wa habari inaonekana haipo, na Serikali imekuwa ikiingiza mkono wake kwa vyombo vya habari na kutoa mfano wa Wahariri wa ZBC kuondolewa katika nafasi zao kwa madai chombo hicho kinampa nafasi kubwa zaidi Maalim Seif kuliko Dk Shein.

Mwinyikai, akifafanua katika mkutano huo alisema kutokana na utendaji wa Wahariri hao kumpa kipa umbele zaidi Maalim Seif, kuliko Dk Shein, kunajenga hisia za upendeleo na kudai kufanya hivyo kunaweza kukapelekea kuwagonganisha viongozi hao.

Aidha alisema hatua hiyo imechukuliwa kwa sababu ya kumtangaza zaidi Maalim Seif kuliko Rais Shein; Na kuongeza kusema zaidi ya habari tatu za Maalim Seif, imeonekana zinapewa dakika tano hewani, huku za Dk Shein zikipewa dakika moja..Jambo ambalo ni kwenda kinyume na utaratibu na mwongozo wa Shirika hilo.

Katibu Mkuu huyo alisema ZBC haliendeshwi kwa misingi ya itikadi za kisiasa kwa sababu ni mali ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa inayoundwa na vyama viwili Vikuu vya Siasa vya CCM na CUF kwa mfumo wa kugawana Madaraka.

Mkurugenzi Mkuu wa ZBC, Hassan Abdallah MITAWI kwa upande wake alisema kuondolewa kwa wahariri hao katika nafasi hizo ni utaratibu wa kawaida na sio jambo geni kwa kuwa walikuwa katika kipindi cha kuangaliwa utendaji wao wa kazi. “Hilo sio jambo geni ni utaratibu wa kawaida kuwahamisha watendaji sehemu moja na kuwapeleka sehemu nyengine lakini kulikuwa na makosa mengine katika utendaji wao”, alisema Mitawi.

Uchunguzi umebaini kuwa habari inayolalamikiwa ya Dk Shein, na kusababisha kuondoshwa kwa Wahariri hao ni tukio la kuapishwa Naibu Mufti Mkuu na kuondoka kwa Dk Shein kwenda Uingereza, ambapo ZBC Televisheni ilitumia dakika 3:56 Na kufuatiwa na Habari ya Kongamano la wanawake wa CUF iliyotangazwa kwa dakika 2:42

Habari nyengine ya Rais wa Zanzibar, inayodaiwa kutokupewa nafasi ya kutosha ni Michezo ambayo ndio ilikuwa habari kuu kwa siku hiyo. Dk Shein, wakati akizungumza na Kamati ya Kombe la Mapinduzi iliyokwenda hewani dakika 2:32 huku habari ya CUF ya michezo ikitumia dakika 1:30 – Habari zaidi zinaeleza kuwa taarifa ya habari ya shirika hilo la ZBC TV husomwa kwa muda wa nusu saa.

Akizungumza baadae kwa ufupi Mhariri huyo aliyeondoshwa Juma Mohamed, alisema hawakupewa nafasi ya kujieleza ili kuweza kujitetea kutokana na madai hayo kwamba walimpa muda mrefu Maalim Seif na kutoa muda mfupi kwa Dk Shein. Madai ambayo ameyakanusha.

Mfumo wa Vyombo vya Habari vya Serikali ya Zanzibar, unahimiza kwanza kutoa uzito kwa habari ya Rais, Makamo wa Kwanza na kufuatia na Makamo wa Pili na ndio Mawaziri na Wananchi. Wahariri na Waandishi wa vyombo vinavyomilikiwa na Serikali, wamekuwa wakilalamika juu ya mfumo huo kwani unanyima nafasi matukoi mengine muhimu.

Mkutano huo pia ulihudhuriwa na Waziri wa Wizara hiyo Abdillahi Jihadi Hassan, ambaye alisema Wizara yake imeweza kupata mafanikio makubwa katika mambo mbali mbali hasa michezo na Utamaduni..

Share: