Habari

Ajira za undugu ni kushindwa kwa mfumo

Thursday, August 7, 2014
Na Salim Said Salim

MOJA kati ya mambo yaliyotawala katika vyombo vya habari hapa nchini wiki iliyopita ni ajira zinazodaiwa kutolewa na Idara ya Uhamiaji kwa watu wenye uhusiano na watendaji wa idara hiyo.

Ajira hizi naweza kuziita ni zile za dada njoo haraka… kaka sogea kwa raha zako… mwite hapa mjomba apumue… shangazi fanya uje ninakwita… shemeji karibia na mkwe tuwe karibu na kufaidi matunda ya nchi.
Taarifa zenye mshiko na uthibitisho zinaeleza kuwa ajira katika Serikali ya Muungano na Zanzibar zinatolewa kwa upendeleo wa misingi ya kindugu na si kutegemea sifa za elimu na uwezo.
Kwa maana hiyo ukisikia unafanyika usaili wa watu kuajiriwa basi hilo hufanyika kama danganya toto.
Mengi yamesemwa, kusikika na kuandikwa juu ya suala hili, lakini imekuwa sawa na kumpigia mbuzi gitaa au kuku mchezea msewe.
Watu wanaofanya haya wamekuwa hawajali na wanaona nchi hii n kama mali za familia zao na wao pekee ndio wenye haki ya uamuzi wanaoutaka kwa mujibu wa utaratibu waliojiwekea.

Wapo wanaosema hata nafasi za kugombea uongozi au kuteuliwa kushika nafasi hizo kama ubunge au Baraza la Wawakilishi nazo hutolewa zaidi kwa misingi ya kifamilia. Ukiangalia Bunge unapata hisia za kukubaliana na hoja hii.
Kwa lugha nyingine watu wengi wanaopata nafasi hizo huwa watoto na jamaa za Ibni Kinana, Ibni Khuzaymat na Ibni Ilyas na wenzangu mie wa kwangu pakavu na hakuna wa kunitilia mchuzi wanabaki kuramba mikono tu na kumeza mate, tena yenye ladha mbaya kama ya kinywa kinachohitaji kupigwa mswaki.
Hata hivyo uongozi wa Wizara ya Mambo ya Ndani hivi kribuni umechukua hatua ya kijasiri na si ajabu watu waliohusika wakaitwa “sio wenzetu” kwa kusitisha ajira za makonstebo na makoplo wa Idara ya Uhamiaji wapatao 200.
Hii imetokana na kubainika kuwepo tuhuma za udanganyifu na upendeleo wa katika ajira zilizotolewa hivi karibuni. Tunapozungumzia ujamaa na kujitegema hatukusudii ujamaa kwa ajira katika serikali.
Kwa mujibu wa taarifa ya karibuni ya msemaji wa wizara hiyo kwa vyombo vya habari, Isaac Nantanga, uamuzi wa kusitishwa kwa ajira hizo umetolewa na Katibu Mkuu wa Wizara, Mbarak Abdulwakil.
Hatua hii imechukuliwa kutokana na tuhuma katika baadhi ya vyombo vya habari na mitandao ya kijamii kuwa kulikuwa na upendeleo kwa ndugu na jamaa za watumishi wa idara hiyo ambao ndio wanaodaiwa kupewa ajira.
Hivi sasa waombaji wote walioitwa na kutakiwa kuripoti makao makuu ya Idara ya Uhamiaji Agosti 6, mwaka huu wameambiwa wasubiri hadi watakapotangaziwa tena baada ya uchunguzi wa suala hili kukamilika na kufanyika uamuzi.
Kwa kweli hata kama hapatachukuliwa hatua za kuirekebisha hali hii Wizara ya Mambo ya Ndani inafaa kupongezwa kwa ujasiri wake wa angalau kuonyesha inajali na kutilia maanani malalamiko ya jamii juu ya ajira serikalini.
Lakini pia si ajabu tukasikia wote waliohusika na kufikia uamuzi huu wamepewa uhamisho au kuondolewa kazini na kutakiwa wangojee kupangiwa kazi nyengine.
Haya yanaonekana kuwa ndio mazoea katika nchi yetu kutokana na kujijengea utamaduni wa kukosoa au kutokubaliana na wakubwa kuwa ni dhambi au kosa la jinai.
Hivi sasa imekuwa mazoea hapa nchini kuambiwa na kulazimishwa kukubali kuwa wakubwa wanayo haki ya kufanya watakalo na anapofumbua mtu mdomo kukosoa akina fulani hueleza bila ya aibu kuwa vongozi wetu ndio walezi wa nchi yetu na watakalowao ndio liwe, imma faimma lazima.
Lakini kama kweli tumeamua kuwa waadilifu basi kurunzi iiyotumika kuangalia namna ajira zilivyotaka kufanyika Idara ya Uhamiaji pia itumike katika taasisi nyengine ambapo upo uozo zaidi ya huo.
Kwa mfano Zanzibar yapo malalamiko kuwa vijana wa Kipemba wanawekewa ngumu kupata ajira serikalini na kwenye vikosi vya Muungano na vya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
Zipo taarifa ambazo sina hakika nazo lakini watu wanadokeza kuwa lisemwalo lipo na ninaona linafaa kuchunguzwa ni kuwa vijana husafirishwa kutoka Unguja kwenda Pemba kuchukua nafasi zilizowekwa kwa kuajiriwa vijana wa kisiwa hicho.
Ukiangalia hata orodha ya wakuu wa idara wakiwemo wakurugenzi na manaibu wao utabaini hilo linalosemwa lina ukweli kwa kiwango kikubwa.
Hivi karibuni tu pamesikika malalamiko kuwa hali hii pia imetia nanga katika taasisi ambayo inatarajiwa kuongoza kutoa mfano wa utendaji haki, yaani mahakama.
Huko wengi wanaoajiriwa ni watoto ambao wazazi wao na mahakimu au wafanyakazi wa ngazi za juu wa mahakama.
Siku hizi katika baadhi ya ofisi ni kawaida kuwakuta watu watatu wa familia moja katika chumba kimoja. Kazi itafanyikaje kama mkuu wa kitengo ni baba, karani ni mtoto na tarishi ni shangazi.
Wapo pia wanaolalamika kuwa baadhi ya ajira zinafanywa kupitia matawi ya chama kimoja cha siasa (Watanzania wanaielewa vizuri hali hii).
Hata baadhi ya wakati inasemekana kushiriki kukimbiza mwenge ni moja ya sifa ya kupata nafasi ya uongozi.
Katika ugawaji wa viwanja hutumika udugu. Baraza la Wawakilishi liliwahi kuelezwa kuwa ugawaji wa viwanja Tunguu, nje ya mji wa Unguja ulifanywa kwa baadhi ya watu, waume au wake za, watoto na wajukuu kupewa viwanja vya eneo hilo (pitia kumbumkubu za Baraza).
Orodha ya vizungumkuti vya upendeleo wa kutoa ajira na vitu mbali mbali serikalini ni ndefu na inasikitisha na kutisha.
Njia nzuri ya kujisafisha kama yanayosemwa si ya kweli, ni kuundwa tume ya uchunguzi kuliangalia kwa undani suala hili.
Kama litaonekana kuwa gumu basi orodha ya watu wote walioajiriwa karibuni itolewe pamoja na maelezo ya wazazi wao wanafanya kazi taasisi gani. Sura itakayojitokeza ndiyo itatoa jawabu la mbichi au mbivu.
Hakuna ubishi kuwa watoto, wajomba mashangazi na ndugu wa wakubwa wanayo haki ya ajira serikalini, lakini hili ni lazima lifanyike bila ya kuwepo mashaka ya upendeleo wa aina yoyote ile.
Hadi pale serikali itakapochukua hatua ya kuwepo na uwazi wananchi wataendelea kulalamikia mwenendo wa ajira katika serikali ambao unadaiwa kuwa na harufu ya ubaguzi na upendeleo.
Huu mtindo wa kuutaka umma uamini kila linalotokea serikalini limefanywa kwa nia njema haukubaliki. Watu wanataka kuwepo na uwazi na panapotokea ajira basi itolewe bila ya upendeleo wa aina yoyote.
Ajira katika serikali haiwezi kutolewa kama zawadi, sadaka au zakka ambayo aliyekuwa nayo huamua nani ape na nani asimpe.
Nchi hii, Bara na Visiwani, ni mali ya Watanzania wote bila kujali kama ni matajiri, masikini na mafukara, wakubwa (kwa vyeo) na wadogo, watu wenye ulemavu na kadhalika.
Utoaji wa ajira kwa upendeleo wa aina moja au nyingine ni rushwa na ufisadi, mambo ambayo yanakwenda kinyume na utawala bora wa haki na sheria na hakubaliani na mfumo wa demokrasia tunaotaka kuujenga nchini kwetu.
Watu huwa na haki ya kurithisha fedha, nyumba. Shamba au mali yoyote ile lakini si kurithishana ajira katika serikali ni dhambi ambayo haikubaliki na ni lazima Watanzania wa Bara na Visiwani wasimame imara kuipiga vita kwa nguvu zao zote.
Kuwaachia wachache kutupanda juu ya vichwa vyetu na kuifanya nchi hii kama shamba lao la kuku ni hatari itakayotuponza siku za usoni na kuwa na matokeo mabaya kwa vizazi vijavyo.
Ubaguzi ni ubaguzi, uwe wa dini, kabila,dini, asili, jinsia, rangi na hata katika ajira. Tuupige vita kwa pamojana tena bila ya muhali leo na siku zjazo.
Kama wanaofanya hivi hawaoni muhali kutenda maovu haya kwa nini na wao tuwaonee muhali kwa kututendea maovu katika nchi yetu.

Chanzo : Tanzania Daima

Share: