Habari

Askofu Bagonza: Muswada wa vyama vya siasa ni wa msajili si wa wananchi

Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kimewakutanisha wadau mbalimbali kuujadili muswada wa marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa wa mwaka 2018 huku wakili maarufu, Harold Sungusia akihofia msajili kuwa na madaraka makubwa kuliko rais.

Anaripoti Faki Sosi – MwanaHALISI
Jumamosi, Januari 12, 2019

ASKAFU Benson Bagonza amesema kuwa muswada wa sheria ya vyama vya siasa siyo kwa ajili ya vyama vya siasa wala wananchi ni wa msajili wa vyama vya siasa.

Akichangia hoja kwenye mjadala wa Muswada wa Sheria hiyo ulioandaliwa na Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS). “Kwa nilivyousikiliza huu Muswada nimegundua kuwa siyo kwa ajili ya vyama vya siasa wala wananchi. Upo kwa ajili ya kumpa nguvu na mamlaka makubwa msajili wa vyama vya siasa,” amesema Askofu Bagonza.”

Askofu Bagonza amesema kuwa muswada huo umemtanabaisha msajili wa vyama vya siasa kuwa kama Malaika ambaye hakosei.

“Muswada huu umempa mamlaka makubwa msajili ambapo unamuona kama Malaika ambaye hakosei wakati yeye ni binaadamu,” amesema Askofu Bagonza.

Naye, Katibu wa Jumiya ya Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda akiachangia hoja kwenye muswada huo amesisitiza uadilifu kwa viongozi wa umma kwa kutengeneza sheria zinazolenga kuwasaidia wananchi sio sheria zitakazo wasaidia wao kwenye maslahi yao.

Mchambuzi wa Masuala ya Siasa Dk Lwaitama amekionya Chama Cha Mapinduzi (CCM) waache kujiita chama tawala kutokana na dhana ya utawala inakwenda sambamba na ukoloni.

“Kutawala ni kitendo cha kuwangia watawaliwa kile anachotaka mtawala ndiyo maana tunasema Mjerumani alitawala Tanganyika,” amesema Dk Lwaitama.

Amesema Muswada umempa msajili wa vyama vya siasa mamlaka makubwa ambapo anawezi kuingia mambo ya ndani ya vyama vya siasa.

Dk Lwaitama amesema kuwa vifungu vya muswada huu mpya vinasura ya kulinda maslahi ya chama fulani ambapo anaona kuwa msajili wa vyama vya siasa anaweza kuamua afute chama fulani kwa namna yeye atakavyoona.

Amesisitiza kuwa maendeleo na Demokrasia vinakwenda sambamba ambapo haoni sababu ya kutungwa kwa sheria itakayotoa upendeleo upande mmoja.

Wakati huo huo, Mwandishi wa Gazeti la Mwananchi, Elias Msuya, kufuatia mjadala uliyoandaliwa na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), amemnukuu Wakili Sungusia katika taarifa yenye kichwa cha habari Wakili ahofia Msajili kuwa na madaraka makubwa kuliko rais.

Wakili maarufu nchini, Harold Sungusia amesema Muswada wa sheria ya marekebisho ya sheria ya vyama vya siasa wa mwaka 2018 ukipita kuwa sheria, msajili atakuwa na madaraka makubwa kuliko hata Rais.

Amesema madaraka ya msajili wa vyama vya siasa yatamfanya msajili kuwa na madaraka makubwa kuliko Rais wa Jamhuri ya Muungano, huku pia akihoji kinga atakayopewa ya kutokushitakiwa.

Akizungumza leo Jumamosi Januari 12, 2019 katika mjadala wa wazi ulioandaliwa na Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), jijini Dar es Salaam, Sungusia amesema muswada huo unapora madaraka ya wananchi kikatiba.

“Msajili anaweza kuamua usajiliwe au usisajiliwe, ufutwe au usifutwe, uwe mwanachama au sio, unafaa kuwa mgombea au hufai, aina gani ya elimu ya uraia inayotakiwa na nani atoe, upewe ruzuku au usipewe,” amesema Sungusia.

“Je, akimfuta uanachama Rais? Yaani msajili ana mamlaka kuliko Rais. Ni jambo kubwa la kikatiba,” amesema Sungusia.

Ameendelea kutaja kifungu cha 6 kinachompa kinga msajili, Sungusia amesema kwa sheria ya sasa angeweza kushtakiwa kwa makosa ya uzembe lakini kwa muswada mpya hashtakiwi kabisa. “Kinga lazima iendane na katiba na haki za binadamu,” amesema Sungusia.

Akizungumzia utungwaji wa kanuni, Sungusia amehoji uhalali wa waziri huyo. “Waziri anatoka wapi, chama gani?

Mnakumbuka kikokotoo, Waziri alitakiwa kutunga kanuni na akatunga kweli. Ukimwachia mwanafunzi atunge kanuni atafanyaje?” Amehoji

Kuhusu vyama vya siasa kutofanya harakati, Sungusia amesema hata chama cha TANU kilifanya harakati hadi uhuru ukapatikana.

“Sasa vyama vitakuwa kwaya za siasa. Kazi ya chama cha siasa ni kuchukua madaraka, huchukui madaraka kwa kuimba pambio. Hata TANU waliwashinikiza Wazungu wakatoa madaraka,” amesema Wakili Sangusia.

Baadhi ya wanajopo waliojadili sheria hiyo akiwemo Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Karagwe mkoani Kagera, Benson Bagonza amesema muswada huo hauakisi matakwa ya vyama vya siasa bali ya msajili.

“Muswada una ujasiri mkubwa wa kuingilia haki za wengine. Kuna hatari ya kujenga mazoea ya kuwa na ujasiri wa vyombo vingine kuingilia haki za wengine.”

“Maana msajili amepewa haki, kama utapita kuna siku vyombo vingine vitaingilia haki ya kuabudu,” amesema Askofu Benson.

Share: