Habari

ACT Wazalendo: Wanachama wetu kisiwani Pemba wabugudhiwa na Polisi

TAARIFA KWA UMMA:

*Dola inaendeleza uchokozi dhidi ya ACT Wazalendo Zanzibar : Wanachama wetu kisiwani Pemba wabugudhiwa na Polisi*

Baada ya ziara visiwani Zanzibar yenye mafanikio ya kihistoria iliyofanywa na viongozi wa kitaifa wa ACT Wazalendo wakiongozwa na Kiongozi wa Chama Ndugu Zitto Kabwe, Makamo wa Kwanza wa Rais Mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Ndugu Maalim Seif Shariff Hamad na viongozi wengine wa kitaifa wa ACT Wazalendo, ni dhahiri kuwa dola imeanza kuingiwa na kiwewe.

Kwenye ziara hiyo ya tarehe 21 Machi hadi 24 Machi 2019, jumla ya wanachama wapya 125,000 walijiunga na chama cha ACT Wazalendo.

Pia, matawi yote yaliyokuwa ya Chama cha CUF visiwani Zanzibar sasa yamekuwa ya ACT Wazalendo kwa sababu wanachama wake wamejiunga na ACT Wazalendo.

Katika kuthibitisha kiwewe cha dhahiri cha dola, Jeshi la Polisi kisiwani Pemba limeanza kamatakamata na kuwabughudhi wanachama wetu.

Jana tarehe 28 Machi 2019, Ndugu Riziki Omar Juma na Ndugu Mwinyi waliitwa na Jeshi la Polisi Wilaya ya Wete na kuhojiwa kuhusu mkutano wa ndani wa ACT Wazalendo uliofanyika tarehe 24 Machi 2019. Walituhumiwa pia kwa kupandisha bendera za ACT Wazalendo kwa takbiir siku ya tarehe 18 Machi 2019. Baada ya mahojiano ndugu hao wameachiwa huru jana.

Aidha, mwanachama wa ACT Wazalendo Ndugu Khatib Kombo wa Wilaya ya Micheweni naye aliwekwa ndani katika kituo cha Polisi Micheweni kwa muda wa masaa matatu kwa kutuhumiwa kwa kosa la kushusha bendera ya CCM siku ya tarehe 18 Machi 2019.

Katika Wilaya ya Micheweni, wapenzi wa ACT Wazalendo Ndugu Shame Kombo na Ndugu Ali Nasoro wa Kijiji cha Shumba Mjini walikamatwa na polisi mkoa wa Kaskazini Pemba siku ya tarehe 27 Machi 2019 kwa tuhuma za kushusha bendera ya CCM usiku wa tarehe 18 Machi 2019. Ndugu hao wameachiwa jana.

MSIMAMO WETU

1. Mikutano yote iliyofanywa visiwani Zanzibar wakati wa ziara ya Kiongozi wa Chama Ndugu Zitto Kabwe na viongozi wengine wa kitaifa ilikuwa mikutano ya ndani. Hakukuwa na maandamano wala mikutano ya hadhara. Hivyo basi, polisi waache kuwabughudhi watu wetu. Kama Chama hatutavumilia kuona wanachama wetu wakiendelea kubughudhiwa na polisi au kubambikiwa kesi.

2. Inafahamika kabisa kuwa CCM ni chama dhaifu sana Zanzibar. ACT Wazalendo hakiwezi kuhangaika na bendera za CCM kisiwani pemba sehemu ambayo CCM haikupata Mbunge wala diwani kwenye uchaguzi halali wa mwaka 2015 na wanachama wake hawajai mkononi!

3. Chama cha ACT Wazalendo kinafanya shughuli zake kwa mujibu wa sheria. Jeshi la Polisi na dola kwa ujumla wake viache mara moja chokochoko na kutuchokoza. Visitufikishe kwenye kona ambayo hatutakuwa na namna isipokuwa kujihami.

Ado Shaibu, Katibu wa Itikadi, Mawasiliano na Uenezi, ACT Wazalendo.
29 Machi 2019.

Share: