Habari

Atakaye muingilia mgonjwa wa akili kukiona

February 9, 2018

. Wapinga mapinduzi waandaliwa adhabu ya saizi yao

NA HAFSA GOLO

MKURUGENZI wa Mashtaka (DPP) Ibrahim Mzee, amesema muswada wa sheria mpya ya adhabu ya mwaka 2018, una umuhimu mkubwa kwa sababu unalinda amani na usalama wa nchi.

Alieleza hayo katika semina ya siku moja kwa wajumbe wa baraza la wawakilishi, kuhusu miswada miwili ya sheria inayotarajiwa kujadiliwa na kupitishwa katika mkutano wa tisa wa baraza hilo.

Alisema sheria hiyo ndio sheria mama kwa Zanzibar ambayo imebeba sheria nyengine zote hasa ikizingatiwa hakuna kosa lolote la jinai litakalopatiwa hatia bila ya kutajwa ndani ya sheria.

Alisema sheria hiyo imetaja adhabu za makosa mbalimbali ya jinai ikiwemo kifo na kifungo cha maisha.

Alisema makosa hayo yameainishwa katika vifungu 397 vya sheria hiyo yenye sehemu 40 na jaduweli moja.

Alitaja sehemu ya sita ya sheria kwa makosa dhidi ya serikali ni mokosa ya uhaini na kupanga kupinga mapinduzi ya mwaka 1964 ambapo adhabu zake ni kifo.

Alisema mambo mengine yaliomo ndani ya sheria hiyo ni pamoja na makosa ya kumuingilia mgonjwa wa akili na adhabu yake ni kifungo cha maisha na kwa mwenye kujaribu kufanya kitendo hicho adhabu yake ni kutumikia kifungo cha miaka 30 jela.

Alisema muswada huo pia umezungumzia makosa ya kuua bila kukusudia, kuua kwa makusudi na makosa mengine yenye kulingana na jinai hivyo adhabu zake zimependekezwa kifo, kifungo cha maisha na miaka saba.

Alisema muswada huo umezungumzia maeneo mengine mapya ya kisheria ambayo awali hayakugusiwa moja kwa moja katika sheria ikiwemo suala la unyanganyi kwa kutumia silaha.

Alisema sehemu ya 36 imebainisha kuhusu alama za biashara huku kifungu cha 387 hadi 389 kinaeleza jinsi raia anavyopaswa kufanya na kufuata taratibu za nchi.

Zanzibarleo

Tagsslider
Share: