Habari

Aokotwa akiwa maiti ,adaiwa kubakwa huko Fundo Pemba

August 9, 2018

Imeandikwa na Salmin Juma Salmin , Pemba

Wananchi wa kisiwa cha Fundo mkoa wa kaskazini Pemba jana walipigwa na butwaa baada ya kupokea taarifa na wengine kushusuhudia maiti ya mtoto wa kike katika ufukwe wa bahari.

Maiti hiyo ilitambuliwa kwa jina la Salma Said Ali (22) ambae ni mgonjwa wa akili.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi kaka wa marehemu (mtoto wa baba mkubwa) aliyejitatumbulisha kwa jina la Yussuf Omar amesema , ndugu yao aliondoka nyumbani tokea majiira ya alaasiri jioni kwenda kujisaidia (bondeni) lakini walipatwa na hofu baada ya kukaa muda mrefu pasi na kurejea hivyo waliamua kumtafuta katika kila eneo la kisiwa hicho.

“ilipofika saa 1 jioni tukapeleka taarifa za kupotea mtoto wetu, kwa kushirikiana na wanakijiji tukaamua kumtafuta na mwisho ndio tukamuona baharini akiwa ameshafariki dunia.

Katika hali ya masikitiko Yussuf amesema, wanasikitishwa na kifo cha mtoto wao, kutokana na kuwa na majiraha mingi mwilini huku taswira ikionyesha kuwa alibakwa kwanza kabla ya kifo chake.

Kwa upande wake sheha wa shehia ya Fundo Khamis Abeid Ali amesema, habari hizo alizopokea kwa masikitiko na alimua kushirikiana moja kwa moja na wananchi wake kumtafuta mtoto huyo hadi hapo majira ya saa 3 usiku walipofanikiwa kumpata akiwa ameshafariki dunia.

“maiti ilionekana imechunika sana mgongoni , inaonekana walimburua mpaka wakamtia habarini, na pia inasemekana amebakwa” alisema sheha huyo.

Sambamba na hayo sheha amevitaka voymbo vya sheria kuzidisha juhudi katika uchunguzi ili sheria ikamate mkondo wake kwa wahusika wa tukio hili.

Nae kamanda wa Polisi mkoa wa kaskazini Pemba Hassan Nassir amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa wanaendelea na uchunguzi na hatua za kisheria zitakapokamilika hawatosita kuwashuhulikia wahusika.

“ni kweli tukio tumelipokea na askari wanalifanyia kazi tukio hilo na pia kuna taarifa za kuwa kabla ya kifo chake alibakwa hivyo pia tunafanyia kazi taarifa hii” alisema kamanda .

Mareheme Salma amezikwa jana jioni huko Mwambe mkoa wa kusini Pemba.

Pemba Today

Share: