Habari

Asemavyo Mzee Kondo kuhusu mapinduzi ya 1964

Nimevutiwa sana sana na mawazo/maoni yako kuhusu Mapinduzi, naiheshimu sana michango yako, kwa sababu kama ilivyo sarafu, mara zote huwa unajikita pande zote mbili katika kufikiri na kuchambua, huku ni kukomaa kiakili. Wengine watadhani kuhitimu kwa alama za juu kielimu peke yake, ndio kiini cha uchambuzi wa kina au kufikiri kwa upeo mzuri. Mimi nasema ukomavu wa akili pia unahitaji, katika kuyakubali mengi mengine ambayo kwa kutumia elimu peke yake, basi ungeliyakataa.

Mapinduzi yetu ya 1964, kama ulivyonena hii sasa ni HISTORIA TU, iko haja ya kujifunza na kukifunza kizazi chetu kipya kwa nini tulipitia historia hii, na kwa nini mpaka leo bado tunapinduana wenyewe kwa wenyewe, tofauti ya mapinduzi yetu ya siku hizi, tumeacha kutumia mapanga, mawe, bunduki au shoka sasa tunatumia KARATASI.

Mapinduzi yetu ya 1964, lengo kuu ilikuwa kumuondoa mkoloni aliyekuwa akitawala au kukalia kiti cha UFALME huku akilindwa na Muingereza, japokuwa waliokuwa wakiongoza serekali ya wakati huo walikuwa Waafrika wenyewe. Sasa tatizo kubwa ambalo mpaka leo bado linatula roho, sisi bado hatumjui nani MUAFRIKA NA NANI SIE.

Marehemu Mzee karume alikuwa Muafrika, kwa mujibu wa mapinduzi yetu na wale wote waliopinduliwa hawakuwa waafrika. Yaani Waingereza na Waarabu wote, ndio maana tuliwauwa bure Waarabu kwa maelfu, hatukuchagua, watoto, wanawake, waja wazito, wazee, vijana bila huruma wala kosa tuliwadhulumu roho zao kwa kisingizio cha mapinduzi yetu ya 1964 na tukawafukia kama mizoga katika makabauri ya watu wengi(mass graves)

Mapinduzi yetu ya 1964 hayakuwa na ulazima wa kuwauwa watu bure na ovyo kwa maelfu ili kuipata nchi, kwa sababu raia hawa waliouwawa hawakuwa na silaha yoyote ya kujihami au kuzuwia nchi isianguke au kupinduliwa. Wao walikuwa ni sehemu ya raia kama walivyokuwa raia wengine. Hii ina ma’anisha kwa kuwa hawa walikuwa Waarabu, haina maana wote walikuwa matajiri, wengi walikuwa masikini pia kama walivyo raia wenzao, rangi zao ndio ziliwaponza na kuonekana au kutiliwa mashaka UAFRIKA WAO,

Wazee wetu walikuwa wakishirikiana nao katika kukopeshana na hata kushirikiana katika harusi na mazishi, lakini siku ya mapinduzi wengine walisahau au kuutupilia mabali utu wao na wa wenzao na waliokuwa wakiishi nao, na kuwageukia kwa kuwadhulumu mali na uhai wao, kwa kuegemea Mapinduzi. Ndio maana niliwahai kuandika kuwa sio kila aliyeuwawa siku hiyo alikuwa HAINI au alistahiki kuuliwa, na ukiuliza au kusema kuwa ni lazima tukubali kuwa makosa yalitendeka, basi wewe sio mwenzetu au hupendi Mapinduzi. Lazima tujuwe kutofautisha chungwa na embe wazungu wana msemo wao “apples and oranges” sisi kwa uhaba wa ma’apples ndio nimeangukia kwenye embe.

Mapinduzi yetu ya 1964 hayana tofauti na mapinduzi ya nchi za wenzetu kote duniani, makosa hutokea na watu huuwawa bila sababu kwa kisingizio hicho. Ndio maana matukio ya kubakwa wanawake, wanaume au watoto, pamoja na kuuliwa au kukatwa mikono na kutiwa vilema vingine, kuchomeana nyumba hutokea katika jamii zote, sio Afrika peke yake, hata nchi za ulaya, Asia na Marekani ya kusini matukio haya yametoke. Sasa sisi tunaogopa nini kukubali Makosa. Wengi wanadhani kukubali ukatili tuliowafanyia raia wenzetu ndio kukataa Mapinduzi huu ni wenda wazimu.

Mapinduzi yetu ya 1964 hayajatufunza na wala hayatotufunza kitu chochote cha msingi ikiwa hatujakaa kitako na kuelimishana faida na hasara ya mapinduzi yenyewe, kwa sababu vyote tumepata hatukupata faida tupu, kama ilivyo biashara yoyote, na sisi Mapinduzi haya tuliyonayo, tukitaka tusitake,tukikubali tusikubali ukweli utatusuta kadri siku zikisonga mbele.

Kama tulipindua ili tujitawale kama alivyotuambiwa Mzee Karume nani anathubutu kufikiri au kusema kuwa sisi ni watu HURU? Hata ukisimama pale mental hospital kidongo chekundu, na kumuuliza mgonjwa yeyote suala hili, basi usije kustaajabu au kujuta akija kupata akili na kukujibu kuwa sisi bado tunatawaliwa na mfalme Magufuli.

Sasa ikiwa lengo la kumuondoa Muingereza na Muarabu ili aje Msukuma mimi simo, na kama itanigharimu utiifu wangu kwa mapinduzi na iwe hivyo. Kama kuna kiongozi nitamuenzi mpaka kufa kwangu basi kiongozi huyo ni marehemu mzee Karume, kwa sababu hakutukomboa kutoka makucha ya wakoloni, kama walivyofanya viongozi wote wa kiafrika wa wakati wake, ili waje kina marehemu Aboud Jumbe, na wengine wote waliofuatia mpaka kufika hapa kwa Dr Sheni, badala ya kututoa utumwani, wao ndio wanatutundika zaidi katika misalaba ya mkoloni Mtanganyika, na ikifika january 12 ya kila mwaka, basi sisi tunatakiwa tutembee vifua mbele na kuambiwa hii ndio siku tuliyokombolewa au kujikomboa, nani tunamdanganya? Tunajidanganya kwa gharama yetu wenyewe.

Zanzibar ilikuwa nchi huru, kabla Muungano huu na mapinduzi haya huu ni ukweli mtupu, sasa irudishieni Zanzibar heshima yake na muache usanii na maneno vinywa tele. Mimi najua tunaukumbatia MUUNGANO na MAPINDUZI kwa kutafuta hifadhi au salama ya CCM hapa visiwani, bila vitu viwili hivi hakuna chama cha mapinduzi hapa. Sasa hatuoni kuwa wananchi walio wengi wa visiwa hivi hawajali haya bali wanataka Nchi yao?

Hivi karibuni wengi walidhani umati wa Zanzibar ulikuwa ukisherehekea mpira tu, baada ya Zanzibar kuingia fainali na kutolewa kwa penalti na Kenya. Ule haukuwa mpira peke yake, wala zile kelele, matusi waliyokuwa wakiyatoa vijana baada ya kuwafunga Tanganyika, zile zilikuwa kelele za uchungu wa kutawaliwa na kumtia adabu mkoloni. Pia furaha za kuionja Zanzibar japo katika uwanja wa mpira na sio siasa, hakukuwa na ccm wala cuf katika kuipokea na kuitafuta Zanzibar siku ile, wote walikuwa Wazanzibari. Wala sikumouna Muarabu wala Mmakonde pale, wote walikuwa kitu kimoja, na wote walililia na kufurahi pamoja kama ndugu wa tumbo moja liitwalo zanzibar. Sasa ni lazima wana siasa mkajua, kuwa nyie ndio mnaotubagua siku zote kwa kutafuta kura, sisi huku sote ni WAAFRIKA AU KWA JINA RASMI NI WAZANZIBARI.

Mapinduzi yana ncha mbili, tuzikubali zote ili tusonge mbele. Tatizo letu ni Tanganyika siku zote/ kwa sasa, sio nani alimpindua nani huko tunakotoka. Yaliyopita si ndwele, tugange yaliyopo na yajayo wahenga wametuusia.

Asante sana.

Share:

5 comments

 1. MAWENI 11 Januari, 2018 at 22:42

  Hi li neno uwaafrika ndio ulotumiwa na waanzishi wa African Assocition katika miaka khamsini ambao viongozi wake wengi walikuwa wageni na ni watu wa kanisa karne ilo pita .Asasi yake ubaguzi dhidi ya Wazanzibari. Neno Uzanzibari lina pigwa vita mpaka leo, tena kwa ujahili wao hao walio rithi ideology hiyo kwao wao muafrika ni mwenye rangi yangozi nyeusi tu.Chuki tu. Wana sahau kuwawao waislamu. Tujigomboe kifra za kibaguzi , Dio tutaweza khigombowa Zanzibar kutoka ukoloni wa Tangangika. K
  Wa Zambia wana jiita wa kwa jinana la nchi yao Zambabwe hivyo hivyo. Wa Ethopia , Nigeria , Tunis , masri , Kenya , Ghana na kdhalika .
  Tuwe wazanzibari wazalendo. “Mpinduzi” nisomo kubwa kwa Zanzibari kujifunza kwa kosa kubwa lilo tendwa kwa mustskbali wa n hi yetu.

 2. Ashakh (Kiongozi) 12 Januari, 2018 at 08:09

  Kwanza tukubali Muarabu ameshaondolewa au bado wapo Waarabu?
  Pili tujitambue sisi ni nani, ni Waafrika, Waarabu au Wazanzibar?

  Tatu, lazima lazima lazima tulegeze misimamo yetu. Vyovyote itakavyoitwa iwe Mapinduzi au Mavamizi, hawa jamaa kwao wao wanafanikiwa. Kwetu sisi tunakhasirika.

  Hebu tuamke, let us think ahead of them. Mwanzo wakituaminisha kwa maneno, muda wote wakipanda mche, sasa ushamea na kuzaa. Sio Wazanzibar tena wanaoendesha nchi yao.

  Tuzaeni fikra za kujikomboa kuliko kubaki kutafuta uhalali na ukharamu

 3. Ghalib 13 Januari, 2018 at 23:15

  Sisi ni wazanzibari, hakuna muarabu, hakuna muafrica wala muhindi wala wachina, kama ulikuwa na vizazi visivyo pungua vitatu ndani ya Zanzibar wewe ni Mzanzibari halisi, haijalishi ethic yako. Hivyo kama wazanzibari maslahi yawe kwa wazanzibari wote na ndio agenda ya mapinduzi, wote sawa, sisi wazanzibari tabia na tradition yetu sawa, ndio maana tukaitwa wazanzibari, uzalendo kwanza, mapinduzi kwanza tuanze ya fikra, ule uwafrica uondoke, Uje uzanzibari.. Naamini mkoloni ataondoka tu

Leave a reply