Habari

Kundi la maharamia latumwa Zanzibar

Kundi la maharamia latumwa Zanzibar

Tayari limeshateka vijana 8 Pemba

Matawi ya CUF yameanza kushambuliwa

Lengo ni kuiingiza nchi kwenye machafuko

Balozi Iddi, Mungiki wa Lipumbwa watajwa kuhusika

Na Mwandishi Wetu, Zanzibar

Taarifa ilizolifikia dawati la habari la Mzalendo.Net zinaeleza kuwepo kwa kundi la maharamia lililoingia visiwani Zanzibar usiku wa kuamkia Jumatano likiwa limegawanywa kwenye makundi manne na kusambazwa Unguja na Pemba.

Kwa mujibu wa mpasha taarifa wetu kundi hilo, ambalo linahusishwa na kampeni ya kuichafuwa Zanzibar kiusalama katika wakati ambapo mgogoro ndani ya chama kikuu cha upinzani, CUF, unazidi kuvungunya na suala la uchaguzi wa 2015 likigonga vichwa, limepewa jukumu la kufanya mashambulizi na hujuma mbalimbali ikiwemo kupiga, kutesa, kuripua mabomu na kuchoma majengo moto na hata kuuwa.

“Hili kundi tayari limeunganishwa na wale munaowaita Mazombi, ambao wana makambi yao Tunguu na Fumba kwa hapa Unguja na wako chini ya usimamizi wa moja kwa moja wa Balozi Seif Idd, kwani hawa wageni walioletwa kutoka Bara wanakaa kwenye majumba yake aliyoyajenga,” kinasema chanzo kimoja cha taarifa kutoka duru za karibu na viongozi wanaotajwa kuhusika na mpango huo wa kiharamia.

Wakati Mzalendo.Net ilipokuwa inafuatilia undani wa kuwepo kwa kundi hilo, kuliibuka ripoti ya vijana sita waliotekwa katika kijiji cha Mtambwe kisiwani Pemba, ambapo mpasha taarifa wetu aliiihusisha moja kwa moja na kundi hilo.

“Nilikwambia kwamba tayari wapo na wanafanya kazi zao kwa uhakika. Hayo ya Mtambwe ni sehemu moja tu. Hata kupachuliwa kwa bendera za matawi ya CUF huko Fuoni na kaskazini Unguja ni njama yenyewe hiyo. Lengo hasa si hapo. Lengo ni kuwa hawa jamaa wa CUF waseme wamechoka na waanze kujibu mashambulizi. Hapo ndipo hasa ngoma itaanza,” kilisema chanzo hicho, ambacho kwa sababu za usalama wake, Mzalendo.Net imeamua kuhifadhi jina na nafasi yake.

Akihitimisha ziara yake ya wilaya za Zanzibar siku ya Alhamisi, Katibu Mkuu wa CUF alitaja matukio ya kupachuliwa na kuchanwa kwa bendera za chama chake katika maeneo hayo hayo aliyoyataja mpasha taarifa wetu, lakini yeye Maalim Seif akiyahusisha moja kwa moja na ziara ya Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan, akimtaja kuwa mmoja wa viongozi wanaopigania kuhakikisha kuwa “haki ya Oktoba 2015 hairudi.”

Katika tukio hilo la Mtambwe, ambalo lilitokea usiku wa kuamkia Ijumaa hii, vijana wanaotajwa kupotea pamoja na umri wao kwenye mabano ni hawa wafuatao: Said Sanani Mohammed (16), Juma Kombo Fimbo (17), Abdallah Khamis Abdalllah (19), Khamis Abdallah Mattar (25), Thuwein Nassor Hemed (30) na Khalid Khamis Hassan (30), wote wakaazi wa kijiji cha Mitambuuni.

Mmoja wa watu walioshuhudia tukio hilo, Suleiman Hemed, alikiambia kituo cha utangazaji cha Ujerumani, Deutsche Welle, hapo jana, kwamba kwa siku mbili kabla ya kutekwa kwa vijana hao, kijiji chao kilikuwa kinatembelewa na magari yenye nambari ngeni kwao.

“Usiku wa jana kama saa tano na nusu, zilirudi tena gari zile zile lakini sasa zikiwa nne, zikiwa na watu wasiopungua 35, wengi wao wakiwa na silaha za moto na waya za umeme, wakagonga milango wakijitambulisha kuwa wao ni maafisa wa usalama wanafanya doria ya karafuu. Wakalazimisha kufungua milango au wangelivunja. Wakaingia na kuchukuwa watoto hadi wa miaka 16, 17. Tukatoa taarifa polisi lakini wakatwambia huko hawako,” alisema Suleiman.

Kamishna Msaidizi wa Polisi wa Kaskazini Pemba, Hajji Khamis, alikiri kupokea taarifa za kuchukuliwa kwa vijana hao lakini kwa sasa hakuwa na taarifa zaidi.

Katika tukio jengine, kijana anayefahamika kwa jina la Juma Ndevu alivamiwa nyumbani kwake Mtoni, Unguja, na kupigwa vibaya. Ndevu ni mmoja wa walinzi wa viongozi wakuu wa CUF, na kwa mujibu wa mpasha taarifa wetu, wao hao viongozi wa CUF ndio walengwa wakubwa wa kundi hili lililo kwenye operesheni maalum.

Matukio haya, kinasema chanzo chengine kutoka ndani ya chama cha CUF, yanafahamika na viongozi wa juu wa chama hicho kuwa yanawahusisha pia wale viongozi hao wanaowaita “wasaliti na Mungiki wa Lipumba”, aliyekuwa mwenyekiti wa chama hicho.

“Huu mpango wa hujuma tunaujuwa sisi. Tunajuwa kuwa Mungiki, hasa Thiney (aliyewahi kuwa mkuu wa ulinzi wa chama hicho kabla ya kujiunga na Profesa Ibrahim Lipumba), wanashirikiana bega kwa bega na akina Seif Ali Iddi na Haji Omar Kheri kuhakikisha kuwa sisi tunashambuliwa, kuuawa na ikishindikana basi tunakamatwa na kufungwa,” alisema kiongozi mmoja wa ngazi za juu wa CUF, ambaye anasema jina lake ni moja ya majina yaliyomo kwenye orodha ya kudhuriwa na kundi hilo.

“Unajuwa mwandishi, wakati alipouliwa yule Ali Juma wa Mtoni (Unguja) mwaka jana, nchi nzima ilitikisika kwa kuwa aliwahi mwenyewe kujieleza kabla ya kukata roho, na makundi yote ya mazombi yakaamriwa kutawanyika kwanza kwa muda. Sasa wamerudi wakiwa na usimamizi wa hawa maharamia bingwa kutoka Bara. Wamekusudia kufanya matukio makubwa sikku itakaponyesha iwe usiku au mchana. Sijui kwa nini wakachaguwa siku ya mvua!” Kinasema chanzo chengine kilichoambatana na chanzo cha awali kwenye mazungumzo yao na Mzalendo.Net.

“Hii ni operesheni maalum. Hawa walioletwa kutoka Dar wanafahamika kwa matendo yao. Sisi wengine tunasema ni kundi lile lile linalohusika na mashambulizi ya kina Lissu, kupotea kwa Ben Saanane, kuuawa kwa viongozi wa Chadema. Ni sehemu ya hao hao. Wao wamepewa mazombi kufuatana nao. Mazombi wanawaonesha maeneo, wao wanatoa mkakati. Kwa pamoja wanatekeleza,” anasema mpasha taarifa wetu.

Tagsslider
Share: