BarazaBarazaniHabari

Baadhi ya watumishi Zanzibar hawana uwezo

Salma Said, Zanzibar
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imetakiwa kupunguza watumishi katika baadhi ya tasisi za umma kutokanana na wengi wao kutokuwa na taaluma kuhusu kazi walizopangiwa.

Kauli hiyo ilitolewa na mwakilishi wa jimbo la Chake Chake Omar Ali Shehe wakati akichangia ripoti ya kamati ya katiba na sheria ya barza la wawakilishi kuhusu utekelezaji wa maagizo ya kazi kwa Wizara ya Nchi Ofisi ya rais- Utumishi na Utawala bora mwaka 2012/2013.

Alisema katika utekelezaji wa mpango huo serikali inaweza kushirikiana na wahisani watakaosaidia kulipa mafao ya wafanyakazi watakaopunguzwa ili kupunguza wafanyakzi ambao ni mzigo kwa serikali.
“Kwanini serikali iendelee kubeba mzigo mkubwa wa wafanyakazi ambao hawana utalaamu. Ni vyema serikali ikawa na wafanyakazi wenye taaluma na kazi wanazozifanya ili kuleta ufanisi,” alisema Shehe ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya ukaguzi wa mahesabu (PAC).

Aidha mwakilishi huo aliungana na wajumbe wengine katika baraza hilo kuiomba serikali kuongeza mishahara ya watumishi wa umma katika bajet ijayo ya mwaka wa fedha 2013/2014 ili kuwawezesha kumudu maisha yao.

Shehe and Mwakilishi wa Jimbo la Mjimkongwe kupitia chama cha CUF Bw Ismail Jussa Ladu walisema uwezo wa serikali wa kuongeza maslahi kwa wafanyikazi wao ni mkubwa hivyo ni vyema kuongeza mishahaa inayolingana na gharama za maisha .

“Kwa uchache, mfanyakazi mwenye familia ndogo sana, anatakiwa apate elfu 20 kwa siku, lakini inasikitisha kuwa serikali inawalipa wafanyakazi wake chini ya elfu 10 kwa siku. Hali hii inasababisha rushwa,” alisema Jussa.

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inakadiriwa kuwa na watumishi zaidi ya 38 elfu nusu yao wanadaiwa hawana taluma za kazi wanazozifanya.

Share: