Habari

Asimamishwa kazi kwa kumtelekeza Mjamzito

NOVEMBER 10, 2017 BY ZANZIBARIYETU

NA ABDI SHAMNAH

MKUU wa Wilaya ya Magharibi ‘A’Unguja, Kapteni Khatibu Khamis, amemsimamisha kazi mfanyakazi wa kituo cha afya Selem, Fatma Ali Khamis, kwa kushindwa kuwajibika akiwa mtumishi wa umma.

Inadaiwa mtumishi huyo anaefanya kazi kitengo cha ukunga, (PHNB), Jumatatu wiki hii saa 8.00 mchana, bila kujali aliondoka kazini na kumuacha kituoni mama mjamzito Nezuma Khamis Juma, aliefika kwa ajili ya kujifungua.

Akizungumza na waandishi wa habari, alisema mfanyakazi huyo amesimamishwa kazi kuanzia leo, huku uchunguzi kuhusiana na kadhia yake ukiendelea.

Alisema katika hatua za awali, mtuhumiwa huyo amemuamuru kufika ofisini kwake na kumuhoji na kutoa maelezo ambayo hayakumridhisha.

Alisema kutokana kuwepo taarifa kwa baadhi ya wafanyakazi wa vituo mbali mbali vya afya ndani ya wilaya hiyo, ikiwemo Selem, kuwa na tabia ya kudharau wagonjwa, amelazimika kumsimamisha kazi ili kupisha uchunguzi.

Aidha alisema endapo itathibitika kuwa mfanyakazi huyo alitenda kitendo kinyume na sheria za utumishi, hatua za kumfukuza kazi zitachukuliwa.

Alieleza kuwa kituo kingine kinachotuhumiwa kuwa na wafanyakazi wenye utamaduni wa kudharau wagonjwa ni Kizimbani.

“Tayari kuna mfanyakazi kwenye kituo hicho nina taarifa zake za kuwadharau wagonjwa, nimeshamtumia salamu kupitia sheha wa shehia hiyo,” alisema.

Alisema kitendo kilichofanywa na mfanyakazi huyo hakikuwa cha kiungwana kwani kulikuwa na uwezekano mkubwa wa mama huyo kupoteza maisha pamoja na mtoto alieko tumboni, kutokana na dharau za mtumishi huyo.

Nae, mmoja ya wafanyakazi wa kituo hicho, ambae hakupendwa kutajwa jina lake,alisema siku ya tukio hilo alifika mjamzito huyo akiwa ameongozana na jirani yake alietambulika kwa jina la Asha Juma, kwa ajili ya kupata huduma za kujifungua.

Alisema wakati alipofika kituoni, mkunga huyo (mtuhumiwa), alikuwa ametoka nje ya geti la kituo, takriban nyumba ya nne kutoka hapo kwa ajili ya kupata chakula (chips).

Hata hivyo, alisema alilazimika kuchukua juhudi za kumfuatilia mkunga huyo ili arudi kituoni haraka kumhudumia mama mjamzito, kwa kigezo kuwa alikuwa ni mkunga pekee siku hiyo kituoni hapo.

“Nilimfuatilia kule kwa muuza chips, lakini nilipofika kwa yule kaka anaeuza, alienieleza tayari ameshakula na ameondoka kuelekea kituo cha daladala kwa ajili ya kupanda gari,” alisema.

Shuhuda huyo aliendelea kueleza kuwa alilazimika kumkimbilia kituo cha daladala na baada ya kumuona alipiga mayowe kumuomba amsubiri kwa vile alikuwa na ujumbe muhimu.

“Nilimkuta pale kituoni anasikiliza simu, aligeuza uso na kuniona, lakini wala hakushituka, alipomaliza kusikiliza simu nilimtaka arudi kituoni kwani kuna mjamzito anahitaji hudum za haraka muda huo, lakini akanijibu yeye hawezi kurudi maana amefiliwa na anaenda zake,” alisema.

Shuhuda akabainisha, “nilimsihi sana arudi ili akamsaidie yule mjamzito kituoni, lakini alisisitiza yeye hawezi kurudi na kutaka ahudumiwe na wafanyakazi waliopo, il-hali akijuwa fika kuwa hakukuwa na mkunga mwengine pale kituoni”, aliongeza.

Shuhuda anasema alilazimika kurudi kituoni na kumuomba radhi yule mjamzito na jirani yake na kuwataka kurudi nyumbani kufanya utaratibu wa kutafuta usafiri wa kuwafikisha Hospitali ya Mnazimmoja.

Aidha, anasema alitoa taarifa kwa mmoja wa kiongozi wa kituo hicho, aliekuwa katika mafunzo Mjini.

Shuhuda anabainisha kuwa taarifa zilizowafikia baadae ni kuwa mjamzito yule alifika mjini salama na kwa bahati njema akajifungua salama na hali yake inaendelea vyema.

Katika hatua nyengine, shuhuda alisema mfanyakazi huyo, mtoto wa aliekuwa Spika mstaafu Ali Khamis, alihamishiwa kituoni hapo yapata miezi mitatu iliopita, akitokea kituo cha afya Fuoni Kibondeni, na kubainisha kuwa katika kipindi chote hicho amekuwa akifanyakazi bila ya ushirikiano na wafanyakazi wenzake, kiasi ambacho amekataa hata kuwapatia namba yake ya simu.

Juhudi za kumpata mfanyakazi huyo ziligonga mwamba, baada ya mwandishi wa habari hizi kumtafuta kwa njia ya simu mara kadhaa, na kuiacha simu yake ikiita mfululizo bila kupokelewa.

Zanzibar yetu

Share: