Habari

Uingereza imeahidi kuendeleza uhusiano wake na Zanzibar

Uingereza imeahidi kuendeleza uhusiano wake na Zanzibar katika nyanja mbali mbali za maendeleo zikiwemo elimu, biashara na vita dhidi ya dawa za kulevya.

Balozi wa Uingereza nchini Tanzania bibi Dianna Melrose, ameeleza hayo alipokuwa na mazungumzo na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad ofisini kwake Migombani.
Amesema daima Uingereza itakuwa ikifanya kazi kwa karibu na Zanzibar katika kuhakikisha kuwa inapiga hatua za kimaendeleo ikiwa ni pamoja na kuimarisha huduma za kijamii.

Balozi Dianna amemueleza Maalim Seif kuwa ofisi yake itawasiliana na taasisi zinazohusika nchini Uingereza kwa lengo la kuangalia namna zinavyoweza kuisaidia Zanzibar kupata walimu wa masomo ya Sayansi, jiografia na Kiingera, ili kupunguza tatizo la wataalamu wa masomo hayo.

Pia ameahidi kuwasiliana na wataalamu wa ubalozi kuona jinsi wanavyoweza kushirikiana na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka katika kudhibiti uingizaji na matumizi ya dawa za kulevya pamoja na vitendo vya uharamia katika bahari ya Hindi.

Mapema Maalim Seif alimueleza balozi huyo wa Uingereza kuwa Zanzibar bado inakabiliwa na upungufu wa walimu wa masomo ya Sayansi na Kiingereza sambamba na upungufu wa wataalamu wa afya, na kuiomba nchi hiyo kuendelea kushirikiana na Zanzibar katika kusaidia utatuzi wa kero hizo.

Kuhusu dawa za kulevya Maalim Seif amesema serikali inaandaa utaratibu wa kuweza kuwabaini wasafirishaji wakubwa wa dawa hizo nchini ili iweze kuwachukulia hatua za kisheria.

“Ukweli ni kuwa wahusika wakuu wa dawa za kulevya ni vigumu kuweza kuwapata wakiwa na ushahidi kamili kwa sababu wao hawabebi dawa hizo bali wanawatuma vijana kufanya kazi hiyo, lakini tunaweza kutumia utaratibu mwengine kuwabaini na kuwachukulia hatua”, alifahamisha.

Katika mpango huo pia amesema watazibainisha nchi zinazotoka dawa hizo, sambamba na kuimarisha ulinzi katika bahari kuu, ili kufikia lengo la serikali la kuifanya “Zanzibar huru bila ya matumizi ya dawa za kulevya”.

Akizungumzia kuhusu Serikali ya Umoja wa Kitaifa, Maalim Seif amesema imepata mafanikio makubwa katika kujenga mazingira bora ya kiuchumi na uwekezaji, pamoja na kuendelea kwa maelewano na mashirikiano miongoni mwa wananchi.

Maalim Seif ametumia fursa hiyo kutuma salamu za rambirambi kwa Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron kufuatia kifo cha Waziri Mkuu wa zamani wa nchi hiyo bibi Magret Thatcher.

Share: