Habari

Asemavyo Mzee Kondo

Mzee Kondo

Nakubaliana na mitazamo ya somo letu la leo au mada husika. Sisi tunahitaji suluhu kwa gharama yoyote ile hapa visiwani kwetu, kwa sababu bila maelewano au maridhiano, nchi au visiwa hivi havitokalika siku zote. Sasa kuna wanaodhani nguvu inatosha kuleta amani wana hiari yao, hao siwezi kuwashawishi vinginevyo, kwa sababu matatizo sio wao, ni upeo au ufahamu wao kuhusu masuala haya walio nao ni mdogo au haupo kabisa.

Dr Mabodi anazungumza kama ccm inavyotaka, sio anavyotaka yeye. Watu kama yeye tunao wengi katika Chama cha Mapinduzi, hata Rais mwenyewe wa sasa yaani Dr Sheni ana mtazamo tofauti na wa CCM kwa sasa kuhusu Zanzibar. Lakini atafanya nini na chama ndio kinamtaka asithubutu kuitafuta SULUHU.

Matatizo yetu siku zote tutashindwa kuyapatia ufumbuzi, kwa sababu kila anaekuja kuwa kiongozi hapa huwa kawekwa na sultan wa Mwanza au Musoma. Sisi Wazanzibari hatujiulizi kwa nini kila tunaemtaka sie awe Rais huwa hapiti Dodoma? Jawabu ni rahisi sana, chaguo letu huwa hawaliamini hata dakika moja. Sasa inategemea huyo wanaetaka wao atakuwa na msimamo gani baada ya kuupata Ugavana. Wengi wameonyesha kuupenda Uzanzibari zaidi, ndio maana kuanzia Marehemu Aboud Jumbe, alipotaka kuinusuru zanzibar ilibidi alazimishwe kujiuzulu. Komandoo Salmin Amour pia alitawala alivyotaka yeye, jambo ambalo lilimletea kutokuelewana na Nyerere. Lakini Mwalimu alimjua zamani au mapema, ndio maana Dodoma wakati Salmin anapitishwa kuwa mgombea urais wa Zanzibar, Mwalim alitamka wazi kuwa yeye sio chaguo lake. Yeye alimtaka Salim, lakini Wazanzibar waliokuwa wakijiita Liberators ndio waliotaka, kina Natepe na wenziwe.

Amani Karume ccm hawakuwa na budi kwa kuwa walimuogopa tena Dr Gharib. Kwa kuhofia siasa za muendelezo za Dr Salmini, kwa kuwa alikuwa mtu wake ccm wakabahatisha kwa mtoto wa Karume. Japokuwa walikuwa wanajua kuwa huyu ni Mzanzibari zaidi, Utanzanzia wake una mashaka matupu. Matokeo yake kaja na katiba mpya ya Zanzibar ambayo inamshinda Dr Sheni kuitawala Zanzibar kwa kuwasikiliza ccm. Katiba ndio kioo cha kuongoza sio chama katika nchi zote duniani isipokuwa Zanzibar tu.

Suluhu katika familia moja huwa ndio msimamo wa kila nyumba. Sisi tunavutana CCM, CUF, CCM, CUF, miaka zaidi ya 25 sasa, tunasahahu kuwa sisi sio CCM wala CUF, sisi ni Waislamu kwanza, halafu tena ndio Wazanzibari. Sasa nani katuroga namna hii miaka yote hii kwa wale wanaoamini shirki.

Tanganyika wanajua siku Wazanzibari wakiamka, na kuvitupa hivi vyama vyote vya siasa, na kuja na bango lao moja tu la kudai nchi yao, huo ndio utakuwa mwisho wa taifa hili linaloitwa TANZANIA au CCM.

Zanzibar kwanza, vyama basi tena sio baadae.

Nashukuru.

Share: