Habari

AZAM TV YAAHIDI KUENDELEZA MASHIRIKIANO NA TAASISI YA RAFIKI NETWORK

Na Ali Othman Ali
Afisa Mkuu wa Utendaji (CEO) wa Azam Media Limited Bwana Tido Mhando ameahidi kuendeleza mashirikiano na Taasisi ya Rafiki network katika kuandaa na kusimamia matukio mbali mbali yenye lengo la kuboresha hali za watu hapa nchini.
Bwana Mhando ameyasema hayo leo wakati alipotembelewa na uongozi wa Taasisi ya Rafiki Network katika ofisi za Azam TV zilizopo Tabata, Barabara ya Mandela jijini Dar es Salam.
Akitoa tathmini ya Tamasha la kimichezo lililofanyika Kisiwani Pemba hivi karibuni Bwana Mhando amesema hawakutegemea kamwe kuwa Bonanza lingekua kubwa na lenye mvuto kwa wenyeji na wageni na hivyo hawakujiandaa vya kutosha kukabiliana na hali hiyo.
Wakati huo huo Mkurugenzi Mtendaji wa Azam TV Bwana Yahya Mohammed Kimaro ameipongeza Taasisi ya Rafiki Network kwa ubunifu na ameahidi kuendeleza mashirikiano hayo na Taasisi hiyo kwa kurusha hewani matamasha mbali mbali yatakayoandaliwa na taasisi hiyo.
Nae Raisi wa Taasisi ya Rafiki Network Bwana Hamad Omar Hamad amemkabidhi cheti Cha Shukrani Mkuu wa Utendaji wa Azam Media Limited Bwana Tido Mhando ikiwa ni ishara ya kuthamini juhudi za Shirika hilo la Utangazaji katika kufanikisha Bonanza la kihistoria lilofanyika kisiwani Pemba hivi karibuni.
Taasisi ya Rafiki Network itaandaa Tamasha Maalumu la Funga mwaka ambalo linatarajiwa kufanyika kisiwani Unguja kuanzia Disemba 29 hadi 31 ambapo katika mwaka 2018 tamasha kubwa lenye hadhi ya kimataifa lijulikanalo kama Pemba International Weekend Bonanza litafanyika Kisiwani Pemba.

Raisi wa Taasisi ya Rafiki Network Bwana Hamad Hamad (kulia) akimkabidhi Cheti cha Shukran Afisa Mkuu wa Utendaji (CEO) wa Azam Media Limited Bwana Tido Mhando (kushoto) huko katika ofisi za Azam TV zilizopo Tabata, Barabara ya Mandela jijini Dar es Salam.

Afisa Mkuu wa Utendaji (CEO) wa Taasisi ya Rafiki Network Bwana Yussuff Hamad (kushoto), Mkurugenzi Mtendaji wa Azam TV Bwana Yahya Mohammed Kimaro na Raisi wa Taasisi ya Rafiki Network Bwana Hamad Omar Hamad (kulia) wakiwa katika ofisi za Azam TV zilizopo Tabata, Barabara ya Mandela jijini Dar es Salam.

Share: